Kinara wa Cord Raila Odinga anatarajiwa kuzuru Mombasa wiki hii ili kuhudhuria uzinduzi wa barabara iliyopewa jina la mwanawe marehemu Fidel Odinga katika eneo la Nyali.
Barabara hiyo ni ahadi aliyotoa gavana Mombasa Hassan Joho, kwa familia ya Odinga wakati wa mazishi ya Fidel Odinga mapema mwaka jana.
Ujio wa Raila mjini Mombasa unawadia wakati joto la kisiasa linazidi kupanda eneo la Pwani hususan baada ya Rais Uhuru Kenyatta kupiga kambi mjini humo, kwa zaidi ya majuma matatu ambapo alitekeleza miradi mbalimbali kwa wakazi ikiwemo kuuzindua mradi wa mwangaza mtaani.
Hata hivyo, kulingana na msemaji wa Raila, Dennis Onyango, kiongozi huyo hatajihusisha na masuala ya siasa wakati atakapozuru Mombasa kama inavyotarajiwa na wengi ila atahudhuria uzinduzi huo na kisha kurejea Nairobi kwa shughuli zingine za kifamilia.
Kauli ya Onyango inakinzani na ya Raila ya awapo awali, ambapo alinukuliwa akisema kuwa atazuru eneo la Pwani ili kuwarai wenyeji kuzidi kuunga mkono mrengo wa Cord kufuatia hatua ya viongozi wengi wa kisiasa eneo la Pwani kutangaza kuuhama mrengo huo na kujiunga na chama kipya cha JAP.
Aidha wengi wanamtarajia Raila kupeleka kampeni za chama cha ODM mjini Kilifi ili kumpigia debe mgombeaji wa chama hicho katika uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Malindi, Willy Mtengo.
Kwa mujibu wa msemaji wa Raila, Dennis Onyango, kiongozi huyo anatarajiwa kutua Mombasa siku ya Jumanne jioni au Jumatano asubuhi.