[ATTACH=full]14837[/ATTACH]
Namshukuru Allah kwa kunipa nguvu za kupambana na miungu midogo midogo. Miungu inayotaka kuiteka nchi nyara na kudhalilisha raia wake. Miungu iliyoifanya Kenya kuwa soko huru, soko la vihoja na ubakaji wa demokrasia, soko isiyo na sheria ila dhulma, mauaji, wizi wa mali ya umma pamoja na demokrasia ya kijambazi. Sina ugomvi na mtu bali nina machungu na mambo yanavyokwenda kombo. Nina machungu kwasababu utaifa nilionayo moyoni hauniruhusu kufyata domo wakati umma unateketea.
Je, wataka kuwa maarufu Kenya? Ni rahisi kabisa. Unga viongozi na serikali mkono. Wakishuta wasifu kwa kusema ni harufu ya marashi, walimbikizie sifa wakiiba, sifu kabila zao na wake zao, heshimu maamuzi ya mipango yao ya kando serikali, Utaogopewa na kila mtu kwani sheria ya wahuni itakukinga. Fungua hospitali kisha uwabake wanawake wanaotafuta matibabu, simama kwenye jukwaa na useme kabila Fulani likatwe kwa upanga likipinga mwito wa serikali iliyo madarakani, watusi kwa kuwaita maskini baada ya serikali hiyo hiyo unayoabudu kuwafilisi raia wake, kuwa mbunge na ubake ndani ya ofisi yako kwani sheria ni ya mama zenu si yetu sote tena, waite viongozi wadini kwa kiegezo cha kuombea taifa baada ya kufanya maasi kwa wananchi wako, cheza na jina la mungu kila kukicha kwani mungu wako ni senti, simama imara na serikali kisha vunja sheria. Hakika utalindwa ndani ya serikali.
Kenya hamna sheria. Nasema pasi na uwoga kwani hata Jaji Mkuu Willy Mutunga yuajua vyema ila hana budi wala sauti ya kusema hivyo. Mahakama ya Willy Mutunga kwa maoni ya wakenya wengi ilikataa kusikia vilio vyao na kutoa uamuzi wa dadika tatu. Ndio, dakika tatu! Sisemi majaji hao walikosea bali kutoa maamuzi ya taifa kwa dakika tatu ni sawia na kutwanga maji kwenye kinu. Hata kesi za mapenzi hazisuluhishwi kwa dakika tatu. Labda Willy Mutunga na wenzake hawana doa lolote; hawana ila, hawana waa japokuwa kuna wenye kukirihishwa na maamuzi yao. Daktari Willy Mutunga sasa kiza kinene kimetunga mithili ya ukungu. Mahakama yako haiheshimiwi tena, mahakama yako ni sawia na simba wa matopeni anayeteleza ovyo ovyo. Nasema hivyo kwa sababu wakenya waliheshimu maamuzi yenu lakini sasa waliotangazwa washindi
hawaheshimu maamuzi mliotoa kuhusu waalimu. Leo Ndugu yangu Willy Mutunga walialia kwenye vyombo vya habari eti baadhi ya majaji ni wafisadi. Usitudanganye! Mchezo wa daganya toto uliishia Westgate na wanajeshi wa KDF. Mahakama na sheria za humu nchini zinafikiria kuwa wakenya wengine sio watu, nyinyi ndio watu mkifanya kitu mnasema tuachie Mungu, wengine wakifanya ni dhambi. Kwani ni Mungu gani huyu mnayeabudu? Ni yule yule ninayemjua ama mna mungu wenu? Nikisema naambiwa sifai kusema kwa sababu mimi ni mwanahabari. Kwani mwanahabari hana hisia? Kwani mwanahabari halipi ushuru? Kwani mwanahabari sio binadamu? Acheni utoto! Nasema nanyi wambea. Mwanahabari ni macho na kioo cha jamii.
MOSES KURIA.
Sijasahau Moses Kuria. Sitaki kumwita mheshimiwa kwani vitendo vyake na matamshi yake si vya kiheshimiwa. Waliomchagua na wamwite mheshimiwa mimi simo. OH pole nimesahau, kwanza alichaguliwa na nani? Moses Kuria endelea kuwadharau wakenya kwa sababu ya ukabila na ubinafsi. Moses Kuria kumbuka nchii hii itakapoteketea kwa sababu ya matamshi kama yako hata shetani hatakuwa na wasaa wa kusikia umaarufu wako wa kuwatenganisha wakenya. Sisi sio wapumbavu lakini nakuhakikishia serikali sio MUNGU. Iko siku haki itashinda na hiyo ndio siku utakapojua tofauti ya kuvua chupi na kuvua samaki.
MUTAHI NGUNYI.
Mutahi Ngunyi sitaki kusema sana lakini ni kweli sisi ni maskini. Tumesalitiwa na serikali, tumeibiwa na kudhalilishwa na hiyo hiyo serikali unayoabudu lakini MUTAHI NGUNYI kumbuka aliyekupa wewe ndiye aliyeninyima mimi. Mutahi Ngunyi watutusi kisha wataka kunywa pombe nasi? Nakukumbusha ufanye adabu yako na ukumbuke kuwa dawa ya maskini si pombe bali chakula. Kama wataka kufanya ukuruba na sisi mwambie Rais wako apunguze bei ya vyakula na kwanza kabisa aanze na maziwa ili watoto wetu wafaidi. Mwambie twajua mwenye kampuni ni nani lakini twajifanya wajinga, mwambie aambie wafanyakazi wake waheshimu maamuzi ya mahakama, mwambie aambie maafisa wake waache kutumia nguvu za bunduki kuwaua vijana ovyo ovyo, mwambie aambie maafisa wake wawache kupora mali ya umma, mwambie awashike walanguzi wa dawa za kulevya sio kuwahangaisha mateja, mwambie dola imefika 107, mwambie uchumi umezorota, mwambie kina mama na dada zetu wanabakwa na watu wanaojiita wafuasi wake sugu, mwambie atupe sisi vijana makazi, mwambie tangu aingie madarakani hatukumbuki lolote alilofanya ila selfie, mwambie aheshimu vyombo vya habari na watetezi wa haki za binadamu, mwambie tuna njaa, mwambie tuna machungu, mwambie sheria hukata pande zote mbili, mwisho kabisa mwambie vijana wamegutuka na twaja kwa mpigo mwaka wa 2017. Mutahi Ngunyi ukifikisha salamu hizi basi sisi maskini hatutaki pombe yako, hatutaki kuleweshwa kisha mali yetu kuibiwa tukiwa ulevini, serikali imetulewesha kwa kipindi cha miaka mitatu na mvinyo mkali kushinda hata changaa, mvinyo wa kutuangamiza na kutufanya watumwa ndani ya nchi yetu. Sisi hatuna kinyongo nawe lakini tutakusamehe na umaskini wetu kwani sisi ni maskini lakini wakubwa kimapenzi moyoni.
ADAN DUALE.
Nadhani nilisema mengi juma lililopita lakini juzi bado nilikuona ukijipiga kifua na kutetea viranja wako na kusahau wana-garissa hawana vitambulisho, vijana wanatekwa nyara na watu wanaodaiwa kuwa maafisa wa polisi na kuuawa, hamna waalimu garissa na Mandera. Naarifiwa ulikuwa mwalimu lakini nashindwa kufahamu ulikuwa mwalimu wa kusema na kuenda ama kusema na kutenda. Mtihani unabisha jitayarishe kuwa na vizazi visivyo na elimu kwa sababu umefeli kuwashughulikia waliokuchagua na badala yake kupiga domo ukitetea serikali isiyoheshimu watu wako. Sitaki kuendelea kwani sijasahau tabia zenu ni kama bata hata mlishwe mawe bado mtahara.
KIPCHUMBA MURKOMEN
Ni hatari sana msomi kuwa na tabia za kitoto. Wasomi ni watu wanaoheshimika. Nawaheshimu wasomi wote wewe ukiwa mmoja wao. Lakini ni hatari sana msomi anayefahamu sheria kwenda kinyume na sheria. Murkomen nataka kukukumbusha kuwa siasa sio mchezo mchafu bali mtu binafsi ndiye mwenye siasa chafu. Kuwa kibaraka sio dhambi lakini kujidhalilisha na kubusu tako la viongozi ndio dhambi kuu. Tumewaona wanasiasa wengi, makalulu na wenye vihoja chungu nzima. Tumewaona kina Joseph Kamotho waliolala na jina la baba lakini siku hizi wanalala na upweke, Kihika kimani, Shariff Nassir na msemo wake wa mpende msipende KANU itatawala. KANU haitawali tena, KANU imezikwa katika kaburi la sahau ila ina watoto wanaojaribu kuinuka na kuturegesha huko. Wanaotawala sasa ni wakenya kwa nguvu za RABUKA. Leo mwaomba mkisema kabila moja inalengwa na mahakama ya ICC, leo mwaomba mkitaka tuwaombee, leo kila mtu anacheza na jina la Mungu. Je, mmesahau waliouawa katika ghasia za baada ya uchaguzi mwaka wa 2007? Ni nani aliyewaua wakenya ndani ya kanisa la kiambaa? Ni nani aliyewaua wakenya huko naivasha? Ulikuwa wapi wewe Murkomen? Mbona sikukuona ukiwaombea waliouawa na wakimbizi wa ndani kwa ndani? Wacha nikupashe basi. Sisi si mamoja, WE ARE NOT ONE AND WE WILL NEVER BE ONE. WE ARE TWO. THE RICH AND THE POOR. Mungu atatulipia sisi wanyonge, Mungu atasikia maombi yetu na ya wale waliouawa mwaka wa 2007, hatutaombea kabila hili wala lile, tutaombea makabila yote kwa maana sisi twaabudu Mungu aliye mkuu. Kipchumba Murkomen MUNGU NI MKUU.
Mohammed Ali ni Mhariri Mkuu wa Kitengo cha Upekuzi KTN.
Kuwasiliana naye: [email protected], FB: Official Jicho Pevu with Mohammed Ali, Twitter: @mohajichopevu