Ukimwangalia kwa makini Rais wetu mpendwa, John Joseph Pombe Magufuli, utaona kwamba ana uroho mkubwa sana wa fedha, tena ana ubinafsi. Hili nimeligundua baada ya kulitafakari sakata linaoendelea sasa hivi la KOROSHO. Wakati Serikali ikibanwa kwa kutorejesha fedha za wakulima wa Korosho, ambazo imezikusanya na inatakiwa zirejeshwe, Serikali IMEJIONGEZA kwa kufanya zaidi na zaidi, kwa kuleta pendekezo kwamba hizo fedha sasa kisheria zibaki Hazina, yaani serikalini. kwa hiyo mezani kuna madai mawili, albaki ya fedha za nyuma zinazodaiwa, na hili la pili la kuhalalisha kabisa ulaji huu wa serikali.
Kwanza utata ninaouona hapo ni kuhusu kile kilichokuwa kinadaiwa kwamba HAKUNA KAMA MAGUFULI, kwamba Wakulima wa Korosho huko mikoa ya kusini HUWAAMBII KITU KUHUSU MAGUFULI, kwa KUBORESHA BEI YA KOROSHO! Hoja hii mimi nilikuwa sikubaliani nayo, kwamba uboreshaji wa bei ya korosho ulisababishwa na mazingira mbalimbali ambayo yalianza kufanyiwa kazi kabla hata ya serikali ya awamu ya Tano chini ya JPM kuingia madarakani. Magufuli ameneemeka na sifa ya kupandisha bei ya Korosho, kama ambavyo amekuwa akineemeka na sifa zinazotokana na mipango ya serikali ya awamu ya nne chini ya Kikwete, pale anapofungua miradi kibao (Ukiacha ufunguzi wa Hospitali ya Mloganzila ambapo alikataa sifa alizorundikiwa na kukiri kwa mara ya kwanza kwamba sifa zote ziende kwa Kikwete). Sasa utata unakuja, hivi huyu ambaye alisimamia kuneemeka kwa wakulima wa korosho, ndiye huyuhuyu atasimamia kuanguka kwa zao hilo, na hivyo kuleta balaa kwa wakulima hao?
Jibu linakuja kwamba pamoja na ubinafsi wa kukusanya sifa ambazo siyo zake, Bado Magufuli amejiongeza zaidi na kuzimezea mate hela za wakulima wa korosho. Huo ndio uroho wa Magufuli. Kawaangalia hawa wakulima wanavyoneemeka weee, kisha katafuta njia ya kuzimega hizo hela. kagundua na kutekeleza. hapo ndio tunapata picha halisi ya saikolojia ya Magufuli ilivyo. ni mroho wa fedha ambaye akisikia tu kuna mtu au kikundi cha watu wana fedha, basi anazitaka, afanyie miradi yake anayoiamini yeye, hata kama haina faida ya kiuchumi ya moja kwa moja. mfano kuhamia Dodoma, kujenga uwanja wa ndege wa kimataifa kule Chato, miradi ya ununuzi wa ndege usio na mpangilio, nk.
Uroho wa Magufuli ulianzia kuhamisha fedha za serikali kutoka mabenki na kuzirundika benki kuu. wakati zikiwa huku kwenye mabenki, fedha hizo zilichochea biashara, uwekezaji na ukuaji wa uchumi. tatizo la Magu, anafikiria kwamba mabenki haya sijui yako nje ya nchi? haya, karundika fedha Benki kuu, huku mtaani fedha ikaanza kupotea.
Magufuli akipita mitaani anaona maduka makubwa anaona ehee, hii hela yote ije kwangu. kodi kila kona. sasa hivi kuendesha biashara wala faida hakuna tena.
Akageukia mashirika. ni kweli kulikuwa na mashirika ambayo yalipitiliza katika kulipana. lakini alichotakiwa siyo kufuta kila kitu, bali kurekebisha kidogo ili kuweka uwiano sawa. lakini yeye magufuli anataka vyote, tena kwa pupa. na tunajua mtaka yote kwa pupa hukosa yote.
Magufuli akiangalia payroll ya mishahara anaona laa!!! fedha yote hii? akaanza na kufuta wafanyakazi hewa, ambao sijui kwa nini imeshindikana kuwamaliza wote, kama ambavyo ripoti ya CAG inaendelea kuonesha. lakini akahamia kwenye “vyeti feki”, lengo likiwa kupunguza ukubwa wa payroll. akasimamisha ajira. akasimisha na kufuta promosheni ambazo tayari zimetoka. Akaingilia wale wa “darasa la saba”, futa mikataba ya maprofesa ambao wamestaafu, bila kujali kwamba hawa watu bado wana mchango mkubwa sana kwa taifa, baada ya kuwa wameandaliwa kwa muda mrefu. si kwamba haya yote anayofanya ni haramu. mengine ni sawa tu, lakini tatizo ni namna yanavyoendeshwa. Magufuli anaongozwa na uroho, wivu wa kwa nini hawa wawe na fedha hizi. roho ya korosho. na ndio maana kuna wakati alitamka kwamba MATAJIRI WATAISHI KAMA MASHETANI. hata anapopunguza mishahara mikubwa, lengo siyo kuleta uwiano, ni kutii kiu yake ya uroho na ubinafsi.
Ni roho hii ya uroho na ubinafsi ndio inamfanya awaonee wivu watu wa kaskazini, ambao kihistoria walipokea mifumo ya elimu kutoka kwa wamisionari. Nyerere wala hakupambana nao kijinga, kama alivyoeleza mbunge Silinde. aliwafanya wachaga wajione ni watanzania. Magufuli anawaonesha chuki ya moja kwa moja. akiwatia umaskini ndio atapata usingizi mwanana. Angalia alivyoshughulika na Manji, anavyoshughulika na wale jamaa wa IPTL, Rugemalira na Singh. hayo mambo ni ya kufuata sheria tu, na siyo kuumiza watu pasipo sababu. na pia mbona viongozi ndio walikuwa wanawatumia hao? viongozi je?
Kwa mwendo huu, hakuna mtu atakaa awe tajiri Tanzania. hata taasisi ikionekana imepiga hatua, atachukua fedha yote. wakulima wakionesha mafanikio anapiga panga. Wafanyabiashara wakifanikiwa anapiga panga. Wafanyakazi nao ndio hivyo panga liko shingoni mwao tayari. sasa kageukia na wavuvi, kawatia ufukara usiseme. Magufuli hana tofauti na fisi ambaye akiona mguu wake mwenyewe unanenepa, anautafuna!