ok

ERIC SHIGONGO
DUNIA HAINA USAWA
Ojuku aliambiwa kwamba Bokasa alikuwa nchini Ubelgiji, hakutaka kuona mwanaume huyo akikimbia na kujificha kama ilivyokuwa kwa marais wengine wa Afrika, hivyo akaagiza watu kuondoka kuelekea nchini humo kwa ajili ya kujua mahali alipokuwa na kumkamata.
Hilo halikuwa tatizo, wanaume hao wakaondoka kuelekea huko, walipofika, wakaanza kuulizia sehemu mbalimbali kuhusu mwanaume huyo, walikuwa na uhakika kwamba alikuwa hapohapo Brussels hivyo hawakutaka kutoka kwenda sehemu nyingine yoyote ile.
Walimtafuta kimyakimya tena kwa kuulizia kwa siku mbili mfululizo lakini hawakufanikiwa kitu kilichowafanya kumpigia simu Ojuku na kumwambia kilichokuwa kimetokea. Hilo tayari likaonekana kuwa tatizo, hakujua ni kwa jinsi gani wangeweza kumpata mwanaume huyo.
Wakati akiwa anafikiria sana ndipo jina la Denis likamjia kichwani mwake, hakutaka kuchelewa, hapohapo akampigia simu na kumwambia kilichokuwa kimetokea kwamba iwe isiwe ilikuwa ni lazima kujua mahali alipokuwa Bokasa.
Denis, ambaye ndiye Godwin akaondoka mpaka kambini na kukutana na Ojuku na kuanza kuzungumza naye kwa undani. Alimwambia lengo lao la kumpata Bokasa, kwa yote aliyokuwa ameyafanya nchini Tanzania, alitakiwa kushtakiwa na kufungwa gerezani.
“Watu wetu wapo Ubelgiji, hawajui mahali alipo,” alisema Ojuku.
“Si tatizo. Ngoja nimtafute.”
Kitu pekee alichokifanya ni kuanza kumtafuta kwa kutumia simu yake. Aliingiza namba ya simu yake katika kompyuta yake na kuanza kumtafuta kila kona. Hiyo ilikuwa kazi yake, alizoea kuifanya kila siku hivyo hakukuwa na shida yoyote ile, baada ya dakika chache, akapata majibu kwamba mtu huyo alikuwa katika Benki ya Brussels.
“Atakuwa benki! Una uhakika?” aliuliza Ojuku.
“Simu yake ipo huko, na bila shaka inawezekana alikwenda kwa ajili ya kutoa pesa. Cha msingi watume waende huko, hata kama hayupo basi kutakuwa na watu wanaojua mahali alipo,” alisema Godwin.
“Sawa. Hakuna shida,” alisema Ojuku, hapohapo akachukua simu yake na kuwapigia watu hao na kuwaambia waende katika Benki ya Brussels ambapo walikuwa na uhakika kwamba mtu huyo anaweza kuwa huko.
“Haina shida. Tunakwenda,” alisema jamaa aliyekuwa huko na safari ya kwenda katika benki hiyo kuanza.


Kila mtu alitaka kuiona Tanzania mpya, matumaini na furaha ya Watanzania ambayo ilikuwa imepotea mioyoni mwao ikaanza kurudi, mpaka kipindi hicho hakukuwa na kitu chochote kilichobadilika lakini tayari Watanzania waliona tayari wameanza kupata maisha mazuri ambayo kila mmoja alikuwa akiyatamani.
Godwin alifanya kazi kubwa sana kupitia akaunti yake ya Mabadiliko ya Kweli, kila mtu nchini Tanzania alitaka kumuona mtu huyo, alikuwa nani na alikuwa na muonekano gani? Hilo likawafanya watu kutengeneza umoja waliouita ONYESHA SURA YAKO ambao ulikuwa na kazi ya kupanga mikakati ya kuandamana kutaka kumuona mwanaume ambaye alichangia kuiweka Tanzania hapo ilipokuwa, na hata kumuondoa Rais Bokasa madarakani.
Hakukuwa na mtu aliyemjua mtu huyo, kila mmoja alikuwa na hamu, watu wengi waliomba kumuona huku wengine wakienda mbali na kutaka kuona mtu huyo akiwa rais wa Tanzania lakini hilo halikuwezekana, Godwin hakufikiria kuwa rais wa nchi hiyo, kitu pekee alichokuwa anakitamani kila siku ni kumuondoa Bokasa madarakani kitu ambacho alifanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Watu hawakuishia kulalamika mitandaoni tu bali baada ya siku kadhaa, wakajikusanya mitaani na kuanza kuandamana maandamano ya amani ya kumtaka Godwin kujitokeza hadharani huku wengine wakitaka hata kuona akizungumza lolote tangu alipoanzia mpaka pale alipofikia.
Kila kitu kilichokuwa kikiendelea, Godwin alikuwa akikifuatilia na wakati mwingine kukusanyika na waandamanaji hao na kuandamana pamoja nao pasipo kugundua kwamba alikuwa miongoni mwao.
“Kesho nitahitaji kuzungumza na watu kupitia akaunti hii, nitasema mimi ni nani, nimeibukaje, nitaeleza kila kitu ila sitohitaji sura yangu ionekane,” aliandika Godwin kwenye mtandao, maneno ambayo kidogo yakawafanya watu waliokuwa wakitaka kuandamana tena kuacha kufanya hivyo.
Kama alivyokuwa ameahidi ndivyo alivyofanya, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kwenda katika Hoteli ya Atriums iliyokuwa Africasana, moja ya hoteli iliyokuwa na ukimya mkubwa, akachukua chumba ambapo humo ndani akaanza kujirekodi video huku akisimulia historia ya maisha yake.
Wakati mwingine alikuwa akilia, hakutaka kuiacha sura yake ionekane, aliiacha ionekane mwisho mdomoni kushuka chini na kuendelea kuhadithia. Alianza tangu siku ya kwanza alipokuwa na ufahamu, aliwaambia watu kwamba yeye alikuwa mtoto wa Mzee Mapoto, mwanasiasa maarufu nchini Tanzania ambaye alitokea kupendwa kuliko mtu yeyote katika ardhi ya Tanzania.
Akaelezea kifo cha baba yake ambaye alichaguliwa kama balozi nchini Marekani, aliwaeleza kwamba hata kifo chake hakikuwa cha bahati mbaya kama watu waliyovyohisi bali nyuma yake kulikuwa na mkono wa Rais Bokasa ambaye alitaka kuitekekeza familia nzima kwa kuhisi kwamba ingemletea matatizo hapo baadaye.
Hakutaka kuficha kitu, alisimulia kifo cha mama yake, ndugu yake, Irene, jinsi alivyokuwa akitafutwa mpaka alipowekwa katika boksi na kutupwa baharini huku akitakiwa kufa ila mtu mmoja aliyeitwa Kihampa hakutaka kuona hilo likitokea.
Akaelezea namna alivyookolewa na wavuvi wa Japan na kupelekwa nchini humo ambapo alisomea kompyuta na kuwa mkali katika Chuo cha Waseda. Alisimulia kila kitu mpaka alipokuwa akihamisha pesa za viongozi, jinsi alivyowasumbua FIS na kuhakikisha kwamba hapatikani.
Hiyo ndiyo ilikuwa siku ya kuwaambia Watanzania kwamba yeye alikuwa nani, kila mtu alishangaa, wengine wakashindwa kuvumilia kwani mateso na shida alizopitia mwanaume huyo hakika hakukuwa na mtu aliyeamini kwamba kuna binadamu angeweza kupitia maisha hayo.
“Nilitaka kulipa kisasi, na kisasi pekee kilikuwa ni kumuondoa madarakani na kuwapa Watanzania nchi yao. Nimefanikiwa sana,” alisema Godwin hali iliyowafanya Watanzania wengi kufurahi.
“Wengi wanasema kwamba nichukue nafasi ya urais. Ndugu zangu, sikuwa na ndoto za kuwa rais, sikuhangaika kumuondoa madarakani Rais Bokasa ili nije kuwa rais, nilifanya hivyo kwa kuwa nilihitaji kuona Tanzania ikiongozwa na mtu sahihi. Kwangu mimi, nadhani Kambili ni mtu sahihi, mtu mwenye uchungu, mtu ambaye anaweza kufanya kila liwezekanalo sisi kufika kule tunapotaka kufika,” alisema Godwin na kuendelea:
“Ninamshukuru Jenerali Ojuku, kuna mengi amepitia ila ninamwambia kwamba kazi yake ilionekana, nilicheza michezo mingi ya hatari, sikucheza kwa lengo baya, nicheza kama njia ya kumsukuma kunisaidia kumtoa rais huyu madarakani, na kweli imewezekana. Nashukuru kwa wote. Hii akaunti haitofutwa, kwa viongozi wote ambao waliweka pesa zao katika akaunti za Uswisi, nimefunga akaunti, na hata wale viongozi wenye pesa hapa Tanzania, nimezuia pesa zao mpaka kesi zao zitakapokwisha. Kufunga akaunti hizo si kazi ya benki tu, nilifanya hivyo ili kuwasaidia. Nashukuru sana. Karibuni kwenye Tanzania mpya,” alimalizia Godwin, huo ndiyo ukawa mwisho wa video yake iliyogawanywa katika vipande thelathini na mbili.


“Sir! We have got a video,” (mkuu! Tumepata video) ilisikika sauti kutoka upande wa pili.
“What is it about?” (kuhusu nini?)
“Godwin! He has released a video,” (Godwin! Ametoa video) alisikika mwanaume huyo.
Kitendo cha Bwana Kom kusikia jina la Godwin akasikia moyo wake ukipiga paa. Hakuamini, hapohapo akamwambia mwanaume huyo kwamba amtumie video hiyo lakini akaambiwa kwamba ilikuwa katika mtandao wa Instagram ambapo alipoingia katika Akaunti ya Mabadiliko ya Kweli, akaiona video hiyo.
Haikuwa ya Kiingereza, ilikuwa ni ya Kiswahili kitu kilichomfanya kumtafuta mkalimani ambaye alikuja kumfafanulia kila neno lililozungumziwa katika video hiyo.
Hapo ndipo alipojua ukweli kwamba mwanaume huyo hakuwa mhalifu kama alivyokuwa akihisi bali alifanya hivyo kwa kuwa alikuwa akipambana na viongozi waliokuwa wakiihujumu nchi yao na hata kuzichukua zile pesa zilizokuwa zimeibwa nchini mwao.
Aliposikia kila kitu, akakifuata kiti chake na kutulia, akaegemea na kuweka mikono kichwani mwake. Hakuamini kama alikuwa akipambana na mtu aliyekuwa akiipigania nchi yake na kuwatokomeza mafisadi waliokuwa wakiwanyonya kila siku.
“Make a call to Halima! Tell her to leave him alone,” (mpigie simu Halima! Mwambie amuache) alisema Kom na hapohapo Halima kupigiwa simu.


Wakati simu kutoka kwa Kom ilipokuwa ikiingia, Godwin alikuwa akiiona, alijua kwamba kulikuwa na kitu mwanaume huyo alitaka kumwambia msichana huyo. Alichokifanya ni kuiunganisha mpaka kwa Halima ambapo msichana huyo alipopokea, akampa taarifa kwamba alitakiwa kuachana na Godwin kwani kwa kile alichokuwa akikifanya, hakuwa mtu wa kutafutwa na kushtakiwa kwa kuwa kulikuwa na jambo jingine la msingi alilokuwa akilipigania kwa ajili ya nchini yake.
Kwa Halima, hiyo ikaonekana kuwa nafuu, alikuwa amehangaika kwa kipindi kirefu kumtafuta mwanaume huyo lakini hakuwa amempata, kitendo cha kuambiwa kwamba alitakiwa kurudi, akanyanyua mikono na kumshukuru Mungu.
Alikwishawahi kufanya kazi nyingi lakini kwa ile ya kumtafuta Godwin ilikuwa ni ngumu kuliko zote alizowahi kufanya katika maisha yake. Hakutaka kuchelewa, aliona kama Bwana Kom angeahirisha na kumwambia kwamba aendelee kupambana kumtafuta, siku iliyofuata ukawa mwisho wa kukaa nchini Tanzania, akapanda ndege na kurudi zake nchini Somalia kuendelea na majukumu yake mengine.
Kwa Godwin, maisha yalikuwa ni furaha tele, akawa anaendelea kuishi na Winfrida, hakumwambia alikuwa nani, aliishi kisiri, kila kitu kilichokuwa kimetokea alikifanya kuwa siri kubwa mno. Kazi yake ikawa ni kuwasiliana na Kambili, alimwambia kwamba kila kitu kilikuwa tayari na aliamini kwamba baada ya siku kadhaa yeye ndiye angekuwa rais wa nchi hiyo.
“Nashukuru sana,” alisema Kambili.
“Usijali! Ila usifanye kama Bokasa.”
“Sitoweza kufanya. Naomba uniamini! Sitoweza kufanya jambo lolote lile baya. Nimepigana kwa ajili ya nchi hii kwa miaka mingi, nitaonekana sina akili kama tu nitaanza kufanya vitu tofauti na vile ambavyo Watanzania wanavitaka kila siku,” alisema Kambili, aliamini kabisa kwamba alikuwa akienda kuchukua nafasi ya urais kwa kuwa Godwin aliamua kufanya hivyo.
Hakuishia hapo, alichokifanya ni kuwasiliana na Jenerali Ojuku na kumuomba msamaha kwa yote yaliyokuwa yametokea, kuiteka familia yake, halikuwa lengo lake ila alifanya hivyo kwa kuwa alihitaji mabadiliko kwa nguvu kubwa na yote yalifanyika.
“Haikuwa kwa faida yangu, ilikuwa ni kwa faida ya Watanzania, faida ya watoto na wajukuu zako,” alimwambia Ojuku kwenye simu.
“Nashukuru sana. Najua niliumia sana, sikuwa nimelijua lengo lako, si baya, ni zuri ambalo ninaliunga mkono kwa asilimia mia moja,” alisema Ojuku kwenye simu.
“Nashukuru kwa kulifahamu hilo!”
“Ila hutujawahi hata kuonana. Ningependa nimuone huyu shujaa ambaye ameifanya Tanzania kurudi katika heshima yake na kuondokana na udikteta,” alisema Ojuku.
“Tulikwishaonana! Tukazungumza na kufanya mambo mengi sana,” alisema Godwin maneno yaliyomshtua Ojuku.
“Tulishawahi kuonana?”
“Ndiyo! Niliisaidia Tanzania hata kuhamisha pesa za Bokasa alizozituma Ubelgiji,” alisema Godwin.
“Inamaanisha wewe ndiye yule kijana aliyeitwa Denis?”
“Ndiye mimi!”
“Ni kijana mdogo mno!”
“Najua! Ni kijana mdogo lakini mwenye kiu ya kupambana. Nashukuru kwa msaada wako,” alisema Godwin.
“Nashukuru pia. Naomba tuonane japo tule chakula cha mchana!”
“Ningefurahi sana kama ningepata nafasi hiyo. Lakini sina jinsi, hutoweza kuniona tena. Nimefanya kazi ambayo nilitakiwa kuifanya kwa uwezo wangu wote. Popote nitakapokuwa, utakuwa na namba yangu, tutawasiliana, kama kutatokea tatizo lolote lile, naomba uniambie, kama kuna pesa zimeibwa, nijulishe nizirudishe,” alisema Godwin.
“Haina shida. Nakutakia maisha mema!”
“Nashukuru pia kiongozi,” alisema Godwin na kukata simu.
Alimaliza kuzungumza na Ojuku, mtu mmoja wa kipekee aliyetamani sana kuonana naye alikuwa Mchungaji Kihampa. Huyo ndiye aliyekuwa amemuokoa, mtu aliyemuweka kwenye boksi, japokuwa alitakiwa kuuawa lakini mwanaume huyo alimuokoa kwa kumuacaha hai na kuokolewa na Wajapan.
“Ni lazima nimtafute huyu mtu. Ni muhimu sana, siwezi kumuacha,” aliseema Godwin, akasimama na kuanza kujiandaa kwenda kumtembelea mchungaji huyo.


Maofisa wa Usalama wa Taifa wakafika mpaka katika Benki ya Brussels kwa lengo la kwenda kumkamata Bokasa ambaye alikuwa akihitajika sana nchini Tanzania. Walipofika hapo, wakataka kuonana na uongozi wa benki hiyo kwani hapo ndani kila walipoangalia huku na kule, hawakuweza kumuona mtu huyo japokuwa mashine yao ya GPS ilionyesha kwamba simu ile ilikuwa humo ndani.
Kuhusu kuonana na meneja wa benki hiyo hakukuwa na tatizo lolote lile, akapigiwa simu na kuambiwa kwamba kulikuwa na watu waliotaka kuonana naye. Wakaruhusiwa na kwenda ndani ambapo moja kwa moja wakaanza kuzungumza naye.
“Sijawaelewa vizuri! Mmesema rais?” aliuliza meneja huyo huku akiwaangalia kwa mshangao.
“Ndiyo! Picha yake hii hapa!” alisema jamaa mmoja huku akimpa picha yya Bokasa.
“Ooh! Kumbe mnamzungumzia huyU! Mmesema kwamba ni rais! Wa wapi?’ aliuliza meneja huku akishangaa na hapohapo kumwambia kwa kifupi kilichotokea.
Hilo halikuwa tatizo, wakaambiwa kwamba mwanaume huyo hakuwa mahali hapo bali aliiacha simu yake ambayo aliihifadhi katika droo ila mwanaume huyo alikuwa hoi hospitalini.
Hawakutaka kuondoka pasipo kumuona hivyo wakaomba kupelekwa huko kwa lengo la kuonana naye. Wakachukuliwa mpaka hospitalini ambapo kwa ruhusa ya daktari wakapelekwa mpaka katika chumba alichokuwa amelazwa.
Walipofika, wakabaki wakimwangalia. Mwanaume huyo alikuwa akitia huruma kitandani pale, alikuwa kimya, alionekana kuwa na hofu kubwa na hapo kitandani alikuwa akipumulia mashine ya oksijeni tu. Walichokifanya ni kumwambia kwamba alikuwa chini ya ulinzi na alitakiwa kusafirishwa mpaka nchini Tanzania kwa ajili ya kushtakiwa kwa kila kitu kilichokuwa kimetokea pamoja na ubadhilifu wa pesa.
“Daktari! Huyu mgonjwa atatakiwa kupelekwa nchini Tanzania haraka sana!” alisema jamaa mmoja.
“Hapana! Ni mapema sana. Mpeni miezi sita kwani bado hali yake si nzuri kabisa,” alisema daktari kiasi kwamba mawasiliano yakafanyika mpaka nchini Tanzania ambapo wakakubaliana kumpa mtu huyo miezi hiyo kwa ajili ya kupatiwa matibabu na hali yake irudi na kuwa kawaida.
“Haina shida! Kwa kuwa ndiyo utakuwa muda wa uchaguzi, mleteni kipindi hicho, ila awe chini ya uangalizi!” alisikika Jenerali Ojuku.
“Haina shida kiongozi!”


Tangu Kihampa aliposikia sauti moyoni mwake ikimwambia kwamba alitakiwa kuyabadilisha maisha yake, akaamua kubadilika na kumtumikia Mungu kwa moyo mmoja. Hakutaka tena kushiriki katika mauaji yoyote yale, moyo wake ulibadilika na ni kitu kimoja tu ndicho kilichokuwa kikimfurukuta moyoni mwake, kumtumikia Mungu katika roho na kweli.
Baada ya kumuweka Godwin ndani ya boksi lile na kulitupa baharini huku akiwa ameweka maboya ndani yake, akaondoka, hakutaka kurudi tena na hivyo kumpigia simu Rais Bokasa na kumwambia kwamba huo ndiyo ulikuwa mwisho wake wa kutumikishwa kufanya mauaji mbalimbali.
Akaanza kumuabudu Mungu, akajiunga katika Kanisa la Praise And Worship lililokuwa Tabata Bima. Hakutaka kusikia kitu chochote kile mbali na kumuabudu Mungu, akaanza kuwa mshirika wa kanisa hilo, akajiunga na kikundi cha vijana cha kuhubiri Injili sehemu mbalimbali nchini Tanzania na baada ya miaka miwili ya huduma hiyo akaamua kwenda kusomea uchungaji katika Chuo kilichopo mkoani Dodoma.
Moyo wake ukaendelea kubadilika, akaendelea kumuhubiri Mungu sehemu mbalimbali na alipomaliza kusomea masomo ya kichungaji ndipo akakabidhiwa kanisa lililokuwa Magomeni Mapipa jijini Dar es Salaam.
Hapo ndipo ambapo Godwin alitaka kwenda kwa ajili ya kumshukuru kwa kila kitu alichokuwa amemfanyia, aliamini kwamba bila mwanaume huyo basi angekuwa marehemu kwani alikuwa na nguvu zote za kummaliza lakini kitu cha ajabu kabisa ambacho hata yeye mwenyewe alikishangaa, aliyakuta maboya ndani ya boksi na wakati alitekwa na mtu huyo huku akipewa amri ya kummaliza.
Alipofika kanisani hapo kulipokuwa na ibada iliyokuwa ikiendelea, akaelekea nyuma kabisa ya kanisa na kutulia hapo. Macho yake yalikuwa yakiangalia mbele, kulikuwa na kwaya iliyokuwa ikiimba kanisa hapo lakini macho ya Godwin yalikuwa kwa mchungaji huyo aliyetulia katika kiti chake huku akisikiliza kwaya iliyokuwa ikiendelea kumuimbia Mungu.
Hakuwa na haraka, aliendelea kusubiri mpaka pale ibada ilipokwisha ambapo moja kwa oja akamfuata mchungaji huyo kwa lengo la kuzungumza naye na kumwambia kile kilichokuwa kimempeleka mahali pale.
“Bwana Yesu Asifiwe mchungaji,” alisalimia Godwin huku akimwangalia mchungaji huyo ambaye baada ya macho yake kutua usoni mwa Godwin, alihisi kuwahi kumuona sehemu fulani.
“Amen! Hujambo mtumishi wa Mungu?” aliuliza huku akimwangalia kwa mtazamo uliomaanisha kwamba alitaka kukumbuka mahali alipowahi kumuona mwanaume huyo.
“Nashukuru Mungu ni mzima kabisa.”
Bado mchungaji Kihampa alikuwa akiendelea kukumbuka, kichwa chake kilikuwa kikifikiria mbali kabisa, aliendelea kujaribu kuikumbuka sura hiyo lakini alishindwa kabisa. Alipoona kwamba haikuwezekana, akamuuliza ambapo bila tatizo lolote lile Godwin akajitambulisha.
“Godwin?” aliuliza huku akiendelea kumwangalia vizuri kabisa.
“Ndiyo mchungaji!”
“Godwin yupi?”
“Wa boksi lililotupwa baharini miaka mingi iliyopita,” alisema Godwin.
Maneno hayo ndiyo yakamfanya mchungaji huyo kuanza kukumbuka kila kitu kilichokuwa kimetokea, hakuwa mgeni tena, alimkumbuka, yeye ndiye alikuwa mtu pekee aliyemuokoa katika mauti kwa kumuweka maboya kadhaa ndani ya boksi alilokuwa amefungwa na kutupwa baharini.
Hapohapo Kihampa akamsogelea zaidi Godwin na kumkumbatia, moyo wake ukawa na furaha tena kwani kwa kipindi chote hicho hakuwa na uhakika kama kijana huyo alinusurika baharini kama alivyokuwa amekusudia alikuwa alikuwa amekufa baharini.
Hapo ndipo Godwin alipoanza kusimulia kila kitu kilichokuwa kimetokea, ilikuwa ni stori ileile ambayo aliisikia sana midomoni mwa watu mara baada ya kusoma katika mitandao ya kijamii.
“Wewe ndiye huyu Godwin msumbufu aliyeitoa Tanzania katika mikono ya Bokasa?” aliuliza Kihampa.
“Ndiyo! Ninamshukuru Mungu kwamba nilipambana kwa nafasi yangu, alinipigania sana, na ninashukuru kwa sababu bila yeye nadhani nisingeweza kumkimbia Bokasa,” alisema Godwin huku akimwangalia mchungaji huyo.
Walibaki na kuzungumza mambo mengi mno, walifurahi na kucheka pamoja kiasi kwamba hata baadhi ya washirika wa kanisa hilo walikuwa wakishangaa, hawakuwahi kumuona mchungaji wao akiongea na mtu mmoja kwa kipindi kirefu kama ilivyokuwa kwa kijana huyo.
Walitumia dakika kadhaa na walipomaliza, Godwin akaondoka kurudi nyumbani ambapo huko akawasiliana na Kambili na kumwambia kwamba alitakiwa kujiandaa kwani uchaguzi mkuu ungeitishwa na yeye kuwa miongoni mwa wagombea ambao walitakiwa kugombea, kwa hiyo alitakiwa kuwaahidi wananchi vile tu ambavyo atavifanya katika uongozi wake, asivyoviweza, aachane navyo.
“Haina shida! Ila kuna siku ningependa sana kukuona,” alisema Kambili.
“Usijali! Kuna siku utaniona, tutazungumza sana, ila bahati mbaya hutonijua kama ndiye mimi,” alisema Godwin kwenye simu.
“Kwa nini unataka kujificha kila siku?”
“Kwa sababu vita vizuri ni kupambana na mtu asiyekujua. Nipo kwa ajili ya Watanzania, tukiongea na kuonana mara kwa mara, utajenga urafiki nami, siku ukifanya ujinga, sitokufanya kitu kwa kuwa wewe ni rafiki yangu, ila ili niwe na nguvu ya kukufanya lolote lile, ni lazima nisiwe rafiki yako, ili siku nikikupiga, nimpige mtu asiyekuwa rafiki yangu,” alijibu Godwin.
“Haina shida! Nitahakikisha napambana kufanya kila kitu ambacho Watanzania wengi wamekuwa wakihitaji kutoka kwangu,” alisema Kambili.
“Nashukuru sana.”
Japokuwa hakuwa na cheo chochote kile lakini Jenerali Ojuku alikuwa akimheshimu mno Godwin, kila alipokuwa akimpigia simu, kwa jinsi alivyokuwa akizungumza naye alizungumza kiheshima, alionekana kama kiongozi wake kiasi kwamba kwa lolote lile ambalo angelisema mwanaume huyo angemuunga mkono kwa asilimia mia moja.
Siku zikaendelea kukatika, miezi sita ilipokatika watu wakawa na hamu ya kuingia katika uchaguzi mkuu ambao haukufanyika nchini humo ngazi ya rais kwa takribani miaka kumi na ishirini, kila mtu alitaka kushuhudia kile ambacho kingetokea.
Wagombea waliokuwa wakigombea nafasi hiyo waliendelea kupiga kampeni ya kuzunguka kila kona nchini Tanzania kuhakikisha kwamba wanachaguliwa na kuiongoza nchi hiyo. Kambili hakuwa na tabu, aliamini kwamba jina la Godwin lingeweza kumpa nafasi hiyo na kila alipokuwa akisimama jukwaani, alisema wazi kwamba angeiongoza nchi hiyo kwani hata Godwin alimuamini kwamba anaweza kufanya yale ambayo Watanzania wote wangependa ayafanye kwa miaka mitano ya kwanza.
“Naombeni mnipe dhamana! Nitahakikisha Tanzania mpya inarudi, kama Godwin ameniamini, kwa nini usiniamini? Nawaahidi wote kwamba sitawaangusha,” alisema Kambili alipokuwa akizungumza na wananchi
“Umepita baba!” alisikika mwanamke mmoja akisema kwa sauti.
“Nimepita?” aliuliza.
“Ndiyoooooo!” watu wote waliitikia kwa sa
Kampeni zilikuwa zikiendelea kila siku, katika kila mkoa ambao Kambili alikuwa akisimama na kuzungumza, Godwin alikuwa kwenye umati wa mkutano huo. Hakukuwa na mtu aliyemfahamu, alikuwa akisikia mauoni ya watu mbalimbali na kila mtu ambaye alimzungumzia Kambili, alisema wazi kuwa kura yake ingekwenda kwa mtu huyo kwa sababu tu Godwin alimwamini.
“Nitampa jamaa kura yangu kwa kuwa Godwin amemwamini! Kama Godwin amekukubali, kwa nini mimi nisikukubali? Ni lazima nikukubali kwani yule jamaa ndiye mkombozi wetu,” alisema mwanaume mmoja huku akionekana kuwa na furaha tele.


“Mpo wapi?”
“Nairobee! Kuna lolote the big boss?” ilisikika sauti ya mtu mwingine.
“Mnaweza kuja huku Mombasa mara moja!”
“Hakuna shida, tunakuja!”
“Sawa. Nawasubir! Njooni haraka sana hapa white house,” alisema mwanaume mmoja.
“Okay!”
Yalikuwa mazungumzo baina ya watu wawili waliokuwa wakiwasiliana kwa njia ya simu. Mmoja alikuwa Mombasa na mwingine jijini Nairobi nchini Kenya. Mazungumzo yao hayakuwa marefu sana, wakakata simu na kila mtu kuendelea na mambo yake.
Mwanaume aliyevalia suti alikaa nyuma ya meza yake katika ofisi yake iliyokuwa ndani ya jumba moja kubwa ambalo kila mtu hapo Mombasa aliliita kwa jina la White House kama ilivyoitwa ikulu ya Marekani. Muda wote mwanaume huyu alikuwa na sigara kubwa aina ya sigar mdomoni mwake, alikaa kwa kujiachia na mezani kwake kulikuwa na mafaili mengi pamoja na cd ambazo ni yeye tu ndiye alijua humo kulikuwa na nini.
Mwanaume huyu aliitwa Stephano Olotu, alikuwa miongoni mwa wafanyabiashara wakubwa nchini Kenya. Alimiliki utajiri wa dola bilioni mbili ambazo zilikuwa ni zaidi ya shilingi trilioni 4, alikuwa na migahawa mingi jijini Nairobi, migodi ya dhahabu na pia alimiliki kisima cha mafuta nchini Nigeria.
Japokuwa alikuwa mfanyabiashara aliyekuwa na mafanikio makubwa na hata kufanya biashara za halali kabisa lakini nyuma ya pazia mwanaume huyo alikuwa na michezo mingi ya hatari. Alijishughulisha na uuzaji wa madawa ya kulevya, maisha yake yalikuwa ni kutanua na wanawake mbalimbali Afrika nzima. Kwa kuwa alikuwa na jina kubwa alilitumia vilivyo kuweka mikakati kabambe kuzoeana na marais wengi ili kuweza kufanya biashara zake za madawa ya kulevya.
Miongoni mwa marais waliokuwa wakipiga naye mishemishe alikuwa Rais Bokasa, alitumia kiasi kikubwa cha pesa kuwekeza nchini Tanzania, huko, aliwatafuta wafanyabiashara wenzake ambao walikuwa wakifanya biashara haramu ya madawa ya kulevya kwa kupitia mgongo wa rais huyo.
Hakuwa akiwafahamu wafanyabiashara hao, Bokasa alikuwa mjanja, alimwambia kwamba mzigo ulitakiwa kufika kwake kwanza na yeye kuwafikishia hao wafanyabiashara wengine ambapo ulipokwisha, alichukua asilimia kumi na tisini ya pesa iliyolipwa kwenda kwa Olotu.
Hayo ndiyo yalikuwa maisha yake. Katika kipindi chote hicho Bokasa hakutaka kumruhusu Olotu kuwafahamu wafanyabiashara wengine aliokuwa akifanya nao biashara hiyo kwani alijua kwamba kama angeruhusu hilo basi kusingekuwa na ulazima wa Olotu kumtafuta na kuwauzia wenzake mzigo mkubwa ambao alikuwa akiutuma nchini humo.
Bokasa aliondolewa madarakani huku akiwa bado hajakabidhi pesa alizokuwa ameuza mzigo mkubwa uliokuwa na thamani ya shilingi bilioni mia tatu. Olotu alichanganyikiwa, hakuamini kama kweli pesa zake asingezipata kwa kuwa tu rais huyo alikuwa ameondolewa madarakani.
Kwa kipindi hicho alihitaji pesa hizo, hakuwa na njia nyingine za kupata mzigo huo zaidi ya kumuuliza Bokasa juu majina ya wafanyabishara aliokuwa akiwauzia kwani alifanya siri lakini kwa hatua aliyokuwa amefikia, hakukuwa na siri tena, alitaka kuambiwa ili awafuate na kudai pesa zake.
Kumpata Bokasa halikuwa jambo jepesi, mwanaume huyo alikuwa nchini Ubelgiji akiendelea kupata matibabu, hakukubali kuona akifa pasipo kumwambia ukweli juu ya mzigo wake hivyo kitu pekee alichokiamua ni kuwasiliana na vijana wake, wasafiri mpaka nchini huko na kumuuliza juu ya wafanyabisahara hao, na kama hataki kuwaambia ukweli basi wamteke, waondoke naye mpaka nchini Kenya ambapo angefanya kitu kimoja tu, kumuua ili kuiridhisha nafsi yake kwa dhuluma aliyokuwa akifanyiwa.
Baada ya saa mbili, vijana wale aliowapigia simu wakafika Mombasa na kuanza kuzungumza nao, aliwaambia hitaji lake kwamba alitaka wao wasafiri mpaka nchini Ubelgiji ambapo huko wangekwenda mpaka katika hospitali aliyolazwa na kumteka huko.
Mipango ikapangwa ndani ya jumba hilo kubwa na hivyo kutakiwa kwenda nchini humo kwa ajili ya kuhakikisha mwanaume huyo anapelekwa haraka sana mikononi mwake na kufanya kile alichotaka kukifanya.
“Hana ulinzi?” aliuliza kijana mmoja, huyo aliitwa Wilson.
“Sijajua! Ila nina uhakika hana ulinzi, atakuwaje na ulinzi na wakati hapendwi? Ninachokitaka ni kujua majina ya wafanyabiashara aliokuwa akifanya nao biashara yangu,” alisema Olotu.
“Basi haina shida.”
Baada ya siku tatu wanaume wawili, Wilson na Okotee wakaondoka nchini Kenya na kwenda Ubelgiji kwa ajili ya kukamilisha kile walichoambiwa. Hawakuona kama wangepata tabu kwani tayari waliambiwa kuwa Bokasa alikuwa katika Hospitali ya Clinique Saint Jean iliyokuwa katika Jiji la Brussels akiendelea kupatiwa matibabu kutokana na tatizo la presha alilokuwa amelipata.
“Tukifika, ni kumchukua na kurudi naye, sidhani kama tutashindwa. Cha msingi ndege ya rais binafsi iandaliwe kwa ajili ya kuondoka naye,” alisema Wilson, kwao, kitendo cha kumchukua Bokasa na kwenda naye nchini Kenya hakukuwa na tatizo lolote lile, ilikuwa ni kama kumsukuma mlevi katika mteremko wa mlima.
Wakati vijana hao wakiwa njiani, alichokifanya Olotu ni kumpigia simu Rais Onyango wa hapo Kenya na kumwambia kuhusu lengo lake. Alimwambia ukweli kuhusu mzigo wa madawa ya kulevya ambao kipindi hicho hakujua uliuzwa kwa wafanyabiashara gani nchini Tanzania, ilitakiwa mtu huyo achukuliwe kutoka Ubelgiji na kupelekwa Kenya kwa lengo la kuwajua watu hao.
“Si tatizo! Unataka nikusaidie nini Olotu?” aliuliza Rais Onyango.
“Ndege yako kwenda kumsafirisha kutoka Ubelgiji kuja huku!” alijibu Olotu.
“Una uhakika ataweza kutolewa hospitalini?” aliuliza.
“Hilo si tatizo!”
“Unajua kama kuna ulinzi huko?”
“Ulinzi gani?”
“Tanzania imetuma ulinzi, kuna watu wanamlinda usiku na mchana mahali hapo.”
“Haina shida! Watu niliowatuma ni hatari sana. Hata kama utaweka ulinzi wa Kimarekani, mwisho wa siku tunapata tunachokitaka,” alitamba Olotu.
“Basi sawa. Wasiliana nao, waulize siku gani huyo mtu atakuwa mikononi mwao kwa lengo la kumchukua na kumsafirisha!”
“Haina shida. Ila nafikiri baada ya siku tatu. Yaani Jumatano kila kitu kitakuwa sawa.”
“Haina shida.”


Bokasa alikuwa kitandani, aliendelea kupumulia mashine ya hewa ya oksijeni, hakuwa na nguvu kitandani pale na kila muda macho yake yalikuwa yakiangalia huku na kule. Alipewa taarifa kwamba kulikuwa na maofisa wa Usalama wa Taifa ambao walikuwa hapo kwa lengo la kumlinda na kuhakikisha wanasafiri naye kuelekea nchini Tanzania mara baada ya kupata nafuu.
Hakutaka kurudi Tanzania, alitamani kuendelea kubaki nchini humo, alijua dhahiri kile kilichokuwa kikienda kutokea mara baada ya kufika huko. Hakutaka kwenda, hakutaka kuona akifungwa gerezani kwa maovu yote aliyokuwa ameyafanya katika kipindi alichokuwa rais wa nchi hiyo.
Kwa kuwa kulikuwa na kazi kubwa, wakaongezwa maofisa wa Usalama wa Taifa wengine ili wawe wanabadilishana mpaka pale ambapo mwanaume huyo angepata nafuu na kupelekwa nchini Tanzania.
“Doctor! There is something we have to discuss,” (dokta! Kuna kitu nataka tujadili) alisikika msichana fulani kutoka kwenye simu, alimpigia simu daktari mkuu wa hospitali hiyo, Dk. Thump.
“Who are you?” (wewe nani?)
“Amanda Kalulu.”
“What is it about?” (kuhusu nini?)
“About my uncle!” (kuhusu mjomba wangu)
“Who is that?” (nani huyo?)
“Bokasa!”
Alipolitaja jina hilo tu daktari akajua ni mtu gani alikuwa akizungumziwa. Hakumjua msichana huyo aliyempigia simu ambaye alitaka sana kuonana naye. Hilo halikuwa tatizo, akamwambia kwamba kama inawezekana basi waonane na kuzungumza kuhusu mwanaume huyo.
Baada ya saa mbili wakaonana ndani ya hospitali hiyo na kuanza kuzungumza. Mwanamke mrembo alikuwa katika kiti cha wageni ndani ya ofisi ya daktari huyo, alifika mahali hapo kwa ajili ya kuzungumza naye kuhusu mgonjwa aliyekuwa ameletwa ambaye alisema kwamba alikuwa mjomba wake.
Walikaa na kuzungumza mambo mengi, alimwambia kuhusu rais huyo kwamba alikuwa mjomba wake kabisa na alisikitishwa kwa taarifa ya ugonjwa aliokuwa nao ambao ulisababisha kupelekwa ndani ya hospitali hiyo.
“Lengo lako ni nini?” aliuliza Dk. Thump.
“Tumekaa kama familia na kuamua jambo moja!” alisema.
“Lipi?”
“Kumpeleka mgonjwa wetu nchini Ufaransa. Anateseka na tunaona kabisa matibabu ya hapa si mazuri kama ambavyo yanatakiwa kuwa. Miezi sita ni mingi sana,” alisema mwanamke huyo.
Dokta Thump alibaki akimwangalia mwanamke huyo, kwa jinsi muonekano wake ulivyokuwa ilikuwa vigumu mno kugundua kwamba hakukuwa na uhusiano wowote ule baina yake na mgonjwa aliyekuwa amelazwa ila kwa kuwa alikuwa akiongea kwa huruma sana na wakati mwingine machozi kumtiririka, daktari akajihisi hukumu kubwa moyoni mwake.
Wakati wakizungumza, mara simu ya mwanamke yule ikaanza kuita, hakutaka kuchelewa, akaipokea na kuanza kuzungumza na mwanaume wa upande wa pili, kwa jinsi mazungumzo yao yalivyokuwa, ilionyesha kabisa kwamba aliyepiga simu alikuwa ndugu yake ambaye naye alitaka kufahamu hali aliyokuwa nayo Bokasa.
“Ni mgonjwa mno. Kama ndugu tulivyokubaliana, inabidi asafirishwe na kuelekea nchini Ufaransa,” alisema mwanamke huyo.
“Sawa. Nakuja na familia yangu kumuona,” alisikika mwanaume huyo wa upande wa pili.
Hicho ndicho kilichofanyika, ndani ya nusu saa, mwanaume mwenye ndevu nyingi akafika hospitalini hapo na moja kwa moja kuonana na Dk. Thump huku akiwa na familia yake ya watu sita.
“Kaka anaendeleaje?” aliuliza mwanaume huyo huku akimwangalia Amanda.
“Ni mgonjwa sana, miezi sita ni mingi mno, hatutokuwa tayari kusubiri kipindi chote hicho,” alisema Amanda huku akimkumbatia ndugu yake huyo aliyejitambulisha kwa daktari kwa jina la Sebastian Gambole.
Ilikuwa ni vigumu sana kugundua kwamba huo ulikuwa mchezo uliokuwa umepangwa, watu hao walikuwa mahali hapo kwa lengo la kumtorosha Bokasa na kuelekea nchini Kenya ambapo tayari walikutana na Wilson na mwenzake na kupanga ni kwa jinsi gani mwanaume huyo alitakiwa kusafirishwa kuelekea huko badala ya Ufaransa kama walivyokuwa wamemwambia daktari.
Kitu cha kwanza walichohitaji ni kuonana na mgonjwa wao, hilo halikuwa tatizo, wakapelekwa katika wodi ile na kuonana naye ambapo huko wakampiga picha na kumtumia Wilson ambaye alithibitisha kwamba huyo ndiye mtu aliyetakiwa kusafirishwa.
“It is him!” (ndiye yeye!)
“Okay!” (sawa)


Ilikuwa kazi ambayo ilitakiwa kufanyika haraka sana kabla ya watu kujua kile kilichokuwa kikiendelea. Walichokifanya mara baada ya kumpiga picha na Wilson kusema kwamba alikuwa ndiye mtu aliyehitajika, wakaondoka hospitalini hapo na kwenda kupanga mikakati ya kumtoa mwanaume huyo katika hospitali hiyo pasipo mtu wale walinzi kutoka Tanzania kufahamu chochote kile.
Mpango waliokubaliana ilikuwa ni lazima wajifanye madaktari ili iwe rahisi kuingia na kuondoka humo na mtu huyo lakini pia kwa Wilson na Okotee walitakiwa kujifanya madaktari waliokuwa wakizungumziwa kutoka nchini Ufaransa ambao walifika mahali hapo kwa lengo la kumchukua Bokasa.
“Na itakuwaje kuhusu Dk. Thump?” aliuliza Amanda.
“Ni kazi nyepesi sana. Kwa kuwa amekubaliana nanyi, hakuna tatizo, kitakachotakiwa ni kumlazimisha kufanya kile tunachokihitaji au vinginevyo tumuue,” alisema Wilson.
“Sawa. Haina shida kama ni hivyo!”
Walitakiw akujiandaa, Dk. Thump hakutakiwa kuhusika, aliambiwa kwamba ndugu wa mgonjwa ndiyo waliokuwa wakishughulikia kila kitu na wao ndiyo waliokuwa wakijia ni hospitali gani mgonjwa wao alitakiwa kwenda.
Hilo halikuwa tatizo, kitu pekee alichokiandaa ni ripoti kuhusu ugonjwa wa Bokasa ambayo ndiyo walitakiwa kupewa madaktari na hivyo kuondoka naye. Ndege ikaandaliwa tayari kwa kuanza safari ya kuelekea nchini Kenya, kitu pekee kilichobaki ni kuona kama kungekuwa na uwezekano wa kuondoka mahali hapo pasipo wale Usalama wa Taifa wa Tanzania kujua kilichokuwa kikiendelea.
“Hivi kile chumba hakina mlango wa nyuma?” aliuliza Okotee.
“Unao! Niliangalia tulipokwenda kumuona, tuliuona mlango wa nyuma,” alisema Amanda.
“Basi itakuwa vizuri kama tukiutumia huo,” alisema Wilson.
Walipanga mipango yao, ilipokamilika, siku iliyofuata Amanda na wenzake walitakiwa kwenda huko kwa ajili ya kukamilisha mipango midogomidogo iliyokuwa imebaki. Walipofika katika hospitali hiyo wakawasiliana na Dk. Sebastian na kumwambia kwamba madaktari kutoka nchini Ufaransa ambao walikuwa wameandaliwa na familia waliwasili nchini humo.
“Nitatakiwa kuonana nao na kuwapa ripoti kuhusu mgonjwa huyo,” alisema.
Hilo halikuwa tatizo, wakasubiri na ilipofika majira ya saa nane mchana, Wilson na Okotee wakaenda mpaka hospitalini hapo na kuanza kuzungumza naye. Walizungumza Kiingereza kizuri kabisa huku wakati mwingine wakichanganya na Kifaransa ili kuvuta uasilia wa kile walichokuwa wakikitaka mahali hapo.
“Ripoti inasemaje?” aliuliza Wilson huku akimwangalia Dk. Sebastian.
“Ana tatizo la presha, hilo tu!”
“Basi sawa.”
Walijifanya kuwa bize kukagua ripoti hiyo na baada ya muda wakamwambia kwamba walitakiwa kumuona mgonjwa wao ili wajue ni kwa namna gani walitakiwa kufanya kazi ya kumsafirisha na kumpeleka nchini Ufaransa.
Walipoingia ndani ya chumba hicho, umakini wao haukuwa kwa mgonjwa, walikuwa wakiangalia mazingira ya chumba hicho na ule mlango walioambiwa kwamba ulikuwa humo. Walipojiridhisha, wakawaambia watu wote watoke ili wamchunguze kwa umakini?
“Mpaka sisi?” aliuliza Wilson.
“Ndiyo! Kila mtu!” alijibu Wilson huku akijifanya kama mtu aliyekuwa makini kwa kile alichokifanya.
Manesi waliokuwa humo, madaktari kutoka katika hospitali hiyo wakatoka ndani, ilikuwa ni lazima wamchunguze mgonjwa zaidi, lakini lengo la kufanya hivyo ilikuwa ni kama kumuandaa kwa safari pasipo walinzi kufahamu chochote kile.
Maofisa wale wa Usalama wa Taifa hawakutakiwa kuingia ndani, ulinzi wao waliufanya nje ya chumba kile, walisimama imara pasipo kuzungumza na mtu yeyote yule, kila kitu kilichokuwa kikiendelea walikuwa wakikiangalia kwa umakini kabisa na hawakuyatilia ulakini kwa kuwa walikuwa wakishirikiana na madaktari wa hospitali hiyo.
Kitendo cha Amanda na wenzake kutoka nje ulikuwa ni mpango ambao uliandaliwa, hawakukaa hapo, wakaondoka mpaka nje ya hospitali hiyo ambapo huko wakaandaa gari lao, wakazunguka kwa nyuma mpaka ulipokuwa mlango ule wa nyuma wa kuingilia ndani ya chumba kile na kuanza kugonga.
Wilson na Okotee wakajua kwamba hao walikuwa watu wao, wakaufungua mlango, wakaanza kukisukuma kitanda kile kupitia mlango ule na kukitoa nje huku Bokasa akiwa kitandani akishangaa, hakupewa taarifa juu ya kilichokuwa kikiendelea, aliona kama kulikuwa na mchezo uliokuwa ukifanyika.
Hawakutakiwa kugundulika hivyo Amanda na mwenzake wakaondoka na kuwaacha Wilson na mwenzake wakiisukuma machela kule nje. Kila mtu aliyekuwa akipishana naye hakuwa na wasiwasi nao, muonekano wao kuanzia mavazi, miwani waliyoivaa ilionyesha kabisa kwamba walikuwa madaktari hivyo kumpeleka Bokasa kwenye gari walilokuwa wamekuja nalo.
Hakukuwa na mtu aliyehoji kitu chochote kile, kitu cha ajabu hata manesi wengine waliokuwa wakikiona kitendo kile waliona ni kawaida sana, imani yao ilikuwa kubwa kwa madaktari hivyo kuhisi kwamba wale walikuwa madaktari wa hospitali hiyo na iliwezekana mgonjwa huyo alikuwa akihamishwa hospitali kwa matibabu zaidi.
Hawakuzungumza kitu, wakaingia ndani ya gari ambapo likawashwa king’ora na kuondoka mahali hapo kuelekea uwanja wa ndege. Kazi hiyo mara ya kwana ilionekana kuwa kubwa mno lakini baada ya kuifanya wakagundua kuwa ilikuwa kazi nyepesi mno ambayo isingeweza kuwasumbua hata kidogo.
“Kumbe ni nyepesi hivi! Haki ya Mungu tumemsukuma mlevi kwenye mteremko wa mlima,” alisema Wilson huku akimwangalia mwenzake kwa furaha kwani kile walichokuwa wamekifanya kilionekana kuwa kitu chepesi kuliko vyote walivyowahi kuvifanya.
Wakati hayo yakiwa yametokea, Dk. Sebastian alikuwa ofisini kwake, kitu pekee ambacho alijua ni kwamba madaktari wake walikuwa wakishughulika na mgonjwa ambaye alikuwa akiandaliwa tayari kwa kusafirishwa na kupelekwa nchini Ufaransa kwa ajili ya matibabu.
Baada ya dakika kadhaa, akaamua kutoka ndani na kuelekea kule. Huko, akaanza kuhisi kulikuwa na kitu kinaendelea kwani alipofika hapo, alishangaa kuwaona manesi wakiwa nje ya chumba kile pamoja na walinzi.
Hilo halikuwa jambo la kawaida, akawasogelea na kuwauliza sababu ya kuwepo hapo nje ambapo walimwambia kwamba wale madaktari walikuwa ndani ya chumba kile wakimwangalia zaidi mgonjwa wao.
“Wapo ndani wakimwangalia mgonjwa wao?” aliuliza Dk. Sebastian huku akiashangaa.
“Ndiyo!”
“Kivipi? Mbona hili ni jambo tofauti sana na utaratibu wetu!?” aliuliza Dk. Sebastian huku akiwaangalia kwa mshangao mkubwa.
Akaufuata mlango kwa lengo la kuufungua, alipofanya hivyo, mlango haukufunguka. Alishangaa, ilikuwaje madaktari hao wawe ndani huku manesi wake wakiwa nje? Ila jambo jingine ambalo lilimshangaza, kwa nini ndugu wa mgonjwa huyo hawakuwa mahali hapo?
“Na ndugu zao?”
“Waliondoka!”
Alipopewa jibu hilo tu akahisi kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea, akaugonga mlango, haukufunguliwa, akaugonga zaidi na matokeo yakawa vilevile hali iliyomtia hofu. Hawakuwa na jinsi, kama hali iliendelea hivyo ilikuwa ni lazima kuuvunja mlango, kitu walichotaka ni kujua kilichokuwa kikiendelea ndani ya chumba hicho.
Mlango ukavunjwa na walipoingia, hawakuwakuta madaktari, na mbaya zaidi hata mgonjwa hakuwa akionekana kitandani hapo hali iliyomshangaza kila mmoja.
Wakaitana, kila mtu aliyekuwa akiangalia kilichokuwa kimetokea, alishangaa. Usalama wa Taifa walipopewa taarifa, wakachanganyikiwa hivyo kuanza kuwatafuta watu hao hapo hospitalini. Walikuwa wamekwishachelewa kwani hata walipouliza walinzi wa getini waliwaambia kwamba kuna gari la wagonjwa liliondoka kama dakika ishirini na tano zilizopita.
“Kuna gari liliondoka? Lina namba zipi?” aliuliza Dk. Sebastian! Akili yake iliruka.
“Bel89J0,” alijibu mlinzi.
“Hatuna gari hilo! Ni la hapa hospitali?”
“Hapana! Hilo sikuwahi kuliona. Na tulishindwa kuuliza chochote kwa kuwa tulijua kwamba ni madaktari ambao mlikubaliana nao kumchukua mgonjwa!” alisema mlinzi maneno yaliyomchanganya zaidi Dk. Sebastian.
Hakutaka kukubali, hakukukalika, akachukua simu na kukipigia kitengo cha ulinzi wa barabarani, akawaambia kwamba kulikuwa na tatizo limetokea, gari moja la wagonjwa liliondoka hospitalini huku likiwa na mgonjwa, hawakujua ni wapi lilielekea lakini baada ya kutaja namba zake, akaambiwa kwamba kamera za barabarani zililinasa gari hilo likielekea uwanja wa ndege.
“Unasema?”
“Kamera zinaonyesha hivyo!”
Hakutaka kuchelewa, haraka sana akawapigia simu polisi wa uwanja wa ndege. Alichanganyikiwa, kitendo cha mgonjwa huyo kuibwa hospitalini hapo kilionyesha kabisa kwamba angekuwa kwenye matatizo makubwa na angeweza hata kufukuzwa kazi, alipopiga huko, akaambiwa kwamba gari hilo lilikuwepo kwani liliingia mpaka ndani kabisa ya uwanja huo.
“Hebu lizuieni. Kuna mgonjwa humo ameibwa. Lizuieni,” alipiga kelele Dk. Sebastian huku akivua koti lake tayari kwa kwenda huko uwanjani.

Je, nini kitaendelea?

Hii riwaya pelekea wizara ya elimu watahinie wanafunzi.

Kusoma yote sio leo.
See you later…

Mimi sasa nisome? Mimi?

https://i.gifer.com/GNzD.gif

Hata summary sitaki.

Kwani ni setbook

WTF!

Audio tafadhali

Good read, leta part 2

Afadhali ata ingekua kisungu

Weka summary SV.

Pati kujia ndugu yako.

:D:D

[ATTACH=full]191640[/ATTACH]