UVUMILIVU WA MUNGU ULIPOKUWA UKINGOJA, SIKU ZA NUHU.

Jina la Bwana wetu Yesu libarikiwe. Nakukaribisha tulitafakari Neno la Mungu, ambalo ndio pekee lenye uwezo wa kuokoa roho za watu.

Ndugu yangu nataka ufahamu kuwa kuzimu inafananishwa na GEREZA kubwa sana lenye Malango na makomeo yake…Soma (Isaya 38:10 na Ayubu 17:6) utalithibitisha hilo…Haisemi mlango au komeo tu kana kwamba ni mmoja mmoja, hapana Bali ma-lango, ma-komeo, Hii ikiwa na maana kuna kifungo, na magereza mengi tofauti tofauti kulingana na aina ya dhambi za watu. Kama ukifa leo katika dhambi basi lipo lango lako uliloandaliwa na watu wa aina yako katika gereza lenu. Na huko sio kukaa tu, hapana kuna shida na mateso ya hali ya juu sana…Wote wanakaa huko wakisubiria siku ile ya hukumu wahukumiwe kisha ndio watupwe katika lile ziwa la moto.

Na gereza la juu kabisa ni lile la shetani na malaika zake, ambalo kwasasa wapo baadhi yao huko wamefungwa wakingojea kutupwa kwenye lile ziwa la moto siku ile ya mwisho itakapofika, japo wapo wengine baadhi yao duniani wakizunguka, ndio hawa wanaoiharibu dunia…

[INDENT]2Petro 2:4 “Kwa maana ikiwa Mungu hakuwaachilia malaika waliokosa, bali aliwatupa shimoni, akawatia katika vifungo vya giza, walindwe hata ije hukumu”;[/INDENT]
Lakini leo nataka tujifunze jambo moja, ambalo pengine huwa tunalipitia kila siku lakini hatulielewi… Na jambo lenyewe ni lile la Bwana Yesu kushuka kuzimu, na kuwaendea roho waliokaa kifungoni…Embu tusome…
https://wingulamashahidi.org/wp-content/uploads/2020/02/83987566_772924323202628_2713546091206279168_n.jpg
[INDENT]1Petro 3:18 “Kwa maana Kristo naye aliteswa mara moja kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili yao wasio haki, ili atulete kwa Mungu; mwili wake akauawa, bali roho yake akahuishwa,
19 ambayo kwa hiyo aliwaendea roho waliokaa kifungoni, akawahubiri;
20 watu wasiotii hapo zamani, uvumilivu wa Mungu ulipokuwa ukingoja, siku za Nuhu, safina ilipokuwa ikitengenezwa; ambamo ndani yake wachache, yaani, watu wanane, waliokoka kwa maji”.[/INDENT]

Utaona hapo, tukio lililofuata baada ya Kristo kufa msalabani lilikuwa ni kushuka kuzimu, na kwenda kuzitembelea hizi roho zilizokuwa vifungoni, lakini biblia haiwataji wafungwa wote, bali inatuonyesha watu Fulani tu, katika gereza Fulani mahususi, ambalo Bwana Yesu alikwenda kuwahubiria… Na hao si wengine Zaidi ya watu wa kipindi cha Nuhu…Sio kwamba hakuenda kwa wengine lakini kulikuwa na sababu kwa nini walilengwa watu wale…kwasababu na sisi ndio tunaofananishwa na kundi hilo…

Sasa huko kuhubiri kunakozungumizwa sio kwenda kuhubiriwa labda watubu au wageuke, hapana, kuhubiri kupo kwa aina nyingi, kutangaziwa hukumu nayo ni moja ya mahubiri, alikwenda kuwatangazia hukumu yao, ni kwanini wao wanastahili adhabu kubwa kuliko wote…

Na dhambi yao ilikuwa si nyingine Zaidi ya kupuuzia “Uvumilivu wa Mungu” uliokuwa ukilia juu yao siku baada ya siku…

Walipokuwa wanajua kabisa ni kweli dunia inakwenda kuangamizwa lakini wanafanya makusudi kushupaza shingo zao, wakiiona Safina ikijengwa, kwa muda wa miaka yote hiyo, walipokuwa wakihubiriwa na Nuhu kwa muda mrefu sana wa miaka 120 watubu waache dhambi zao lakini wanakataa…Wakimsikia Nuhu akiwaambia Mungu anawapenda, hataki hata mmoja aangamie, lakini wao wanaenda kinyume chake, wanaishi Maisha ya uovu, wanazini makusudi, walewa makusudi, wanafanya uchawi na ushirikina…wanasema huyo Mungu anayesema ataangamiza dunia mbona hatumwoni akiangamiza, kashakufa, wewe Nuhu acha ukichaa, wewe ni mvivu, hutaki kujishughulisha wewe unawaza tu mbinguni, na Maisha mwilini utaishije sasa, umaskini wa akili na ulimbukeni wa kifikra?..

Lakini siku ilipofika uvumilivu wa Mungu uliposema Basiii…Hakusalia hata mmoja…na wote moja kwa moja wakapelekwa katika gereza lao moja mahususi, lililokuwa limetengwa kwa ajili ya watu wa namna hiyo wanaostahili hukumu ya juu Zaidi…Na ndipo huko Kristo alipowafuata kuzimu…

Biblia inatuambia kama ilivyokuwa katika siku za Nuhu ndivyo itakavyokuwa siku za kuja kwake mwana wa Adamu, Siku za Nuhu watu walipuuzia wokovu, japokuwa walielezwa kuwa dunia inakwenda kuteketezwa lakini walitukana…Ndivyo ilivyo leo hii, dalili zote za kuja kwa Kristo zimeshatimia katika karne hii ya 20 na 21,…Na mojawapo ya dalili ya juu kabisa ni kutokea na kuongezeka kwa kasi kwa manabii wa Uongo na makristo wa uongo…mambo ambayo ukimuuliza hata mtu aliyekufa mwaka 90’, atakwambia jambo hilo hatujawahi kuliona wala kulisikia kama limeshawahi kutokea katika historia…Lakini sisi leo hii tunalishuhudia kwa macho yetu, lakini badala watu watubu wamgeukie Mungu, ndio kwanza wanatoa maneno ya kudhihaki…huyo Yesu mpaka leo miaka 2000 imepita hajaja amekufa…,mizaha, jina la Kristo linatajwa kiholela holela mpaka kwenye comedy …. wanaudharau uvumilivu wa Mungu…

Moja ya siku hizi, hii dunia itafika mwisho… Na kibaya Zaidi tumeambiwa mwisho huo utakuja kwa ghafla sana. Hakuna mtu atayetazamia kama kweli huo ndio wakati wenyewe…kwasababu biblia inatuambia utakuja wakati wa amani…sio wakati wa vita…leo hii tunaishi katika hicho kipindi… Na kama ikitokea umekufa katika hali ya dhambi, ukijua kuwa kila siku umekuwa ukikutana na mahubiri na injili zinazokuhubiria ugeuke lakini hutaki…basi ujue gereza lako litakuwa ni lile la hali ya juu Zaidi kuliko lile la watu wa Nuhu na lile la watu wa sodoma na Gomora.

[INDENT]Mathayo 11:20 “Ndipo akaanza kuikemea miji ile ambamo ndani yake ilifanyika miujiza yake iliyo mingi, kwa sababu haikutubu.
21 Ole wako, Korazini! Ole wako, Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwenu ingalifanyika katika Tiro na Sidoni, wangalitubu zamani kwa kuvaa magunia na majivu.
22 Walakini nawaambieni, itakuwa rahisi Tiro na Sidoni kustahimili adhabu zao siku ya hukumu kuliko ninyi. 23 Nawe Kapernaumu, je! Utakuzwa mpaka mbinguni? Utashushwa mpaka kuzimu; kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwako ingalifanyika katika Sodoma, ungalikuwapo mji huo hata leo.
24 Walakini nawaambieni, itakuwa rahisi nchi ya Sodoma kustahimili adhabu yake siku ya hukumu kuliko wewe”.[/INDENT]
Ukiona kwanini dunia mpaka dakika hii haijateketezwa, ujue kuwa sio kwamba Mungu anafurahia ulawiti wako, au uzinzi wako, au ulevi wako, au uvaaji vimini vyako, ni kwasababu uvumilivu wake unakungoja utubu, ili usiingie katika adhabu kuu ya siku ile.

Kama bado unasua sua, au upo vuguvugu ni wakati sasa wa kuanza kuyatengeneza mambo yako sawa na Mungu wako…Usijivunie dini au dhehebu,…wakati tuliopo ni wakati wa kuutafuta uhusiano wako binafsi na Mungu wako. Jiulize je! Ikiwa unyakuo utapita leo nitakuwa na uhakika wa kwenda na Bwana…Je! nikifa leo nitakuwa na uhakika wa kwenda mbinguni, au kwenye haya magereza ya milele nikiteseka huko usiku na mchana…

Watu wa kizazi chetu hichi ni watu ambao tumewekewa thawabu kubwa Zaidi kama tukishinda(Ufunuo 3:21)…Lakini pia tuzimbea na kuichezea neema tumeahidiwa adhabu iliyo kubwa zaidi kuliko wote waliotutangulia… Hivyo uamuzi ni wetu sisi, Uzima au Mauti. Lakini sisi tunaopenda Maisha tutachagua uzima ambao unaletwa na Yesu Kristo tu peke yake,kwa kumwamini yeye na kujitwika misalaba yetu kila siku na kumfuata.

uvumilivu wa Mungu ni upendo kwetu.

Ubarikiwe.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe au piga namba hii +255 789001312

Maran Atha.

https://wingulamashahidi.org/category/mafundisho/