Wenza wangu hamjambo, na wakuu shikamoo,
Natumai mna jambo, pia miye nina mwao,
Akilini kama chambo, nanasa nyie pomboo,
Nswi wa ziwani ndoo, tutatuwe hili jambo,
Alinaswa kwa ulimbo, huku mjini jogoo,
Tukaandaa na tembo, ifike mtondogoo,
Tukapenga hino bimbo, lipojua kumbe koo,
Nswi wa ziwani ndoo, tutatuwe hili jambo,
Sisuti yakwe urembo, akamaka eti loo!
Utanashati wa umbo, hwenda ikawa dondoo,
Bora asinende kombo, yu ngali wetu pomboo,
Nswi wa ziwani ndoo, tutatuwe hili jambo,
Alitupiga makumbo, tukawa koho kohoo,
Kisa tulijipa tumbo, kuuliza jina soo,
Akaachana na sambo, katuaga eti ‘poo’,
Nswi wa ziwani ndoo, tutatuwe hili jambo,
Najua tangu kitambo, mungwana hushika moo,
Na angatolewa bombo, hujifanya ye’ tondoo,
Na japo apawe fimbo, ni maji katika ndoo,
Nswi wa ziwani ndoo, tutatuwe hili jambo.
Malenga wa ziwa kuu