UhuRuto: Kisa Cha Ndoa Ya Machozi Inayoyeyuka

[ATTACH=full]349418[/ATTACH]
Tunachosubiri sasa ni king’ora rasmi cha talaka; ni bayana kwamba kila mmoja yuko mbioni kukusanya virago aondoke. Walianza kwa kulishana pambaja na busu lakini itabidi waachane kwa cheche za lawama, Hata hivyo, ukichanganua kwa kina utabaini kwamba ili Uhuru na Ruto wafaidike kisiasa, ni muhimu talaka yao iwe ya hamaki na machozi ya kusalitiana. Hii ni kwa sababu kila mmoja wao anahitaji kujitakasa mbele ya umma. Katika historia ya nchi hii, kipindi cha uongozi wa wawili hawa ndicho kilichofeli zaidi ikilinganisha na tawala zingine tangu 1963.
Uhuru na Ruto pia wamewatwika Wakenya mzigo mzito wa deni la taifa licha ya raia kuzama zaidi katika umaskini, uvundo wa ufisadi, ukosefu wa ajira na kuzorota kwa uchumi. Manifesto waliyozindua pamoja mwaka 2013 imegeuka kejeli; ahadi ya paradiso imekuwa machungu ya jehanamu kwa wananchi.

Babu yangu alinisimulia kisa cha ndoa ya machozi. Malkia Chaurembo, mke wa mfalme, alilazwa kitandani akiugua maradhi yaliyomwacha amekonda kama ng’onda, anateseka kwa maumivu. Jitihada za waganga kubaini na kutibu maradhi hayo hazikufua dafu. Hali ya malkia ilizidi kuzorota na kuwatia kiwewe jamaa.
Siku moja jioni chumbani, Chaurembo alikuwa amelaza kichwa kwenye paja la mumewe analia kwa kukata tamaa huku pumzi ikikatikakatika.
Alijikaza na kwa sauti hafifu akatamka: “Mume wangu kipenzi kuna jambo lazima niseme kabla nife ili roho yangu ipone.”
Mumewe alimkumbatia na kumwambia: “Usijisumbue, utanieleza yote ukipata nafuu. Kwa sasa pumzika.” Malkia aliendelea: “Lazima ujue ukweli. Nimekusaliti katika ndoa hii. Kifungua mimba na kitinda mimba si wanao, mimi ni mzinifu. “Dhahabu na almasi nilinyakua kutoka hazina yetu nilimpa mpenzi wangu wa kando. Pia ni mimi niliyemsingizia ndugu yako tuhuma za uwongo akahukimiwa kifo na kisha akanyongwa. Nisamehe mume wangu. Ninatubu!” Mfalme hakuonekana kushangaa. Aliinua kichwa na kumweleza: “Usiwe na shaka malkia. Yote uliyosema ninayajua. Ndio sababu nilikutilia sumu kwenye kinywaji. Kwa sasa, naomba utulie sumu imalize kazi.” Kisha akaondoka chumbani. Katika mirindimo ya siasa kali, uungwana huja baada ya maslahi ya kibinafsi. Talaka ya kiungwana haiwezekani kwa ndoa ya Uhuruto kwa sasa. Itadhuru azma zao.

Ruto hawezi kutwaa urais kwa kusherehekea mafanikio ya Jubilee. Lazima atafute wa kulaumu. Atalaumu handisheki na usaliti.

Uhuru naye hatakubali kustaafu na tope la kufeli. Atasema tamaa ya Ruto ilisaliti uhusiano na kuvuruga utendakazi wao.