USIIGEUZE NYUMBA YA MUNGU KUWA PANGO LA WANYANG’ANYI.

Jina la Bwana wetu Yesu libarikiwe, Kama umeamka salama ni jambo la kumshukuru Mungu sana, hivyo nakukaribisha katika kuyatafakari maneno ya Uzima ya Bwana wetu, ambayo ndio chakula cha roho zetu.

Neno la Mungu linasema…

[INDENT]Yeremia 7: 9 “Je! Mtaiba, na kuua, na kuzini, na kuapa kwa uongo, na kumfukizia Baali uvumba, na kuifuata miungu mingine ambayo hamkuijua;
10 KISHA MTAKUJA NA KUSIMAMA MBELE ZANGU KATIKA NYUMBA HII, iitwayo kwa jina langu, na kusema, Tumepona; ILI MPATE KUFANYA MACHUKIZO HAYO YOTE?
11 Je! Nyumba hii, iitwayo kwa jina langu, imekuwa PANGO LA WANYANG’ANYI MACHONI PENU? Angalieni, mimi, naam, mimi, nimeliona jambo hili, asema Bwana”.[/INDENT]
Tusome tena…

[INDENT]Mathayo 21: 13 “akawaambia, Imeandikwa, Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala; bali ninyi mmeifanya kuwa PANGO LA WANYANG’ANYI”[/INDENT]
Umewahi kujiuliza kwanini, kwanini Bwana alitumia huo usemi…. “bali ninyi mmeifanya kuwa PANGO LA WANYANG’ANYİ”. Umewahi kutafakari pango la wanyang’anyi ni kitu gani?.

Siku zote wezi/vibaka wanakuwaga na maskani yao wanayojifichia, ambayo kwao ndio sehemu salama, na inakuwa ni sehemu ya maficho kwa muda, mara nyingi inaweza kuwa kwenye kipori fulani, au kwenye jengo fulani ambalo halijakamilika, au kwenye mapango ambayo ndani yana giza, Lengo ni kwamba wakishamwibia mtu, wanakimbilia huko, kujificha kwa muda, na baadaye kurudia tena kufanya uhalifu wao…hivyo inakuwa ni ngumu kuwakamata… Na mara nyingi kwenye hayo maficho yao, ndio sehemu zao za kuchezea kamari, au kuvuta sigara, au kufanyia biashara zao haramu kama za kuuziana mihadarati n.k

Mfano kamili wa leo, mtu atatoka kufanya uasherati, lakini mtu huyo huyo jumapili atakwenda kanisani…jumatatu atarudia kufanya kile kile kitu na kurudi tena kanisani, jumapili inayofuata…Mtu huyo ameigeuza nyumba ya Mungu kuwa pango la wazinzi, kanisa ni sehemu yake ya kujisitiri kwa muda, ili aonekane kwamba na yeye ni mkristo, au ili ajifariji moyoni kwamba bado anampenda na kumjali Mungu, na ili ajifariji kwamba jamii inamwona msafi…Lakini kiuhalisia hana mpango wa kuacha uasherati wake, wala hana mpango wa kumwacha yule mtu anayeishi naye ambaye wanayefanya naye uasherati.
https://wingulamashahidi.org/wp-content/uploads/2020/11/7fa9947c-3216-4f6a-874d-51dbab1bad09_x365.jpg

Mwingine ni fisadi, au tapeli lakini atahudhuria kanisani kama ilivyo ada, na wala haendi kwa lengo la kubadilika, bali anakwenda pale kama sehemu yake ya kusitiri maouvu yake…

Ndugu yakumbuke maneno ya Bwana… “Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala; bali ninyi mmeifanya kuwa PANGO LA WANYANG’ANYİ”.

Usiigeuze nyumba ya Mungu kuwa ni sehemu yako ya maficho ya dhambi zako…bali pageuze kuwa mahali pa sala, mahali patakatifu pa kukujenga roho yako. Kadhalika nyumbani kwa Mungu sio mahali pa kwenda umevaa nusu uchi, umevaa vimini, au umepaka wanja na lipstick, au umenyoa kiduku, kwa ufupi sio mahali pa kutangaza mwili wako au biashara yako…pale ni mahali pa kumheshimu Mungu.

Kama Bwana alizipindua zile meza za wafanya biashara kwenye nyumba yake, hatashindwa kuipindua biashara ya kuuza mwili wako huo usio na staha uliokuja kuuza pale kwenye nyumba yake. Kama umeamua kutangaza biashara ya mwili wako, yapo mapango mengi huko mitaani, lakini usijaribu kuiguza nyumba ya Mungu kuwa kama mojawapo ya mapango hayo.

Kama hujampa Kristo maisha yako, wakati ni sasa. Tubu leo naye atakusamehe bure kabisa. Kumbuka Kristo anarudi, siku moja hutasikia maneno kama haya ambayo unaona sasa ni upuuzi na kelele…wakati huo unyakuo utakuwa umepita, na hutasumbuliwa sumbuliwa na mahubiri tena. Lakini akiamua kutubu leo, Kristo atakupokea kama neno lake linavyosema…katika Yohana, na atakupa Roho Mtakatifu atakayekuongoza katika kuijua kweli yote.

[INDENT]Yohana 6:37 “Wote anipao Baba watakuja kwangu; wala ye yote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe”.[/INDENT]
Maran atha

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312

https://wingulamashahidi.org/

Usifanye kijiji chetu kuwa uwanja wa kuleta ujinga na upusi wa wakoloni!