[ATTACH=full]470192[/ATTACH]
Jina la Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo libarikiwe, karibu tujifunze biblia…
Vipo vipindi viwili vya Bwana Yesu kutuita katika maisha yetu.
Hebu tujifunze namna alivyowaita wanafunzi wake mara ya kwanza na mara ya pili, ili itusaidie na sisi kujua jinsi wito wa Mungu ulivyo…
Mara ya kwanza Bwana Yesu aliwaita wanafunzi wake kipindi wapo katika shughuli zao, ndio hapo utaona anamfuata Petro na Adrea kuwaambia wamfuate (Mathayo 4:19), baadaye tena anamfuata Mathayo katika shughuli yake ya utoza ushuru na kumwambia nifuate (Mathayo 9:9). Lakini katika wito wote wake huo, hakuwapa masharti yoyote magumu wanafunzi wake… wengi wao aliwapa maneno ya faraja tu kuwa “watakuwa wavuvi wa watu badala ya samaki”.. wengine waliambiwa wataona mbingu zikifunguka na malaika wakishuka na kupanda juu ya Mwana wa Adamu (Yohana 1:51).
Kwahiyo wito wa kwanza kwa ufupi ulikuwa ni wito wa faraja na wa matumaini, haukuwa wito wa Masharti…
Lakini tunapokuja katika wito wa pili, tunaona Bwana Yesu akizungumza maneno mengine ambayo ni magumu kidogo… Tunaona anawaita tena kwa mara ya pili: Na wakati huu hawabagui tena kama alivyofanya hapo kwanza… kwamba anakwenda mahali Fulani na kumtafuta Petro na Adrea peke yao!, na kuacha watu wengine, au anakwenda Forodhani na kumchagua Mathayo peke yake !, na kuacha watoza ushuru wengine…
Bali tunaona wakati huu wa pili, anawaita watu wote kwa pamoja, bila kubagua yule ni wanafunzi wake au sio wanafunzi wake, na kuwaambia maneno mengine mapya… Na maneno hayo tunayasoma katika mstari ufuatao…
[INDENT]Marko 8:34 “Akawaita mkutano pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, Mtu ye yote akitaka kunifuata na ajikane mwenyewe, ajitwike na msalaba wake, anifuate”[/INDENT]
Mara ya kwanza Bwana Yesu hakutoa uhuru wa mtu yeyote kumfuata, yeye ndio alikwenda kuwatafuta akina Petro, na kuwachagua watembee naye… Lakini mara hii ya pili, ANATOA NAFASI KWA WOTE! (wakike au wa kiume, awe mdogo au mkubwa, awe mlemavu au mzima).. na anawaambia wote (Mitume pamoja na Makutano). Kuwa mtu yeyote akitaka kumfuata, “AJIKANE MWENYEWE, AJITWIKE MSALABA WAKE AMFUATE”.
Wito huu wa pili ni kama unaufanya ule wito wa kwanza usiwe na nguvu tena!!.. Kwasababu hapa Bwana Yesu anawaita wote(wanafunzi wake pamoja na watu wa mataifa)… Pengine wakina Petro walingetemea maneno hayo waambiwe wakutano tu!, lakini wanashangaa na wao wanajumuishwa huko huko…
Wote wanapewa agizo moja! Bila upendeleo… Maana yake ni kwamba pia alitoa mlango wa mtu yeyote kuondoka kama anataka kuondoka, haijalishi tayari alikuwa ameshaitwa hapo kwanza, haijalishi kama alikuwa tayari ameshapewa ahadi na Bwana…
Tunaweza kulithibitisha hilo katika…
[INDENT]Yohana 6:66 “Kwa ajili ya hayo wengi miongoni mwa wanafunzi wake wakarejea nyuma, wasiandamane naye tena.
67 Basi Yesu akawaambia wale Thenashara, JE! NINYI NANYI MWATAKA KUONDOKA?
68 Basi Simoni Petro akamjibu, Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele.
69 Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu”[/INDENT]
Umeona hapo?.. Yule Petro ambaye aliitwa hapo kwanza kwa wito wa faraja, safari hii Bwana anamwuliza “JE UNATAKA NA WEWE UNATAKA KUONDOKA??”, anamwuliza pia na Nadhanieli ambaye aliambiwa ataona malaika wakipanda na kushuka juu ya mwana wa Adamu, “JE UNATAKA NA WEWE UNATAKA KUONDOKA??”, maana yake ni kwamba kama wangetaka kuondoka, basi mlango upo wazi Bwana angewaruhusu wala asingembembeleza… Na ahadi zile alizowaahidiwa Bwana angewapa wale waliokuwa tayari. (Hii inaogopesha sana!!).
Ndugu inawezekana kipindi unasikia wito wa Mungu kukuita ulikuwa unapokea maneno ya faraja kutoka kwa Bwana Yesu, na kujiona wewe ni wa kipekee sana…huenda Bwana Yesu alikwambia wazi kabisa kuwa utakuwa mtumishi wake na utawavuta wengi kwake na utakuwa Baraka kwa maelfu ya watu…
lakini nataka nikuambia kuwa “usibweteke na wito huo wa kwanza wa faraja”…”utendee kazi wito wa pili” Kwasababu hata Petro na Yohana waliambiwa hivyo hivyo, hata Nadhanieli mara ya kwanza aliambia maneno ya faraja kama yako!..lakini baadaye Bwana Yesu aliwageukia na kuwaambia kuwa “Mtu ye yote akitaka kunifuata na ajikane mwenyewe, ajitwike na msalaba wake, anifuate”…Na Bwana Yesu aliwaweka kundi moja na makutano kana kwamba hakuwahi kuwaita huko nyuma… Kana kwamba siku hiyo ndio aliyokuwa anawaita kwa mara ya kwanza.
Ndugu yangu, huenda ulishausikia wito wa Kwanza, na sasa upo katika wito wa pili, Amua leo kumfuata YESU upya kwa kujikana nafsi!!.. Wakina Petro, baada ya kusikia hayo maneno ndipo walipojijua kuwa wanapaswa wahakiki wito wao upya!.. Ndipo wakaamua kujikana nafsi kweli kweli na kumfuata Yesu.
Na wewe leo, achana na ukristo vuguvugu wa kujisifia maono au karama, anza kujikana nafsi na kubeba msalaba wako, kaa mbali na dhambi na ulimwengu, kwa kadiri uwezavyo, weka chini fasheni za kidunia ambazo hazimpi Mungu utukufu, acha kuvaa kikahaba, acha kuweka wigi kichwani, acha kuweka hereni na mikufu, na kuvaa nguo za kubana…ni machukizo kwa Mungu (1Timotheo 2:9), acha kuabudu sanamu, acha kufanana na watu wa ulimwengu huu….hata kama dunia nzima itakuona umerukwa na akili, hata kama ndugu na wanadamu watakwona umechanganyikiwa… wewe mfuate Yesu, na udunia uweke nyuma, na siku ile utapokea Taji ya uzima.
Kumbuka siku zote kuwa “waitwao ni wengi, bali wateule ni wachache”(Mathayo 22:14).
Tujitahidi tuwe wateule wa Bwana Yesu.
Bwana akubariki.
Maran atha!
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;