JUMUIYA NA TAASISI ZA KIISLAMUTANZANIA
WARAKA WA EID EL FITR 1439H | 2018
Bismillahir Rahmanir Rahiim
A: UTANGULIZI
Awali ya yote tunamshukuru Mwenyezi Mungu na tunamtakia Rehma na Amani Mtume wake Muhammad (SAW). Waraka huu ni kilele cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Tunamuomba Allah atukubalie saumu yetu. Kuhusu mwezi huo wa Ramadhani Allah anatueleza: “Enyi mlioamini! Mmeandikiwa saumu, kama waliyo andikiwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Mungu”. (2:183). Miongoni mwa umuhimu wa mwezi huu ni tukio la kushushwa Qur’an Tukufu ndani yake kama Mwongozo kwa watu na kipambanuzi cha Haki na Batili. Ni lengo la waraka huu, pamoja na mambo mengine, kuweka msisitizo juu ya upambanuzi wa haki na batili, kama ilivyosisitizwa na Qur’an Tukufu.
Watukufu Waislamu jana Eid mosi na leo Eid pili tunaadhimisha sikukuu hii adhimu. Sisi viongozi wa Waislamu nchini, tunao wajibu wa kuitumia nafasi hii kutoa nasaha kwenu na jamii nzima ya Watanzania kuhusu mambo mema (mambo ya haki), na kuwanasishi kuacha mambo mabaya (mambo ya batili). Miongoni mwa hayo ni Uhuru,
Haki, Udugu na Amani. Mambo haya ni muhimu katika dini yetu na ni msingi wa ujenzi wa taifa letu kama ilivyotakiwa katika utangulizi wa katiba ya nchi yetu ya mwaka 1977.
Sisi viongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu tumeona nchi yetu imeyumba katika hayo. Na kwa sababu hiyo imekuwa kawaida sasa kwa Tanzania kushuhudiwa mauaji ya watu na maiti kutupwa hovyo, utekwaji wa watu, ukamatwaji wa raia wasio na hatia, na baadhi yao wakipotezwa kabisa.
Tunashuhudia watuhumiwa wote wa ugaidi wanakuwa ni Masheikh, Walimu wa Madrasa na Waumini wao. Jambo baya zaidi, ni kesi zao, ambazo karibu zote ni za kubambikiwa na kusingiziwa, hazisikilizwi kabisa – na hivyo wamenyimwa hata nafasi ya kupata haki mahakamani. Imekuwa jambo la kawaida Waislamu kuteswa na kuuwawa bila ya hatia. Serikali inafanya hivyo mitaani na huenda mbali zaidi kwa kuuwa katika nyumba tukufu za Mwenyezi Mungu, Misikiti. Watoto wa madrasa na walimu wao wamekuwa wakivamiwa na vyombo vya ulinzi kama wahalifu, kukamatwa na kuteswa kwa kisingizio cha ugaidi au kutokusajiliwa kwa Madrasa wanazosoma. Imekuwa kawaida kwa viongozi wa taifa letu kutoa amri na matamko yanayokiuka misingi ya haki, utu, sheria na demokrasia.
Zaidi Waislamu ni sehemu ya jamii ya Watanzania, mambo yote ya nchi yetu nasi ni sehemu yake, tunaguswa na changamoto za nchi yetu hatuwezi kujiweka pembeni bila ya kushiriki kuzishughulikia. Katika kutimiza wajibu huo, siku zote tunamuomba Mwenyezi Mungu atupe hekima na busara, ili atupe maarifa ya kuzitafutia majawabu
changamoto hizo, hasa wakati wa kuunasihi umma na kuwashauri viongozi wa Taifa letu kama tunavyofanya kupitia waraka huu.
Kwa muktadaha huo, Ramadhani 29, sawa na Juni 14, 2018, viongozi wa kiislamu nchini kupitia jukwaa lao kongwe la JUMUIYA NA TAASISI ZA KIISLAMU TANZANIA, tulikutana Jijini Dar es Salaam kujadili na kutafakari kuhusu masuala mbalimbali ya kidini na ya kijamii. Ujumbe huu wa Eid ni matokeo ya kikao hicho muhimu.
B. HAKI NA AMANI
Jamii ya Watanzania imejengwa na wafuasi wa itikadi, imani na mila tofauti. Hata hivyo sote tutabaki kuwa ni watu wa jamii moja ambayo yapo mambo yanayotuunganisha. Kati ya mambo hayo muhimu ni suala la amani na utulivu. Uislamu ni dini ya amani hivyo viongozi wa Waislamu tunao wajibu wa kuimarisha amani kwa jamii yetu, ili kudumisha umoja wetu wa kijamii. Lakini pia tunao wajibu wa kuonya
pale tunapoona kuna dhulma, na hakuna haki, na hivyo kuwepo kwa dalili au viashiria vya kutoweka kwa amani. Sisi viongozi wa Waislamu, tunatambua kuwa uongozi bora, wenye kuheshimu haki na utu wa watu ni msingi madhubuti wa kuongoza maisha ya watu kwa ujumla. Lakini kwa bahati mbaya, hivi sasa tunashuhudia matukio yaliyo
kinyume na misingi iliyolilea taifa letu. Baadhi ya matukio hayo ni yafuatayo:
- Haki ya uhai:
Kwa siku za karibuni nchi yetu imekumbwa na matukio mbalimbali
mabaya yanayotoa viashiria vya haki ya uhai na kuishi kuanza kutoweka nchini. Matukio hayo mabaya na yasiyo ya kitanzania yamehusisha utekaji na uteswaji wa raia, kuokotwa kwa miili ya watu waliouawa ikiwa kwenye viroba kwenye fukwe mbalimbali za mito, maziwa na bahari nchini, kupotea kwa watu mbalimbali huku pakiwa na viashiria vya ushiriki wa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama katika kupotea kwao, mashambulizi ya silaha dhidi ya viongozi wa kiislamu na viongozi wa kisiasa, hasa wa vyama vya upinzani nchini, mauaji yenye mwelekeo wa kiitikadi aidha za kidini au kisiasa, vitisho kwa wote wanaoonekana kuwa na maoni mbadala juu ya uendeshaji wa nchi yetu, ubambikiziaji wa kesi hasa zinazohusu masuala ya ugaidi na
uraia kwa wote wanaoonekana kupingana na serikali, na zaidi matumizi mabaya, na ya nguvu kupita kiasi, ya vyombo vya dola dhidi ya raia.
Ushauri:
Viongozi wa Jumuiya na Taasisi za Waislamu Tanzania, tunaishauri Serikali ichukue hatua madhubuti kurudisha imani ya wananchi juu ya uwezo Serikali wa kulinda haki zao ya uhai na kuishi. Kwa kuwa vyombo vya Dola vilivyopaswa kulinda raia na kufanya uchunguzi juu ya uhalifu navyo ni sehemu ya wanaotuhumiwa na
kulalamikiwa kusababisha kutoweka kwa haki ya uhai na kuishi, ni wakati muafaka sasa wa kuwa na TUME YA KIJAJI ya kuchunguza masuala yote yanayohusu kutekwa, kupotezwa na kuuawa kwa watu, ili ukweli ujulikane na wanaohusika na masuala hayo wachukuliwe hatua. Pia tunashauri Jumuiya ya Kimataifa, Bunge na Taasisi za Kiraia za kutetea haki za binaadamu kuibana serikali kuhusu kuundwa tume hiyo muhimu kwa taifa. Pia tunatoa unatoa rai kwa waislam wote na kila mtanzania kuchukua ahadi, yeye na kizazi chake, kuendelea kuilinda haki hii ya Uhai na Kuishi, yake binafsi, ya jamii nzima, bila kujali imani ya dini au mrengo wa siasa.
- Haki ya kuabudu:
Sehemu ya jamii nchini, hasa sisi jamii ya waislamu, imeathirika
zaidi na kuminywa kwa haki ya kuabudu nchini, hasa kwa waumini na viongozi wetu kutekwa, kuuawa, kupotezwa, kufungwa, kufunguliwa mashtaka na kudhalilishwa wakiwa katika mikono ya vyombo vya ulinzi na usalama nchini. Mateso yote hayo huikuta jamii ya Waislamu kwa kisingizio cha mambo ya ugaidi. Yapo matukio kadhaa ya kuonyesha madhila tunayofanyiwa, tukio kubwa zaidi ni la Julai 21, 2017, la kushambuliwa kwa risasi, kuuwawa, kujeruhiwa, kuteswa na kisha kutekwa na kupotezwa kwa waumini 10 wa wakiwa kwenye ibada katika Msikiti wa Ali Mchumo, Kilwa, Mkoani Lindi.
Ushauri:
Viongozi wa Jumuiya na Taasisi za Waislamu Tanzania, tunaitaka Serikali iache kutumia kisingizio cha Ugaidi kuminya haki ya kuabudu kwa baadhi raia wake, jambo hili likiendelezwa litachochea uhasama wa kidini nchini na kujenga chuki kati ya jamii inayoondolewa uhuru wake wa kuabudu dhidi ya Serikali. Pia ni muhimu serikali ifanye uchunguzi wa kina juu ya kadhia ya Msikiti wa Ali Mchumo, mpaka leo
waumini wenzetu haijulikani hatma yao, hili ni jambo tete kwetu waislamu, na ni jambo linalojenga chuki na hasira za waislamu dhidi ya Serikali yao. Zaidi Serikali iiandike upya sheria ya Ugaidi, au iifanyie marekebisho makubwa kuondoa vipengele vyote vinavyosababisha haki za raia (hasa za kuabudu) kuvunjwa. Sheria hii ya Ugaidi
ilipokuwa inajadiliwa Bungeni mwaka 2002, Mbunge wa Lindi, Mohamed Abdulaziz alisema yafuatayo: “Sheria hiyo ikipitishwa thamani ya maisha ya mwanadamu haitakuwepo”. Maneno haya yametimia sasa, na kwa bahati mbaya jamii inayoathiriwa zaidi na sheria hiyo ni jamii ya waislamu. Mwisho tunashauri Mahakama,
Jaji Mkuu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Waziri wa Sheria na Mkurugrnzi Mkuu wa Mashtaka (DPP) kuhakikisha kuwa kesi zote za watuhumiwa wa ugaidi zinasikilizwa kwa haraka na watu hao kuapata haki yao, kwani “Haki inayocheleweshwa ni haki inayonyimwa”.
- HAKI NA UHURU WA HABARI NA KUJIELEZA:
Taifa letu sasa linaelekea katika kutoweka kwa haki na uhuru wa kujieleza, kukusanyika, na kupata habari. Kanuni za maudhui mbalimbali zinazoongoza na kusimamia uendeshaji wa sekta ya habari nchini zinatumika zaidi kuua kabisa uhuru wa kupata habari na kujieleza kwa wananchi.
Sisi Viongozi wa Jumuiya na Taasisi za Waislamu Tanzania, pamoja na waumini tunaowaongoza, kama sehemu ya jamii ya Watanzania inayopunguziwa uhuru wa kujieleza na kupata habari, nasi ni waathirika wa hali hiyo.
Ushauri:
Viongozi wa Jumuiya na Taasisi za Waislamu Tanzania, tunaishauri Serikali iwe na uvumilivu wa kusikia hata maoni isiyoyapenda. Jamii inayo haki na uhuru wa kutoa maoni juu ya namna serikali yao inavyofanya kazi zake, maoni hayo yanaweza kutumiwa na serikali ili kuboresha utoaji huduma wake. Lakini pia jamii inao uhuru wa kusoma, kuangalia na kusikiliza naoni hayo ya ukosoaji kupitia vyombo mbalimbali vya habari nchini. Kupunguza uhuru wa watu kujieleza na kupata habari si njia nzuri ya kuongoza Taifa letu.
- UHURU WA BUNGE NA MAHAKAMA:
Tumeshuhudia kubanwa na kupungua kabisa kwa Uhuru wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwanza kwa kufutwa kwa haki
ya wananchi kuona matangazo ya moja kwa moja ya wawakilishi wao wakiwa bungeni kama ambavyo ilizoeleka, kisha kwa matendo kadhaa ya Bunge na Serikali yanayopunguza hadhi na uzito wa mhimili wa Bunge kwa nchi. Kwa kiasi fulani Uhuru wa Mahakama nao umepungua mno, utendaji kazi wake na uwezo wake wa kujiendesha kifedha umewekwa mtegoni na Serikali, kwa kuwekewa masharti ya
kumalizwa, kupelekwa kwa haraka au kutolewa kwanza hukumu za madai ya kikodi katika kesi zinazoihusisha Serikali.
Ushauri:
Viongozi wa Jumuiya na Taasisi za Waislamu Tanzania, tunaishauri Serikali ifuate Katiba na Sheria za Nchi, na iache Bunge na Mahakama vijiendeshe na kufanya kazi zake kwa uhuru na kwa mujibu wa sheria na katiba. Serikali haipaswi kutoa vitisho na maelekezo kwa mihimili hiyo ya nchi yetu. Na pia ni muhimu fedha zinazopitishwa na Bunge kwaajili ya uendeshaji wa shughuli za Mahakama zitolewe kama zilivyopangwa, na zitolewe kwa wakati, bila masharti. Mwisho tunashauri wananchi warudishiwe haki ya kuona moja kwa moja wawakilishi wao wakiwa bungeni kama ilivyokuwa awali.
- UHURU WA KUCHAGUA:
Tumeshuhudia kukosekana kwa mazingira ya haki na huru ya kuchagua na kuchaguliwa katika chaguzi mbalimbali nchini mwetu. Hali hiyo imetokana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, NEC kutokuwa huru, na pia kuendesha na kusimamia chaguzi mbalimbali kwa misingi isiyo ya Haki na Usawa.
Ushahidi ni chaguzi kadhaa za karibuni ambazo NEC kwa Dhahiri walishindwa kuziendesha, na hivyo kusababisha vyama kadhaa kugomea chaguzi hizo pamoja na kutokea kwa vurugu. Sababu kuu ya yote hayo ni NEC kuwatumia wanachama wa chama tawala, walio Wakurugenzi wa Halmashauri, kama wasimamizi wakuu wa chaguzi hizo, kushindwa kuwaondoa hata pale malalamiko ya upendeleo dhidi yao yalipoibuliwa nk. Mambo hayo yote yameondoa dhana ya Uchaguzi wa Haki, Uwazi na Usawa, badala yake ni chaguzi zetu kugubikwa na ubabe, hila, vitisho, vurugu, matumizi makubwa ya nguvu ya dola, watu kujeruhiwa, na hata vifo.
Ushauri:
Viongozi wa Jumuiya na Taasisi za Waislamu Tanaznia, tunaishauri Serikali, NEC, Vyama vya Upinzani pamoja na wadau wote, kukaa pamoja kujadili changamoto za mazingira ya sasa ya chaguzi zetu, ili kupata namna bora ya kuwa na chaguzi huru, za haki na zenye usawa. Pia ni muhimu yafanyike mabadiliko makubwa ya Sheria zetu za Uchaguzi, yenye lengo la kuongeza uhuru, uwazi na ufanisi wa NEC. Mabadiliko hayo ya sheria za uchaguzi yahakikishe kuwa muundo wa NEC, upatikanaji wa Viongozi na Watendaji wake, pamoja na uwezo wake wa kuwa na watumishi wake wa kudumu katika ngazi ya Halmashauri vinapatiwa ufumbuzi utakaotoa nafasi ya kuwa na Tume
Mpya Huru ya Uchaguzi.
- UTII WA KATIBA NA SHERIA:
Tumeshuhudia pia kukosekana kwa utashi wa kutii sheria mbalimbali pamoja na katiba ya nchini yetu, hasa kwa Serikali na viongozi wake. Mifano mikuu ni Serikali kutokuheshimu Mamlaka za Serikali za Mitaa (LGA’s), kuziingilia, kupunguza uwezo wake wa kujitegemea kimapato, Serikali kufanya matumizi ya fedha za umma kinyume na sheria na nje ya utaratibu wa kibajeti, Serikali kutokufuata sheria na taratibu ilizojiwekea ikiwa ni pamoja au kutosukumwa na udini, itikadi au ukabila katika uteuzi wa viongozi mbalimbali wa Serikali, na
Serikali kutokufuata sheria katika ukamataji na ushikiliaji wa watu mbalimbali unaofanywa na vyombo vya usalama.
Ushauri:
Viongozi wa Jumuiya na Taasisi za Waislamu Tanzania, tunaishauri Serikali iwe mfano katika utii wa sheria na katiba ya nchi yetu, ili wananchi nao waige mfano huo. Pia ni vyema Serikali iziache Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini zifanye kazi zake kwa mujibu wa sheria, iache uingiliaji wake ulio kinyume na sheria na unaoleta
migogoro, pamoja na kuacha kuziondolea uwezo wa kimapato mamlaka hizo kunakorudisha nyuma utekelezaji wa shughuli zake za maendeleo.
- UHURU WA KISIASA:
Tumeshuhudia kutoweka kabisa kwa Uhuru wa mfumo wa Siasa
za vyama vingi nchini, tangu tuurudishe mwaka 1992. Serikali, kinyume na sheria zetu, inazuia kabisa mikutano ya hadhara na maandamano ya vyama vya siasa vya Upinzani nchini, huku viongozi wa Serikali ambao pia ni viongozi wa chama tawala wakiwa na uhuru wa kufanya mikutano hiyo. Zaidi tumeshuhudia viongozi wa kitaifa wa vya vyama vya Upinzani nchini wakizuiwa kufanya ziara za kutembelea wafuasi
wao na hata kutembelea maeneo waliyopewa ridhaa ya kuyaongoza nchini, kinyume na viongozi na wa Chama Tawala walio na fursa ya kufanya yote hayo bila kubughudhiwa. Jambo baya zaidi, tumeshuhudia, kwa mara ya kwanza nchini kwetu, Mbunge wa Upinzani akipigwa risasi akiwa kwenye eneo la Bunge, na mpaka sasa
kukiwa hakuna uchunguzi wowote wa tukio hilo uliofanyika, wala kutiwa mbaroni kwa waliohusika.
Ushauri:
Viongozi wa Jumuiya na Taasisi za Waislamu Tanaznia, tunaishauri Serikali kwanza iondoe zuio la mikutano ya hadhara na maandamano ya Vyama vya Upinzani, ambalo ni kinyume cha Sheria na Katiba ya nchi yetu. Pili Serikali, Vyama vya Siasa nchni (Tawala na Upinzani) wafanye “KIKAO CHA MASHAURIANO CHA KITAIFA”, ambacho sisi Viongozi wa dini tutakisimamia ili kujadili kwa kina changamoto za
kisiasa nchini, na kuleta suluhu kati ya Serikali, Chama Tawala na Vyama vya Upinzani nchini, na kuendeleza uhuru wetu wa kisiasa na kidemokrasia wa tangu mwaka 1992.
- HAKI ZA KIMAHAKAMA:
Tumeshuhudia Viongozi mbalimbali wa Kiislam katika maeneo mbalimbali nchini wakicheleweshewa au kukoseshwa kabisa haki za
kusikilizwa na kuhukumiwa na Mahakama zetu nchini. Mfano hai ni Masheikh wa Uamsho, Masheikh wa Arusha, pamoja na mamia ya waumini wengine waliofurika katika magereza ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na magereza mengine huku kesi zao zikiwa hazisikilizwi kwa miaka kadhaa sasa. Mbaya zaidi mahakama zikikataa hata kusikiliza malalamiko yao juu ya udhalilishwaji na mateso mbalimbali wanayokumbana nayo mikononi mwa vyombo vya usalama na magerezani.
Ushauri:
Viongozi wa Jumuiya na Taasisi za Waislamu Tanzania, tunaishauri Serikali (DPP) pamoja Mahakama watimize wajibu wake wa kutoa haki kwa watu, matendo haya dhidi ya Viongozi wa Waislam nchini yakiachwa yaendelee, jamii nzima ya Waislam itakosa Imani na Mahakama zetu, jambo ambalo si zuri kwa ustawi wa haki
nchini.
C. JAMII NA UCHUMI
Tumeshuhudia jitihada, ari na nia njema ya Serikali katika ukusanyaji Kodi nchini, usimamizi wa matumizi ya fedha za umma, kupinga rushwa pamoja kusimamia uvunaji na umilikaji wa raslimali za nchi kwa manufaa ya Taifa zima. Aidha, tunapongeza jitihada za ukusanyaji wa mapato na kodi ili kuiwezesha serikali kugharamia huduma za kijamii nchini. Hata hivyo, bila kukatisha tamaa jitihada hizo, tunapenda kusema yafuatayo:
- Kodi:
Yapo malalamiko kutoka kwa walipa kodi nchini, hasa sekta binafsi, juu ya namna ukusanyaji kodi huo unavyofanyika. Maeneo makubwa ya malalamiko hayo yakiwa ni mazingira yasiyo rafiki ya kikodi, ukadiriaji wa kodi kubwa kuliko uwezo wa kibiashara wa walipa kodi, ubabe wa watoza kodi, pamoja na ukomoaji wao kwa wafanyabiashara.
Mamlaka za utozaji kodi nchini nazo zinayo malalamiko mbalimbali
juu ya wafanyabiashara wasio waaminifu na wanaokwepa kulipa kodi, na hivyo kurudisha nyuma juhudi za Serikali za kuboresha huduma za jamii na kuleta maendeleo kupitia mapato hayo ya kodi.
Ushauri:
Viongozi wa Jumuiya na Taasisi za Waislamu Tanzania tunaamini kuwa Wafanyabiashara na Sekta Binafsi kwa ujumla si adui wa Serikali, shughuli za kiuchumi zinazoendeshwa nao zinapaswa kuboreshwa zaidi ili kupanua wigo wa ajira pamoja na ukusanyaji kodi wa Serikali. Hali ya mahusiano mabaya iliyopo sasa inaua biasahara
zao, na hivyo kupunguza mapato ya Serikali. Tunaamini kuwa mambo yote hayo yanapaswa kuzungumzwa ili kuboresha mfumo mzima wa utozaji kodi nchini. Pia Viongozi wa Jumuiya na Taasisi za Waislamu Tanzania tunaamini kuwa pamoja na kuboresha mahusiano kati ya watoza kodi na walipa kodi, jambo jingine endelevu la kutilia muhimu ni elimu juu ya umuhimu wa ulipaji kodi nchini.
- SHUGHULI ZA UCHUMI:
Kwa sasa tunaona kuuwa lipo tatizo kubwa la kukosekana kwa ajira nchini, hasa kwa vijana. Tunatambua dhamira ya Serikali ya kuifanya
Tanzania iwe nchi ya uchumi wa kati, unaoendeshwa na viwanda, lakini uchumi huo wa viwanda tunaoujenga bado hatujauhusianisha na sekta za kiuchumi zinazowagusa wananchi wengi wa Taifa letu, ambazo ni kilimo, ufugaji na uvuvi.
Ushauri:
Viongozi wa Jumuiya na Taasisi za Waislamu Tanzania, tunaishauri Serikali ifanye juhudi za makusudi katika kuhakikisha inatoa nafasi zinazoongeza shughuli za kiuchumi nchini, kwa mipango ya miradi maalum, uwekezaji, pamoja na sera za kikodi. Uwepo wa shughuli nyingi zaidi za kiuchumi nchini utaongeza ajira kwa vijana wetu, utaboresha uchumi wa kaya zao, pamoja na kuongeza mapato ya kikodi kwa Serikali.
Mkazo uwekwe katika uendelezaji wa shughuli mbalimbali za kilimo, ufugaji na uvuvi, kwa kuhakikisha upatikanaji wa mapema, na wa bei rahisi, wa mbegu bora, kutoa elimu ya kilimo, ufugaji, na uvuvi bora, kuongeza uwezo wa uhifadhi na usindikaji mazao, kuweka mazingira ya uwepo wa viwanda vya kuongeza thamani mazao hayo,
pamoja na uhakika wa masoko.
- NIDHAMU YA MATUMIZI:
Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, CAG kwa mwaka wa fedha wa 2016/17 imeonyesha kuwa lipo tatizo katika namna Serikali inavyotumia fedha za umma inazozikusanya kutoka katika vyanzo mbalimbali, hasa matumizi ya nje ya Bajeti pamoja na ukopaji wa fedha zaidi ya ukomo unaowekwa na Bunge. Mambo hayo kwa ujumla wake hayaonyeshi nidhamu katika matumizi ya fedha za umma, na huwafanya wananchi wahisi kuwa Serikali yao inatumia vibaya fedha zao za kodi, na hivyo kushusha ari na utayari wao wa kulipa kodi.
Ushauri:
Nidhamu ya Matumizi ya fedha za umma imewekewa misingi kwenye Katiba ya Nchi yetu na Sheria mbalimbali. Viongozi wa Jumuiya na Taasisi za Waislamu Tanzania, tunaishauri Serikali ijiepushe na Matumizi ambayo hayakupitishwa na wawakilishi wa wananchi kwenye Bunge. Pia Serikali kutokuwa na maelezo kwa matumizi makubwa ya Serikali kunaondoa imani ya wananchi kwa Serikali kama
ilivyotokea hivi karibuni baada ya kuwasilishwa kwa Taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Umma. Serikali ikizingatia sheria kwenye matumizi ya fedha za Umma itaepusha ufisadi mkubwa wa kimfumo uliowahi kutokea kwenye nchi yetu mara kadhaa.
D. KATIBA MPYA IWE MSINGI WA MUAFAKA WA KITAIFA
Waislamu hapa nchini, kama sehemu ya jamii ya watanzania, walishiriki kikamilifu katika mchakato wa kuandika Katiba mpya ya nchi yetu, mchakato uliokwama kwa sababu mbalimbali.
Ushauri:
Ni ushauri wetu sisi Viongozi wa Jumuiya na Taasisi za Waislamu Tanzania kuwa umefika wakati muafaka sasa kwa Serikali kurejesha mchakato ule wa Katiba Mpya, ili tujenge msingi mpya wa utaratibu wa kisheria na kikatiba wa Taifa letu.
Lakini, Kutokana na uhalisia wa yaliyojiri wakati wa mchakato wa kupata Katiba hiyo mpya, ni dhahiri kuwa ipo nakisi ya kuaminiana kati ya makundi makuu mawili ya wananchi, kundi linalokubaliana na Katiba Inayopendekezwa na kundi linalokubali Rasimu ya Katiba ya Tume ya Jaji Warioba.
Kwa mazingira hayo, tunashauri kuwa ipo haja ya kuitishwa kwanza kwa Mkutano Mkuu wa Kitaifa wa Katiba. Kazi kubwa ya mkutano huu iwe ni kuweka msingi wa muafaka kati ya makundi hayo, na Taifa zima kwa ujumla, juu ya namna njema ya kurejesha mchakato wa Katiba Mpya. Tunaamini mkutano mkuu wa kitaifa wa Katiba ukifanyika utapandisha kiwango cha muafaka hasa kwenye masuala ambayo bado yanabishaniwa au yamekosa muafaka wa kitaifa na yana umuhimu wa kuingizwa, kubakishwa au kutolewa kwenye katiba mpya. Pia mkutano huu unaweza kupendekeza mambo ambayo yataingizwa kwenye marekebisho ya sheria zitakazosimamia
uendelezaji wa mchakato wa katiba mpya nchini.
Mkutano huu uhusishe uwakilishi mpana wa wananchi kutoka makundi mbalimbali yakijamii, kuanzia viongozi wa Serikali, Vyama vya Siasa, Taasisi za Dini, Asasi za Kiraia, Makundi ya Kitaaluma, Vyama vya Ushirika nk. Lengo likiwa ni kuwa na uwakilishi mpana utakaotoa taswira ya utaifa wetu. Mwisho, sisi viongozi wa dini tuko tayari kuwa daraja la kuwezesha mkutano huo wa kitaifa wa katiba, TUTUMIENI.
E. HITIMISHO
Tunahitimisha salaamu zetu za Eid–l-Fitri kwa kuwatakia Waislamu wote na Watanzania kwa ujumla kheri na fanaka ya sikukuu hii, kuwaomba waendeleze Umoja, Amani na Mshikamano kati yao, pamoja na kubeba mafunzo ya kutenda wema (haki) na kukataa ubaya (batili) yatokanayo na mwezi wa Ramadhani. Zaidi tunawahimiza
kutokukaa kimya wanapoona haki inavunjwa kwani kukemea matendo maovu ni maagizo ya Mtume wetu Muhammad (SAW). Sisi Viongozi wa Dini ya Kiislamu tunataka Tanzania yenye amani na isiyo na aina yeyote ya ubaguzi, yenye kuheshimu haki na usawa wa binaadamu wote na yenye maendeleo.
Wabillahi Tawfiq
Eid Mubarak
Tamko letu sisi Masheikh na Maimamu chini ya Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania limetolewa nasi kwa pamoja chini ya Viongozi wetu:
Sheikh Shaaban Hijja Mrisho
Kaimu Mwenyekiti
Jumuiya ya Taasisi ya Kiislam Tanzania
Sheikh Ponda Issa Ponda
Katibu Mkuu
Jumuiya ya Taasisi ya Kiislam Tanzania