Tanzania Mercantile Exchange (TMX) Yauza Korosho Tani 147,410 Katika Minada iliyofanyika Mtwara (Warehouse Receipts Imeondoa walanguzi wa Kenya)

Mkoa wa Mtwara umeweka rekodi nyingine katika mauzo ya zao la korosho baada ya kuuza zaidi ya tani 147,410 kupitia minada sita iliyofanyika mpaka sasa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX).

Kaimu Mrajis Msaidizi wa Mkoa wa Mtwara Bw.Robert Nsunza amesema haya wakati aliposhiriki mnada wa tatu wa mauzo ya Korosho kwa MAMCU LTD uliyofanyika katika halmashauri ya wilaya ya Masasi, ‘Vyama vikuu vya ushirika TANECU na MAMCU kwa pamoja vimeshuhudia mafanikio makubwa kwa kufikisha sokoni jumla ya tani 147,410 za korosho katika minada iliyofanyika hadi sasa’

Kwa mujibu wa Nsunza anasema MAMCU katika minada yake mitatu imeuza tani 82,000 huku TANECU ikiuza tani 65,000 kupitia minada mitatu iliyofanyika chini ya mfumo wa kidijitali wa TMX.

Amebainisha kuwa wakulima wote tayari wamelipwa fedha za mnada wa kwanza na malipo ya mnada wa pili yakiwa yamemalizika isipokuwa kwa baadhi ya AMCOS chache zikiliwa zinamalizia kulipa wakulima, hatua iliyowatoa wasiwasi wakulima wengi wanaohitaji kupata haki zao kwa wakati.