Yeremia 4:22 “Kwa maana watu wangu ni wapumbavu, hawanijui; ni watoto waliopungukiwa na akili, wala hawana ufahamu; ni wenye akili katika kutenda mabaya, bali katika kutenda mema hawana maarifa”.
Shalom, Mungu anatazamia kila mmoja wetu siku anapofanyika kuwa kiumbe kipya, bidii mpya iumbike ndani yake na hari mpya ya kutafuta kumpendeza yeye kwa namna yoyote ile ionekane.
Kama vile tunavyojua mtu aliyekatika dhambi huwa hakai hivi hivi tu, bali anafanya juu chini kuhakikisha kuwa kile anachokitamani anakipata katika ubora wote… Kwamfano ukimtazama mlevi, utajiuliza huyu ni kwanini mwaka mzima anakunywa tu?. Unaweza kusema ana pesa nyingi, Sio kwamba ana pesa nyingi sana kwenye akaunti yake zaidi ya wewe, hapana, bali ukimchunguza utagundua kuwa ili aweze kunywa kwa kadiri awezavyo, na kutoshelezeka itamgharimu mchana kutwa akifanyie kazi, ili apate pesa jioni au wikiend akanywe makreti ya bia. Unaona hapo ametumia akili katika mambo yake, ilimpasa akakifanyie kazi, ili afurahie ulevi wake, na ndio maana Bwana Yesu alisema,
[INDENT]Luka 16: 8b “…wana wa ulimwengu huu katika kizazi chao wenyewe huwa na busara kuliko wana wa nuru”.[/INDENT]
Lakini mkristo, anayejua kuwa jumapili anahitajika kwenda kanisani, mahali ambapo analishwa chakula cha kiroho, mahali ambapo anapata baraka za kimbinguni, hawezi kudunduliza chochote na kukipeleka nyumbani kwa Bwana atakwenda mikono mitupu. Na mtu kama huyo, bado anatazamia viwango vyake vya kiroho viwe kama anavyotarajia… Kumtolea Bwana sio kumnufaisha mchungaji wako, kumtolea Bwana ni kuonyesha upendo wako kwake, na kuwa unathamini wokovu wake aliokupatia bure bila malipo.
Lakini mwingine wakati huo huo akisikia, kuna shughuli ya jirani yake, pengine harusi na kunahitaji michango mikubwa, ataanza kulihangaikia hilo, hata miezi miwili au mitatu kabla, ili huo wakati utakapofika atoe kiwango kile kile alichopangiwa, asiabike. Sasa mkristo kama huyu kibiblia ni mjinga katika kutenda mema, bali mwenye maarifa katika kutenda mambo mengine.
Vivyo hivyo katika kusali,
Mtu wa mwilini labda tuseme mwanafunzi, anajua kabisa ili afaulu katika masomo yake itamgharimu, kusoma kwa bidii, kila siku na wakati mwingine kukesha usiku,…lakini kwa mkristo, haipo hivyo, atataka akue kiroho katika mazingira ya kusubiria ahubiriwe kanisani jumapili, au aombewe, na hata kama akiomba mwenyewe basi ataomba dakika mbili, tatu,., Hapo ni sawa na tunakuwa wajinga katika kutenda mema, tumepungukiwa akili katika mambo ya rohoni. Tukitaka tupate matokeo mazuri rohoni, ni sharti tutumie akili zilezile tulizokuwa nazo katika dhambi, isipokuwa tu tunazihamishia kwa Mungu,. Hapo tutaufurahia wokovu wetu sana.
https://wingulamashahidi.org/wp-content/uploads/2020/12/download-6.jpg
Biblia inatuonyesha zipo faida za kuyatafuta mambo mema hususani pale tunapotumia bidii, na faida kuu ni kuwa Mungu atamshusha mara moja shetani chini ya miguu yetu, Anakuwa hana nguvu yoyote ya kutushinda sisi. Soma.
[INDENT]Warumi 16.19 “….lakini nataka ninyi kuwa wenye hekima katika mambo mema, na wajinga katika mambo mabaya.
20 Naye Mungu wa amani ATAMSETA SHETANI CHINI YA MIGUU YENU UPESI. Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja nanyi. [Amina.][/INDENT]
Je! Unataka shetani na kwako awe ni kitu kirahisi sana, kitu kinyonge?, jibu ni moja tu, kuwa mjinga katika kutenda mabaya, na kinyume chake tumia akili zako nyingi katika kumtumikia Mungu. Fanya zaidi ya pale ulipozoelea kufanya siku zote. Kila siku hakikisha unaiga hatua moja kiroho, hatua katika kumtolea yeye, katika kuomba, katika kusali, katika kufunga, n.k. Na matokeo utayaona. Utaishi maisha kama vile shetani hakujui wewe. Kumbe ni siku nyingi sana Mungu alishamshusha chini ya miguu yako.
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312