ASKOFU RUAICHI AWAJIBU VIBARAKA WA FISIEMU KUHUSU UCHAGA NA UKATOLIKI.
JUU YA MWAMBA HUU NITALIJENGA KANISA LANGU, WALA MILANGO YA KUZIMU HAITALISHINDA" [Mathayo 16:18]
Siku za hivi karibuni, wameibuka watu wenye kujidai kuwa ni Wakatoliki wenye nia njema, wakijitahidi kutumia ujuzi wao kulikosoa Kanisa Katoliki hasa Baraza la Maaskofu, kwa kudai eti limetawaliwa na ukabila(uchaga) jambo linalopelekea kuwa baraza la kisiasa kwa kujihusisha na Chama cha Demokrasia na Maendeleo{CHADEMA} ambacho nacho limekuwa kikishutumiwa kwa muda kuhusu swala la ukabila.
Mimi nami, nimeona nisiwe kimya tu, maana nami kwa Ukatoliki wangu, kwa njia ya Ubatizo na Kipaimara nimeshirikishwa ofisi tatu za Kristo, yaani Ukuhani, Unabii na Ufalme.
- Chanzo cha tatizo.
Kila kitu kina chanzo chake. Chanzo cha haya ni pale Maaskofu wetu walipotoa ujumbe wa Kwaresima 2018, ambao ndani yake katika ukurasa wa 12 na 13, Maaskofu walitushirikisha kuhusu hali ya siasa hapa nchini, ambapo katika nchi yetu uhuru wa vyama vya siasa ambao ni jambo la haki kisheria umebanwa vya kutosha. Vyama vya siasa sio kikundi vya kigaidi ni vyama vinavyotambuliwa na Katiba ya nchi yetu. Sasa hali ya vyama kujitangaza imebanwa sana. Maaskofu wakatahadharisha kuwa kama hatua hazitachukuliwa, kutakuwa na ongezeko la matabaka kati ya watanzania na wengine watabeba chuki na visasi dhidi ya wenzao.
Baada ya ujumbe huo kutolewa, ambao serikali walipaswa kurudi kwenye katiba na kugundua hicho kilichosemwa ni kweli au si kweli?
Matokeo yake, anaanza kutafutwa “mchawi” na matokeo yake, “ramli” za kisasa yaani kubashiri-bashiri tu kuwa mbaya ni Huyu au yule kukaanza!
Sasa kilichofanyika ni kufananisha tu, CHADEMA na wachaga, pamoja Baraza la Maaskofu na Wachaga, hapo ikipatikana mantiki kwamba upo uhusiano wa karibu, na hiyo ikawa ndio hukumu kuu kwa Kanisa Katoliki ambayo inatolewa na watu wanaojidai eti Wakatoliki.
- Maaskofu na ukabila.
Naomba niandike kuwa, Kanisa Katoliki sio la kikabila na Baraza la Maaskofu, sio la kikabila, ni baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, ni Baraza la Maaskofu wanaoongoza majimbo Katoliki sio makabila.
Kwa hiyo uaskofu haupatikani kwa vigezo vya ukabila bali kwa:
A) Kwa mwangaza wa Roho Mtakatifu
B) Kwa sifa za mtu mwenyewe kadiri ya sheria za Kanisa.
Askofu hapatikani kwa sababu ya kabila lake, Bali kwa sababu ya wito, mang’amuzi sahihi na hali ya mtu.
Kadiri ya sheria za Kanisa Katoliki ( Codex Iuris Canonici) namba 375-380,
Ufafanuzi makini wa Kanisa unatolewa juu ya namna Askofu anavyopatikana na sifa zake. Kwa kifupi,
-Baba Mtakatifu ndio anamteua Askofu
- Wanaohusika katika mchakato ni Askofu mtangulizi, ambaye huwasilisha majina ya mapadri watakaomrithi, baraza la Maaskofu wanapitisha majina ya mapadri hao waliopendekezwa, lazima wakubaliane, balozi wa Papa naye atatafuta uthibitisho kwa rais wa baraza
la Maaskofu, wanajopo la ushauri wa Jimbo, wakuu wa Kanisa la Cathedral na makleri wengine, kisha anatuma pendekezo lake kwa Kiti cha kitume.
Hizo ni hatua chache tu za kumpata Askofu, kumbe kwa mchakato huu swala la ukabila haliwezi kupata nafasi, maana Rais wa Baraza sio mchaga, Balozi wa Papa sio mchaga, na Maaskofu waliostaafu hivi karibuni sio wachaga!
Kumbe, kushutumu Kanisa Katoliki kwa msingi au kwa hoja ya ukabila ni kutaka kuwafanya Wakatoliki wachanganyikiwe, wachukie imani yao kwa sababu ya mtazamo potofu na wa hiyana.
Wakatoliki tudumu katika imani yetu. Sipeperushwe na upepo huu ambao msingi wake ni kujitetea tu, baada ya kuguswa na ujumbe wa Kwaresima.
Tangu mwaka 2010, Kanisa Katoliki, limepata Maaskofu wapya hapa Tanzania wapatao 14, na kati yao watatu ndio wachaga, na wengine 11 ni makabila mengine. ninaorodhesha Maaskofu hao nitaanza na hao wachaga,
Mhashamu Rogath Kimaryo, Askofu wa Same.
Mhashamu Joseph Mlola, Askofu wa Kigoma.
Mhashamu Prosper Lyimo, Askofu msaidizi wa Arusha.
Wasio kuwa wachaga, ambao wao ni wengi zaidi ni
Mhashamu Salutaris Libena, Askofu wa Ifakara
Mhashamu Eusebius Nzigilwa, Askofu msaidizi wa Dar es salaam.
Mhashamu Renatus Nkwande, Askofu wa Bunda.
Mhashamu Gervas Nyaisonga, Askofu wa Mpanda.
Mhashamu Bernard Mfumbusa, Askofu wa Kondoa.
Mhashamu John Ndimbo, Askofu wa Mbinga.
Mhashamu Titus Mdoe, Askofu wa Mtwara.
Mhashamu Liberatus Sangu, Askofu wa Shinyanga.
Mhashamu Edward Mapunda, Askofu wa Singida.
Mhashamu Flavian Kasala, Askofu wa Geita, na
Mhashamu Novatus Rugambwa, balozi wa Baba Mtakatifu nchini Honduras.
Bila shaka tumeona kuwa Maaskofu waliopatikana kati ya mwaka 2010 hadi sasa ndio hao. Na kuhusu wachaga wapo watatu tu.
Sipigii upatu juu ya ukabila, nataka tuone tu waandishi wanavyopotosha kwa kusema, wanaoteuliwa kuwa Maaskofu ni wachaga tu. Hapana.
- Kanisa miaka 455, na mapapa wa kiitaliano.
Niwakumbushe tena, kadiri ya historia ya Kanisa Papa Adriano wa VI, aliliongoza Kanisa mwaka 1522 hadi 1523, Papa Huyu alikuwa mdachi, kutoka Uholanzi.
Baada yake alifuata Papa Clement wa VII, ambaye alikuwa mwitaliano, kwa muda wa kuanzia mwaka 1523 hadi mwaka 1978, Mapapa walioliongoza Kanisa Katoliki kwa nyakati tofauti walikuwa ni 45 na wote walikuwa waitaliano, hadi mwaka 1978, tulipompata Papa Yohane Paulo wa II, ambaye ni Mpoland.
Sasa kama watu wanahama Kanisa Katoliki kwa sababu ya wingi wa maaskofu wachaga, tuseme kuwa tatizo lao ni uelewa juu ya imani, au wanakerwa na wachaga au nini?
Kama Kanisa liliongozwa na waitaliano kwa miaka 455, hapa kwetu Tanzania, Rais wa baraza la Maaskofu Mhashamu Tarsusius Ngalalekumtwa sio mchaga, wala Katibu wa baraza la Maaskofu, Padri Raymond Saba naye sio mchaga!!!
Tatizo ni nini?
Tatizo ni ukweli, Kanisa Katoliki linahukumiwa kwa sababu ya ukweli. Ukweli wa “kiyohane mbatizaji” unafanya “uherode” uibuke.
Wakatoliki tutambue kwamba, Kanisa Katoliki sio mali ya chama chochote, ndio maana ndani yake wamo wana CCM, wana CHADEMA, wasio na vyama nk.
Pia linatoa huduma za afya, elimu, nk kwa watu wa dini zote bila kubagua na kuajiri vile vile.
Kwa sababu hiyo, ndugu zangu, tusiyumbishwe na maneno ya kizushi ya watu wajiitao Wakatoliki.
Maaskofu wamesema neno?
Maaskofu wako kimya, hawajasema lolote. Sasa wamepata wasemaji wao humu mitandaoni, ambao wanajua Askofu gani kajalia kaa la moto na mwingine vile!!!
Nahitimisha.
Ndugu, Kanisa Katoliki ndilo Kanisa la Kristo mwenyewe, halitaanguka kwa fitina za kitoto hivi. Wakatoliki tuzidi kusali ili Mungu aendelee kuwa upande wetu, tuwaombee na hao wanaojiita Wakatoliki huku wamevaa “mabomu” na kujiripua kwa madai ya nia njema.
Tuiombee pia nchi yetu Tanzania, tuwe na amani ya kweli ambayo chimbuko lake ni haki inayopatikana kwa kwa misingi ya kisheria.
Mungu awabariki sana.