Mussa Azzan Zungu ni mwanasiasa mkongwe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye amehudumu bungeni kwa muda wa miaka 20 mfululizo, huku akijipatia heshima kubwa kutokana na uzoefu wake wa muda mrefu katika shughuli za Kibunge na utumishi wa umma.
Mussa Azzan Zungu ni Mhandisi wa ndege aliyepata mafunzo nchini Tanzania na Canada, akionyesha umahiri katika taaluma ya kiufundi kabla ya kuingia kwenye siasa.
Kwenye uzoefu wa kibunge amekuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu miaka ya 2000.
Amekuwa mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Bunge kati ya mwaka 2016 na 2025, amekuwa
Mwenyekiti wa Bunge kati ya mwaka 2012 na 2021, na pia amekuwa Naibu Spika kati ya mwaka 2022 na 2025 kabla ya kuchaguliwa kuwa Spika wa Bunge la 13.
Akiwa bungeni amewahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kwa zaidi ya miaka 16.
Mussa Azzan Zungu amewahi kufanya kazi na Maspika wanne tofauti, jambo linalompa uzoefu mkubwa wa kiutawala na Kibunge.
Kwenye uongozi wa Kimataifa, amewahi kuwa kiongozi wa Bunge la Tanzania katika mikutano ya Umoja wa Mabunge ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (ACP) pamoja na Bunge la Umoja wa Ulaya (EU).
Pia amewahi kuwa kiongozi wa Chama cha Mabunge ya Jumuiya ya Madola (CPA – Tanzania Branch) na mwakilishi wake katika vikao vya kimataifa.
Ameshiriki ziara za mafunzo ya Kibunge katika zaidi ya nchi 23, akijenga uelewa mpana wa mifumo ya Mabunge duniani.
Kwenye Serikali amewahi
kuhudumu kama Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), nafasi iliyompatia uzoefu katika masuala ya utawala wa Serikali na ushirikiano wa Muungano.
Kwa heshima na sifa binafsi, ni
mweledi wa kanuni na taratibu za uendeshaji wa Bunge, mtumishi wa umma mwenye uadilifu, aliyejitolea kulitumikia Taifa kwa uwazi na uaminifu, na ni mshindi wa Nishani ya Vita ya Kagera, kama ishara ya uzalendo na mchango wake kwa Taifa.

