Maelekezo kwa wananchi wote wa tanzania. Udikteta unaposhika kasi! by Zito Zuberi Kabwe

Nini kifanyike Tanzania?

Na Zitto Kabwe

Hali yetu ya sasa

Ni dhahiri kuwa hofu imetanda miongoni mwa Watanzania. Ingawa watawala na mashabiki wao hukanusha jambo hili, ukweli ni kuwa nina amini wao wenyewe ndani ya mioyo yao wanakiri kuwa nchi sasa inaendeshwa kwa hofu na wananchi wamejaa hofu kubwa.

Hivi sasa mwananchi akifanya jambo lolote linaloonekana kuwa kinyume na fikra za watawala, wenzake wanamtazama kwa jicho kuwa atakuwa mhanga wa vitisho, mateso, kutekwa, kupotea ama kubambikiwa kesi.

Hakika jamii iliyojaa hofu haiwezi kuwa jamii huru na kamwe haiwezi kupata maendeleo.

Hofu hii iliyotamalaki imekomazwa na matendo ya utawala kukandamiza uhuru wa watu kujieleza, kupata/kupasha habari, kukusanyika na kuhoji/kukosoa Serikali yao. Hizi ni haki za kikatiba ambazo wajibu wa Serikali ni kuzilinda.

Tumeshuhudia wananchi na haswa vijana wakishtakiwa mahakamani kwa makosa yatokanayo na haki yao ya kujieleza kwenye mitandao ya kijamii. Baadhi ya vijana wamehukumiwa vifungo ama kulipa faini.

Mmiliki wa mtandao wa JamiiForums, mtandao wenye kutoa mawazo huru kwa wananchi na kwa muda uliochangia kwa kiasi kikubwa vita dhidi ya ufisadi nchini, Maxence Melo bado anaendelea na kesi zilizofunguliwa dhidi yake ikiwa sehemu ya vitisho vya dola ambavyo pamoja na shauri hilo amekuwa akilazimishwa kutoa majina ya wachangiaji wa mtandao huo.

Licha ya kwamba katiba yetu inaruhusu vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara na kujitangaza, kuandikisha wanachama, kukosoa sera za Serikali na hata kueneza sera mbadala, Serikali kupitia amri isiyo ya kikatiba wala kisheria ya Rais imezuia vyama kufanya shughuli zake hizo halali.

Matamko halali kabisa ya kisiasa ya wanasiasa sasa yanachukuliwa kama ni uchochezi na watoa matamko kushtakiwa kwa makosa ya jinai ikiwemo kwa kutumia sheria mpya kandamizi ya huduma za habari (The Media Services Act 2016 ).

Tumeshuhudia wabunge wakifungwa jela kwa makosa ya matamko ya kisiasa ambayo yangepaswa kujibiwa kisiasa tu kutoka upande wa pili ( watawala ).

Hivi sasa viongozi wakuu wa vyama vya upinzani wanakwenda mahakamani kila wiki kujibu tuhuma za kisiasa, lengo likiwa ni kuwapotezea muda na kuwajaza hofu washindwe kufanya shughuli zao ipasavyo.

Utawala umeweza kusambaza hofu kwa kugusa kila kundi katika jamii. Wanasiasa wanatishiwa na kesi za uchochezi, kutekwa au majaribio ya kuuawa kwa kupigwa risasi mchana kweupe ndani ya eneo lenye ulinzi mkubwa.

Waandishi wa Habari wanatishwa kwa ama vyombo vya habari kama magazeti kufungiwa au kutekwa na kutoonekana kabisa; Wakulima bei za mazao yao zimeporomoshwa makusudi kutokana na maamuzi ya hovyo ya kisera ya Serikali; Wavuvi wanachomewa nyavu zao na mitumbu yao kuchomwa moto; Wafugaji wanaondolewa kwenye maeneo yao ya malisho ili kuanzisha ranchi binafsi na wengine kuuwawa; Wafanyabiashara wanabambikiwa kesi ama kodi kubwa ili kuwakomesha na kuweka utii kwa dola; Wanawake wanatukanwa na kudhalilishwa ikiwemo kuwanyima fursa ya kujiendeleza kimasomo watoto wa kike wanaopata uja uzito mashuleni.

Viongozi wa dini wanaojaribu kuhoji watawala wanachunguzwa uraia wao; Wanaharakati wa asasi za kijamii wanaotoa mawazo yasiyopendeza watawala wanatangazwa sio raia wa Tanzania na asasi zao kutishiwa kufutwa kwa kutungiwa kanuni kandamizi za uendeshaji wa asasi hizo.

Wananchi kwa ujumla wanaumizwa na hali mbaya ya uchumi inayotokana na maamuzi ya hovyo ya kisera ya Serikali katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo. Wananchi wa Zanzibar wamenyimwa haki ya kuongozwa na Serikali waliyoichagua katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Hakuna kundi katika jamii ambalo limebakizwa, kila kundi limeguswa.

Tunataka nini?
Kwa maoni yangu Watanzania wengi wanapenda kuwa huru; Uhuru wa Mawazo, kujieleza, kukusanyika nk. Nadhani tunataka Tanzania yenye raia wenye uhuru kwa mujibu wa Katiba. Vyama vya siasa viwe huru kufanya shughuli zao bila bugudha na kwa mujibu wa sheria, Bunge la Wananchi liwe huru kuisimamia Serikali bila kuzongwazongwa na Watendaji, vyombo vya habari viwe huru kuandika/kutangaza habari bila woga wala upendeleo; Wananchi wawe huru kuikosoa serikali dhidi ya sera zake kandamizi zinazowasokomeza kwenye umasikini, Wazanzibari wapate haki yao ya uchaguzi (electoral justice) waliyoporwa Oktoba 2015 na viongozi wa dini na asasi za kiraia wawe huru kufanya kazi zao bila vitisho. Kiufupi tunataka nchi ya kidemokrasia ambayo asasi za kidemokrasia zinatimiza wajibu wao kwa uhuru.

Tufanye nini?

Sasa wakati umefika wa kujenga mshikamano kurejesha demokrasia tuliyokuwa nayo nchini na kujenga demokrasia madhubuti ambayo haitachezewa tena na yeyote. Haitoshi kila mtu kusema lake kwa wakati wake anapoguswa na matendo ya kidikteta, tunapaswa kuwa na sauti nyingi lakini zinazoratibiwa ili kuhakikisha kuwa tunalinda haki za watu na kuhami uchumi wa nchi wetu usiendelee kuporomoka. Tunapaswa kuwa na harakati za kutetea haki za kijamii (social justice), haki za kujieleza (freedom of speech) na Demokrasia. Tunapaswa kujenga vuguvugu pana la watu a broad based popular movement) ili kuleta mabadiliko ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.

Ili kujenga vuguvugu hili ni lazima kuweka mbele maslahi mapana ya Taifa letu na kuachana na maslahi binafsi ambayo yamekuwa yakitawala siasa za Tanzania kwa miongo miwili sasa bila mafanikio ya maana. Ni lazima kukubali ukweli kuwa, kwa hali ya nchi ilivyo sasa hakuna chama kimoja pekee ama kundi la jamii moja pekee linaweza kukabili utawala dhalimu wa kidikteta uliopo nchini na kushinda. Wasioweza kuukabili ubinafsi wao kwenye mambo haya tuwaombe basi wauweke kama akiba kisha tukimaliza kazi hii ya mabadiliko waendelee nao. Kila jambo tufanyalo lazima lijibu swali ‘ hili linatusaidia kutufikisha kwenye lengo la kuondoa utawala wa kidikteta nchini?’

Ni lazima tuwe na mshikamano katika kukabili dubwana tunalokabiliana nalo. Hatupaswi kuruhusu hata siku moja ya ziada baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 tukiwa na ‘regime’ hii tuliyonayo sasa.

Hili ni jambo linalowezekana iwapo tutakuwa na mshikamano madhubuti bila kujali vyama vyetu vya siasa.

Watanzania wapo tayari, wanapaswa kuongozwa tu. Uongozi huu ni lazima uwe na watu wasiopenda yanayoendelea nchini ndani ya watawala, walio nje ya watawala, Wafanyakazi, Wakulima, Wavuvi, Wafugaji, Vjana, Wanawake, Wafanyabiashara, wana harakati na kila mtu anayetaka Tanzania na Zanzibar zilizo njema zenye Uhuru na Demokrasia.

Tunaweza tukiamua. Haya #twenzetu tukaunde vuguvugu hili kuanzia mitaani tunamoishi, vijijini na mijini.

Dar Es Salaam
5/11/2018

Tanzania yangu kwa sasa inasikitisha sana

So sad to see WWMD turn into this.

Mambo mengi yanasikitisha sana…

Ila ndiyo maagizo wanayopenda kutoka juu, namna ya kupeleka mambo…

Cc: @Mahondaw

Tanzania iko kwenye hatari kubwa

Leohii jiwe kaidhirishia dunia kuwa ni yeye anayeamuru wapinzani wafungwe jela, yaani hii ya mhimili mmoja kujichimbia mzizi ndani ya mihimili mingine ni kaburi la demokrasia katika nchi yetu.