NINI MAANA YA KUISHI KWA KUUKOMBOA WAKATI?

Shalom mwana wa Mungu, ikiwa Mungu amekupa neema ya kuiona siku hii ya leo, basi usipuuze kujifunza ni kitu gani anataka kutoka kwako leo?, Kukutana na ujumbe huu si kwa bahati mbaya bali Mungu anakusudi na wewe juu ya wakati aliokupa hapa duniani.

[INDENT]Tukisoma Waefeso 5:15-18 biblia inatuambia hivi… “15 Basi angalieni sana jinsi mnavyoenenda; si kama watu wasio na hekima bali kama watu wenye hekima;
16 MKIUKOMBOA WAKATI kwa maana zamani hizi ni za uovu.
17 Kwa sababu hiyo msiwe wajinga, bali mfahamu ni nini yaliyo mapenzi ya Bwana.
18 Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi; bali mjazwe Roho;”.
[/INDENT]

Nataka leo tujifunze nini maana ya kuukomboa wakati kimaandiko. Tunajua tafsiri rahisi ya hili neno kuukomboa wakati ni “kuutumia muda vizuri”, tulipokuwa shuleni moja ya vitu ambavyo vilikuwa vinawachukiza sana waalimu ni pale walipokuwa wanaona wanafunzi wanautumia muda wao vibaya (hawaukomboi wakati), Hususani pale mwalimu anapotazama muda waliobakiwa nao mbeleni jinsi ulivyo mchache, topics bado ni nyingi za kusoma, halafu mwanafunzi, anaruka ruka hajisomei, anapiga kilele darasani, hazingatii masomo, haudhurii darasani, inawatia sana hasira waalimu pamoja na wazazi. Vivyo hivyo na katika mambo mengine.

Lakini pia katika upande wa maandiko, tunafundishwa tuukomboe wakati, kwasababu biblia imeweka wazi kabisa kuwa zamani hizi ni za UOVU, na tunauokomboa wakati kwa namna gani? Biblia inasema ni kwa kutaka kufahamu ni nini yaliyo mapenzi ya Mungu kwetu.Huko ndiko kuukomboa wakati kuliko na maana mbele za Mungu.

Ndugu huu ulimwengu una mambo mengi na mahangaiko mengi, Ni kweli tunafahamu kwa sehemu moja au nyingine hatuwezi kuepuka mihangaiko kama ipo lakini tunaonywa tuishi kama watu wenye hekima, na sio wajinga, tukijua kuwa sisi ni wapitaji tu hapa duniani, na siku zetu zinakimbia kwa kasi sana, biblia inasema sisi ni kama MVUKE uonekanao kwa kitambo kisha kutoweka (Yakobo 4:14), Mvuke sio kama moshi ambao unaweza walau ukauona ukipaa mawinguni, mvuke wenyewe hata kwenye dari haufiki umeshapotea, ndivyo maisha yetu yalivyo. Biblia inasema na mwanadamu ni kama maua ambayo hayo hayana maisha marefu,(Zaburi 103:15 ”Mwanadamu siku zake zi kama majani; Kama ua la kondeni ndivyo asitawivyo).

Hata kama tutaishi miaka 60 tu au miaka 120 bado siku zetu zitabakia kuwa ni chache sana. Hivyo swali tunalopaswa kujiuliza tukifa leo huko tunapokwenda ni kitu gani cha maana kitaoneka tumekifanya hapa duniani?. Kwasababu kule hatutaulizwa tulikuwa na majumba mangapi, au magari mangapi, au biashara ngapi, au watoto wangapi,wala hatutaulizwa tulikuwa maskini kiasi gani LA! Tutaulizwa ni kitu gani tumeongeza katika ufalme wa mbinguni…Tukiliweka hilo akilini basi itatusaidia sana kuishi kiungalifu.

Tunamwona Bwana wetu Yesu alijua nini maana ya kuukomboa wakati, angalia alichowaambia wanafunzi wake…Yohana 9:4 ”Imetupasa kuzifanya kazi zake yeye aliyenipeleka maadamu ni mchana, usiku waja asipoweza mtu kufanya kazi…”

Unaona Japo alikuwa ni Mungu katika mwili alijua nini maana ya muda, kuwa kuna kipindi kinachoitwa usiku (KIFO) ambacho mtu yoyote atatamani kufanya kazi ya Mungu asiweze, Na tunamwona Bwana wetu japo aliishi miaka 33 tu lakini kazi aliyoifanya ina matunda makubwa mpaka sasa tunayafaidi. Hiyo ni kwasababu aliukomboa muda wake vizuri hapa duniani ipasavyo. Wakati mwingine hakuwa na muda hata wa kula. Alipoletewa chakula.

NA SISI JE! TUNAWEZAJE KUUMBOA WAKATI WETU?

https://1.bp.blogspot.com/-nKvoug0mvRs/XPe_WtuSbhI/AAAAAAAACU0/Ruj_I_5c8rkO9x3j45HNh2H8mmz7Z764ACLcBGAs/s640/62000414_595291020965960_135173066165583872_n.jpg
Tujijengee utaratibu wa kila siku mpya inapoanza tumwombe Mungu atusaidie tufanya kitu ambacho kitakuwa na manufaa katika ufalme wa mbinguni na katika maisha yetu ya rohoni… tuzitazame siku zetu ikiwa inaweza kupita siku nzima, wiki, mwezi bila kuona kitu chochote cha maana tulichokifanya kwa ajili ya maisha yetu ya rohoni au kwa ajili ya ufalme wa Mungu, basi tujue hatuukomboi muda haijalishi tunatengeneza mabilioni pa pesa kiasi gani kwa siku. Ndugu huu ndio wakati wa kuanza kuitengeneza njia yako upya mbele za Mungu, kabla ya siku ile kufika.

Muda ambao unautumia kuchati kwenye magroup ya whatsapp, au kusoma habari zisizokuwa na maana mitandaoni, komboa wakati kwa kutumia muda huo kujifunza Neno la Mungu, au kusoma mahubiri au mafundisho ya Neno la Mungu. hayo ndio mapenzi ya Mungu kwako, au tumia muda huo kukaa katika utulivu kumsifu na kumwimbia Mungu wako…peke yako au pamoja na wakristo wengine…

Tukiwa makazini kwetu, tumwombe Mungu atusaidie sio wakati wote, tutakuwa buzy na shughuli, au kuongea na wafanyakazi wenzetu mambo ya kikazi, tutumie muda wetu wakati mwingine kuwashirikisha habari za Yesu, huku tukiwaelekeze katika vyanzo vizuri vya kupata habari za Mungu, kwa kufanya hivyo pia tutakuwa tumeukomboa wakati na siku yetu kuwa na maana mbele za Mungu.

Muda ambao tumekaa hatuna shughuli yoyote, tunaweza tumia muda huo kwenda kuomba, hata kama hatutakuwa na mahitaji wakati huo mbele za Mungu, lakini pia tumeagizwa kuwaombea wengine, hivyo tumia muda huo kuwaombea watu wengine, kuna ndugu zako, rafiki zako, jamaa zako, taifa lako, kanisa n.k…Kwa kufanya hivyo utakuwa umeukomboa wakati. Na pia maombi yanasaidia kuepukana na majaribu.

Kama biblia inavyosema Mungu utusaidie kuzihesabu siku zetu tupate mioyo ya hekima (Zab 90:12). Hivyo na sisi tupate leo hekima ya kujua kuwa muda unakwenda sana, na jukumu bado ni kubwa mbele yetu na mtihani ulio mbele yetu bado hatujauvuka. Basi tusiwe kama wajinga, tukaze mwenda, tuanze kutumia muda wetu sasa kwa vitendo kujifunza kwa bidii Neno la Mungu kuliko jana, tuombe, na tuifanye kazi yake pia kana kwamba hatua tena mwaka mbele. Maana usiku waja asioweza mtu kuitenda kazi.

Mungu akubariki sana.

https://wingulamashahidi.org