Leo tutaona kibiblia ni kwanini uuthamini mkesha wako wa kuingia mwaka mpya. Wengi wetu tunapuuzia, tunaona ni jambo la kawaida tu, na hivyo tunautumia msimu huu pengine kulala, au kwenda kufanya anasa, au kwenda kufanya part na ndugu au marafiki n.k… Ni heri upange kwenda kusheherekea nao siku inayofuata kuliko siku ya mkesha wa kuukaribisha mwaka mpya.
Lipo jambo kubwa sana la kiroho katika usiku wa siku hiyo.
Ukisoma biblia utaona Mungu alipokuwa anawatoa wana wa Israeli Misri, siku hiyo kwao ndio ilikuwa siku ya kwanza ya mwaka wao mpya… Lakini utaona Mungu hakuwatoa mchana, au jioni, au alasiri bali aliwatoa usiku wa manane, Sio kwamba mchana wasingeweza kusafiri, hapana, lakini siku ya kutengwa na maadui zako, na siku ya kuukaribisha mwaka mpya sikuzote ni lazima maandalizi yaanzie angali bado kuna giza nene.
Utasoma usiku ule kabla ya kuamkia tarehe moja, walimla yule pasaka(mwanakondoo), wakiwa wamevaa viatu vyao chini, kiashirio kuwa wapo mbali na vitanda vyao, na huku wamefunga mikanda yao viunoni, kuashirio kuwa wapo tayari kwa safari, kisha wamejifungia ndani wakimtafakari Mungu na kumwimbia, wakisubiria tu muda ufike wa kuondoka…
[INDENT]Kutoka 12: 11 “Tena mtamla hivi; mtakuwa mmefungwa viuno vyenu, mmevaa viatu vyenu miguuni, na fimbo zenu mikononi mwenu; nanyi mtamla kwa haraka; ni pasaka ya Bwana.
12 MAANA NITAPITA KATI YA NCHI YA MISRI USIKU HUO, NAMI nitawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, wa mwanadamu na wa mnyama; nami nitafanya hukumu juu ya miungu yote ya Misri; Mimi ndimi Bwana”.[/INDENT]
Kwasababu walifahamu wanaingia katika mwaka wao mpya wa kufanywa huru mbali na maadui zao. Sasa embu fikiria kama wangekuwa wamelala, halafu asubuhi ndio wanaamka watake kuondoka Misri, hali ingekuwaje? Ni wazi wasingetoka kwa ushindi mnono kama walivyotarajia.
Vivyo hivyo na sisi, siku kama ya leo, ndio tunavuka kuingia mwaka mpya. Usiku ambao tunayaacha mambo ya mwaka huu, na kuyakaribisha mambo ya mwaka mwingine mpya, Hivyo kama tunataka Mungu ampige adui yetu shetani kwelikweli, ili mwaka wetu mpya tunapouanza uwe wa kuwa huru, na wa Baraka nyingi na wa mafanikio, hatuna budi leo kukesha nyumbani mwake, katika kuomba, kumwabudu na kumfanyia ibada.
Yaani tarehe moja ya mwaka mpya isikukute upo kitandani, isikukute unaangalia MUVI, isikukute unacheza gemu, isikukute unazurura zurura mtaani, isikukute unapiga piga stori na marafiki zako n.k., bali ikukute nyumbani mwa Bwana unamshukuru na kumtukuza.
Hata kama upo katika nchi ambazo, ibada zimekatazwa makanisani, bado unayo nafasi ya kujifungia mwenyewe nyumbani na familia yako ukawa unaomba na kumshukuru Mungu, kama wana wa Israeli walivyofanya. Hakikisha kuwa mwaka wako mpya unaukaribisha ukiwa macho kwa Bwana.
https://wingulamashahidi.org/wp-content/uploads/2020/12/clock-midnight.jpg
Itakuwa ni ajabu sana, kama mwaka huu utashindwa kumshukuru Mungu kwa wema wake aliokutendea mwaka mzima…Wewe mwenyewe unajua mambo tuliyoyapitia mwaka huu jinsi yalivyokuwa mazito , lakini umepewa neema ya kuyavuka, ujue sio kwa nguvu zako,wala fedha zako, wala afya yako wala chochote ulicho nacho.
Hivyo utumie mkesha huu, vema kwasababu hakutakuwepo tena na mwingine kama huu, kwa miezi mingine 12 ijayo. Bwana akubariki
Pia wakumbushe na wengine, jambo hilo. Na shea kwa wengine.
Mwisho kabisa, nikutakie HERI YA MWAKA MPYA WENYE MAFANIKIO YOTE YA MWILINI NA ROHONI KATIKA JINA LA BWANA YESU KRISTO.
AMEN.