KISA CHA MWANA KONDOO.
1)Kondoo kavua gamba,twamwona kumbe ni nyoka
Kondoo sasa atamba,nasi twazidi nyooka
Kondoo huyu ni simba,wengi chini wadondoka
Tusingefanya makosa,laiti tungelijua.
2)Kondoo ananguruma,hata hovyo aropoka
Kondoo anatuuma,kimya chozi latutoka
Kondoo anajituma,hajui anapotoka
Tusingefanya makosa,laiti tungelijua
3)Kondoo atukomoa,kimoyomoyo acheka
Kondoo kumkosoa,jambo lisopendezeka
Kondoo akikujua,si ajabu kutoweka
Tusingefanya makosa,laiti tungelijua
4)Kondoo anachukia,kwa mabaya kusemeka
Kondoo afurahia,watu wakitetemeka
Kondoo ajitambia,kwa maovu kutendeka
Tusingefanya makosa,laiti tungelijua.
5)Kondoo kitu libabe,kimya kimya lilizuka
Kondoo kupata shibe,mbuzi akawageuka
Kondoo ni tupu debe,kwa uozo ananuka
Tusingefanya makosa,laiti tungelijua
6)Kondoo mpenda vitu,kule kwao kupeleka
Kondoo binafsi jitu,kifikra limezeeka
Kondoo hili si kitu,kinafki lapenda Cheka
Tusingefanya makosa,laiti tungelijua
SHAIRI- KISA CHA MWANA KONDOO.
MTUNZI-Idd Ninga,Tengeru Arusha
+255624010160
[email protected]
TANBIHI: Ni utunzi hauna mahusiano na tukio lolote la kweli.