Nilimsikia Mbunge wa Vunjo, James Mbatia, alipoleta hoja ya Jinsi magazeti mbalimbali yalivyochapisha makala ambazo wengi wanaona ni za UCHOCHEZI na hazina tija kwa umoja wetu wa kitaifa. Jana Waziri Mwakyembe tumemsikia akimjibu Mbatia, kwamba ameshitushwa na kauli za “uwepo wa ubaguzi wa kikabila” kuletwa bungeni, kwamba hapa si mahali pake, kwamba kama anaona kabila la wachaga linabaguliwa basi aende mahakamani. Mwakyembe alijaribu kuhamisha msingi wa mada kutoka tishio kwa umoja wa kitaifa kuja kuwa ni tishio kwa mtu au kikundi, na akasema ufumbuzi ni kwenda Mahakamani.
Serikali ya awamu ya Tano inaonekana imegundua mbinu ya kukabiliana na tuhuma na mashambulizi mbalimbali kutoka kwa WAPINZANI, nayo ni “kuwashauri” waende mahakamani kufungua kesi. kuanzia shutuma za kuvunja katiba ya Jamhuri ya Muungano, na pia Sheria ya Vyama vingi, kwa kuzuia mikutano ya siasa, kubana magazeti na vyombo vya habari na mitandao, mpaka hii iliyoletwa bungeni na Mheshimiwa Mbatia, ushauri ni huo huo: kama mtu anaona kwamba hajatendewa haki, aende mahakamani!
Ukiangalia juu juu utakubaliana na akina George Mkuchika na Mwakyembe, kwamba kwenda Mahakamani si ndio kwenye utoaji wa haki? lakini ukichunguza kwa makini utagundua kwamba kuna hila ipo ndani yake. Kwanza kabisa, pale inapotokea kwamba Serikali yenyewe imekosolewa vikali, au kikundi cha watu au mtu au taasisi yenye msimamo unaounga mkono ule wa Serikali, basi Serikali wala haiendi mahakamani, na wala haisubiri huyo mtu au kikundi au taasisi inayounga mkono serikali, waende mahakamani. Serikali huchukua hatua yenyewe, ama kufungia kama ni chombo, au kumtetemesha huyo mhusika kwa “kuhojiwa na Polisi” tena kwa ratiba ya kumchosha. mara ngapi serikali imefungia magazeti yenye msimamo unaotofautiana na wa serikali? tena kwa hoja dhaifu? pia wakati Kardinali Pengo alipotofautiana na Maaskofu wenzake kuhusu waraka fulani ulitolewa hapo nyuma, siyo huu wa juzi wa Kwaresima ya 2018, Askofu Gwajima alimshambulia na kumkosoa. Serikali badala ya kusubiri Kardinali Pengo aende mahakamani kufungua kesi, Jamhuri yenyewe ilifungua kesi dhidi ya Gwajima, na alihojiwa na Polisi hadi presha ilipanda ikabidi apelekwe Hospitali kwanza.
Lakini kwa hili la “waraka dhidi ya Kanisa Katoliki” kuchapishwa na magazeti, tena huo “waraka” ni wa kichochezi haswa, Serikali inakaa pembeni na kudai kwamba kama kuna mtu anaona hajatendewa haki, aende tu Mahakamani!! Kuna suala la huyu mtu anaitwa Musiba, ambaye anatoa tuhuma nzito na vitisho na hata kutishia vifo kwa wanasiasa wa upinzani. lakini kwa kuwa wanaoshambuliwa ni “WAPINZANI”, ambao kwa mujibu wa serikali yetu, WAPINZANI siyo WATANZANIA, basi serikali iko kimyaaaa, utadhania haipo vile. ukitaka kujua kwamba nchi hii kuna serikali, mchokonoe Magufuli, au serikali yenyewe, hapo utajua.
Mheshimiwa Mwakyembe, tumekusikia, na wala hujatudanganya. unajidanganya mwenyewe na serikali yenu ya kikandamizaji na undumila kuwili.