Taasisi ya vijana wa Tanzania ya African Leadership Initiatives for Impact (ALII) imetunukiwa Tuzo ya UNESCO Global Citizenship Education katika hafla iliyofanyika kwenye Makao Makuu ya UNESCO, Paris Desemba 09, 2025.
Tuzo hiyo inayofadhiliwa na Jamhuri ya Korea, imetolewa kwa taasisi ya ALII ya Tanzania kwa kutambua mchango wao katika kuimarisha fikra za amani na maendeleo kwa zaidi ya vijana 50,000 wa Kitanzania. Katika hafla hiyo, taasisi za Tanzania na Equador zimeshinda Tuzo ambazo ziliwaniwa na taasisi 154 kutoka nchi 76 ulimwenguni. Bw. Joseph Brighton Malekela, Mkurugenzi Mtendaji na Bi. Neema Chusi, Mwenyekiti wa Bodi ya ALII wamewakilisha vijana wenzao kupokea tuzo hiyo.
Ubalozi wa Tanzania nchini Ufaransa ambao pia unawakilisha kwenye UNESCO unaupongeza kwa dhati uongozi wa taasisi ya ALII pamoja na wanachama washirika wake kwa mchango wao kwenye ujenzi wa amani na maendeleo miongoni mwa vijana, mchango ambao umetambuliwa na jumuiya ya kimataifa.
