Washitakiwa 114 wafunguliwa kesi ya uhaini Mwanza, kufuatia maandamano Jumla yafikia 320 nchi nzima

Jumla ya watu 114 wamefikishwa mbele ya mahakama ya wilaya ya Ilemela

Mwanza: Jumla ya watuhumiwa 114 waliokamatwa wilayani Ilemela mkoani Mwanza kati ya Oktoba 28 na 29, 2025 wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilemela wakikabiliwa na mashtaka mbalimbali yakiwamo ya kula njama na uhaini.

Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka yao leo Jumatatu Novemba 10, 2025 kuanzia saa 7 mchana hadi saa 22 mchana katika Kituo cha Hakimu Jumuishi cha Buswelu mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Christian Mwalimu na Stella Kiama.

Watuhumiwa hao wamesomewa mashitaka katika kesi tatu tofauti, kesi ya kwanza ikiwa na watuhumiwa 22, kesi ya pili 64, na tatu kesi 28, ambapo upande wa Jamhuri ulikuwa ukiwakilishwa na Mawakili wa Serikali Mwandamizi, Mwanahawa Changale na Safi Amani akisaidiana na Adam Murusuli.

Upande wa utetezi uliwakilishwa na mawakili tisa kutoka Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) wakiongozwa na Erick Mutta.

Mahakama iliambiwa kuwa washtakiwa wote hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo kukosa mamlaka ya kusikiliza kesi hizo, huku makosa yote hayana dhamana hivyo washtakiwa wote wataendelea kusota rumande huku upelelezi ukiendelea.

Katika shtaka la kwanza namba 26565/2025 mbele ya Hakimu Christian Mwalimu, Wakili wa Serikali Mwanahawa Changale alisema watuhumiwa 22 wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama na uhaini kinyume na kifungu cha 384 na 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, wakidaiwa kula njama za kuvuruga uchaguzi mkuu na kuharibu mali za serikali.

Kesi ya pili, kesi namba 26641/2025, inayowakabili washtakiwa 64 (Fredy Malebele na wenzake 63), ilisomwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Stella Kiama ambapo upande wa Jamhuri ulifungua mashtaka mawili ya kula njama na uhaini yaliyofanyika kati ya Oktoba 28 na 29 katika maeneo ya Pasiansi, Kona ya Bwiru, Kitangiri na Kitangiri.

Katika kesi hizo, upande wa utetezi uliibua hoja tano za kuiomba Mahakama iuelekeze upande wa Jamhuri kuzifanyia kazi haraka kabla ya tarehe ijayo kwa ajili ya kutajwa kwa shauri hilo, ikiwamo kuomba kupatiwa matibabu washtakiwa ambao ni wagonjwa na kutoa nguo na viatu kwa wasiokuwa navyo.

Baada ya kusikiliza maombi hayo Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi Christian Mwalimu alimuamuru Mfawidhi wa Gereza la Butimba kuwapeleka hospitali washtakiwa tisa na kuwasilisha taarifa za matibabu mahakamani siku ya kutajwa kwa kesi hiyo pamoja na kuhakikisha washtakiwa wote wanapatiwa nguo na viatu.

Naye Hakimu Mkazi Mkuu, Stella Kiama aliliagiza Jeshi la Magereza kuhakikisha watuhumiwa wanapata haki zao wakiwa chini ya ulinzi ikiwa ni pamoja na kukutana na ndugu zao kwa kufuata utaratibu uliowekwa na vyombo vya ulinzi na usalama.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa TLS Mkoa wa Mwanza, Erick Mutta, alisema jumla ya mawakili 37 wa chama hicho wamejitolea kuwatetea watuhumiwa wote waliokamatwa kufuatia matukio yaliyotokea kati ya Oktoba 29 na 31, baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

poo GIF