KISA CHA NGE NA MZEE.
Niwasalimu wa bush wenzangu!
MZEE mmoja aliona nge akitapatapa kuzama kwenye maji. Imani na roho ya kusaidia ikamjia, akaingiza mkono majini ili kumhami. Alipomgusa tu, nge akamgonga. Maumivu aliyoyapata, alijikuta akitoa mkono bila kumuokoa.
Pamoja na maumivu ya sumu ya nge, mzee alipotupa macho tena majini, alimwona nge akizama na kuendelea kutapatapa.
Haraka aliingiza mkono ili kumsaidia. Na kama awali, nge akamgonga tena na kumwachia maumivu makali.
Kijana aliyekuwa amesimama kando, alimuuliza mzee: “Kumradhi mzee, naona kama utadhurika bure. Hivi huoni kila unapojaribu kumsaidia, naye anazidi kukugonga?”
Mzee alijibu, “Uhalisia wa nge ni kugonga, uhalisia wangu kama mwanaadamu ni kusaidia. Uhalisia wangu wa kusaidia, hauwezi kubadilika kama ambavyo uhalisia wa nge wa kugonga usivyobadilika.”
Punde, mzee alichukua kipande cha mti, akakitumia kumuopoa yule nge na kumtoa nje ya maji. Kijana akaandoka kichwa chini, mikono nyuma.
FUNZO: Kamwe usijibadili uhalisia wako. Ukifanya ihsani ukalipwa nuksani, usibadilike.
Badala yake, chukua tahadhari kisha badili mfumo wako wa kusaidia. Hutokea kipindi mtu akakudhuru si kwa makusudi, bali kwa mapungufu yake ya kimaumbile. Kwahivyo, kulipizia uovu ni kujidhulumu nafsi na kujishushia hadhi.
Siku Njema.
Kazi ya Control + C na Control + V