Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) imeanzisha safari mpya za kwenda Victoria Falls, Zimbabwe na Cape Town, Afrika Kusini zinazotarajia kuanza Desemba 11, 2025 kwa punguzo maalum za nauli ambali ni Dola 499, kwa tiket ya kwenda na kurudi ikiwa ni zawadi mahsusi kwa wateja wake katika msimu huu wa sikukuu.
Safari hizi zitafanyika mara mbili kwa wiki, kila Alhamisi na Ijumaa, zikianzia Dar es Salaam – Victoria Falls – Cape Town, huku lengo kuu la safari hizo ikiwa ni kuhudumia wateja wake ambao ni wasafiri, watalii na wafanyabiashara.
Aidha, kuanzishwa kwa safari hizi ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa kibiashara wa ATCL unaolenga kutoa huduma za usafiri wa anga zinazozingatia vipaumbele vya wateja wake kwa kuwaongezea machaguo ya safari na kurahisisha upatikanaji wa huduma.
Kwa sasa maandalizi yote yamekamilika, na Kampuni inatarajia kuzindua safari hizi kwa kushirikisha wadau wake wakiwemo wanachama wa Twiga Miles, mawakala wa usafiri na utalii na wafanyabiashara.
ATCL inaendelea kupanua mtandao wake wa ndani na nje ya bara la Afrika kwa kuunganisha Dar es Salaam na miji ya kimkakati ikiwemo Dubai, Guangzhou, Mumbai, Lagos, Johannesburg, Nairobi, Kinshasa, Zanzibar, Harare, Lusaka, Ndola, Lubumbashi na Entebbe, huku ikiifanya Dar es Salaam kuwa kitovu cha safari za anga katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
