https://wingulamashahidi.org/wp-content/uploads/2020/11/footsteps-in-the-sand.jpg
Shalom, Jina la Bwana Yesu libarikiwe, karibu tuyatafakari maandiko pamoja…
Ukifika mahali umepotea, na huoni mtu hata mmoja mbele yako wa kukupa msaada, lakini unapotazama chini, unaona nyayo za miguu zinaelekea upande fulani…bila shaka hatua inayofuata ni kuzifuata hizo nyayo, kwasababu unajua mwisho wa hizo nyayo ni kumfikia huyo mtu alipo.
Na Kristo sasa hayupo hapa duniani kwa namna ya mwili, yupo juu mbinguni…lakini katuachia nyayo…ambazo katika hizo tukizifuata tutamfikia yeye na kumwona macho kwa macho.
Sasa nyanyo hizo ni zipi?
Neno la Mungu linasema…
[INDENT]1Petro 2:20 “Kwa maana ni sifa gani kustahimili, mtendapo dhambi na kupigwa makofi? Lakini kustahimili, mtendapo mema na kupata mateso, huu ndio wema hasa mbele za Mungu.
21 Kwa sababu ndio mlioitiwa; maana Kristo naye aliteswa kwa ajili yenu, AKAWAACHIA KIELELEZO, MFUATE NYAYO ZAKE.
22 Yeye hakutenda dhambi, wala hila haikuonekana kinywani mwake.
23 YEYE ALIPOTUKANWA, HAKURUDISHA MATUKANO; alipoteswa, hakuogofya; bali alijikabidhi kwake yeye ahukumuye kwa haki”.[/INDENT]
Tunapokuwa wapole kama Yesu alivyokuwa hapo tunaziendea nyayo zake, katika hii dunia iliyojaa upotofu, tunapostahimili mabaya, tunapotukanwa haturudishi majibu kama yeye, tunapoudhiwa ni lazima tusamehe…hapo tunazifuata nyanyo zake…na tutakapomaliza mwendo tukiwa tumezifuata nyayo hizo ni lazima tutamfikia hatutapotea.
Lakini sasa kuna nyayo nyingi duniani, kila mtu anatengeneza nyayo zake…mfano wa nyayo potofu ni hizi zinazosema… “mpende akupendaye, asiyekupenda mchukie”… Hizi ni nyayo ambazo zinaonekana ni za faraja na za kujilinda, lakini ni nyayo potofu, mwisho wake ni upotevuni…Mwisho wake ni ziwa la moto.
Hivyo tusijifanye tunajua kumsahihisha Bwana Yesu Kristo na kufikiri, hakupaswa kuwa mpole vile… Siku zote fahamu kuwa Yesu alikuwa na uwezo wa kuwapoteza maadui zake pale kwa dakika moja tu, wala hakuna mtu ambaye angeweza kumgusa. Lakini hakuutumia huo uwezo kwasababu lengo lake ni hao watu watubu kwa wema wake…
Ndicho kitu Yesu anachotaka kwetu pia, kwamba kwa wema wetu, wengi wavutwe kwake…Lakini kama tukijiona kwamba sisi tuna ufunuo kuliko yeye, kwamba hatupaswi kuwa wapole, na wanyenyekevu, hatupaswi kuwa watu wa kusamehe wanaotuudhi, hizo njia tunazoziendea tutajikuta kwenye ziwa la moto.
[INDENT]Mathayo 26:51 “Na tazama, mmoja wao waliokuwa pamoja na Yesu akanyosha mkono wake, akaufuta upanga wake, akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio.
52 Ndipo Yesu akamwambia, Rudisha upanga wako mahali pake, maana wote waushikao upanga, wataangamia kwa upanga.
53 Ama wadhani ya kuwa mimi siwezi kumsihi Baba yangu, naye ataniletea sasa hivi zaidi ya majeshi kumi na mawili ya malaika?”[/INDENT]
Soma tena…
[INDENT]Luka 9:52 “akatuma wajumbe kutangulia mbele ya uso wake; wakaenda wakaingia katika kijiji cha Wasamaria, ili kumtengenezea mahali.
53 Lakini wenyeji hawakumkaribisha kwa vile alivyouelekeza uso wake kwenda Yerusalemu.
54 Wanafunzi wake Yakobo na Yohana walipoona hayo, walisema, Bwana, wataka tuagize moto ushuke kutoka mbinguni, uwaangamize; [kama Eliya naye alivyofanya]?
55 Akawageukia, akawakanya. [Akasema, Hamjui ni roho ya namna gani mliyo nayo.]
56 Kwa maana Mwana wa Adamu hakuja kuziangamiza roho za watu, bali kuziokoa. Wakaondoka wakaenda mpaka kijiji kingine”.[/INDENT]
Bwana atupe macho ya kuona nyayo zake, na kuzifuatia katika Jina la Yesu.
Maran atha.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312