[ATTACH=full]26023[/ATTACH]
Shalom. Ni wakati mwingine tena Bwana ametupa neema ya kuyatafakari maneno yake, hivyo nakukaribisha katika kuyatafakari pamoja.
Lipo jambo tunapaswa tujue kuwa tukisema tu tumemwamini Yesu, kisa tu tumeona anaponya watu, au anafufua watu, au anabariki watu, au amekubariki hata na wewe, hicho sio kigezo cha kuwa Yesu ameikubali imani yako kwake. Hatumpokei Kristo kwa hisia tu, yeye huwa anakwenda zaidi ya hapo?
Katika biblia utaona kuna wakati alipokuwa anakwenda Yerusalemu kwenye sikukuu ya pasaka, na kufika Hekaluni alikutana na mambo ya ajabu, kwasababu mahali ambapo alitarajia watu wamwabudu Mungu, wampe Mungu heshima yake, akawakuta wanapafanyia biashara. Huo ni uvunjifu wa heshima mkubwa sana, hawakuweza kutofautisha vya Mungu na vya Kaisari, Ndipo Yesu alipofika pale kama tunavyoijua habari alizipundua meza zao na kuwafukuza wote, lakini jambo hilo liliwaudhi sana, na ndio ilikuwa sababu mojawapo iliyomfanya wamshitaki ili asulibiwe.
Lakini tunaona Bwana Yesu alipoingia hekaluni, hilo halikumfanya aache kutimiza huduma yake ya kufundisha na kufanya miujiza. Sasa watu wengi walipoona miujiza ile, kwamba viwete wanaponywa, vipofu wanaona, viziwi wanasikia, wenye ukoma wanakuwa wazima, wenye matatizo sugu yote wanaponywa, watu wengi wakaanza kumwamini walipoziona tu zile ishara.
Lakini kwa upande wa Yesu mambo yalikuwa ni tofauti, Yesu ambaye aliijui mioyo ya watu, ambaye aliyajua mawazo ya watu, hakujiaminisha kwao hata kidogo, tusome…
[INDENT]Yohana 2.23 “Hata alipokuwapo Yerusalemu kwenye sikukuu wakati wa Pasaka, watu wengi waliamini jina lake, walipoziona ishara zake alizozifanya.
24 LAKINI YESU HAKUJIAMINISHA KWAO; kwa kuwa yeye aliwajua wote;
25 na kwa sababu hakuwa na haja ya mtu kushuhudia habari za mwanadamu; kwa maana yeye mwenyewe alijua yaliyomo ndani ya mwanadamu”.[/INDENT]
Unaona? Biblia inasema aliwajua wote… hata sasa Yesu anatujua wote,…Embu jaribu kutafakari Yesu ambaye kusudi la kwanza lililomleta hapa duniani lilikuwa ni kuwafanya watu wamwamini yeye wapokee uzima wa milele, ambaye sehemu nyingine alisema wote wajao kwangu sitawatupa nje kamwe. Lakini wakati huu, wote waliotaka kumwamini, hakujiaminisha kwao, ni kwanini? Unadhani anajipinga? Jibu ni hapana!
Yesu anayewajua watu mioyo aliiona mioyo yao, walimwamini kwa hisia tu, kisa wameona Yesu ni muweza, ni mtu wa maajabu, anafanya miujiza lakini hawakuwa tayari kupokea badiliko ndani ya mioyo yao, hawakuwa tayari kuacha kuigeuza nyumba ya Mungu kuwa pango la wanyang’anyi, hawakuwa tayari kupokea ubatizo halisi wa Roho Mtakatifu.
Tukumbuke kuwa Yesu ni yeye Yule jana na leo na hata milele, aliyoyafanya wakati ule anayafanya na sasa. Haijalishi tutakuwa ni kundi kubwa tunaodai tunamwamini Yesu, na tumeongozwa sala ya toba mara nyingi kiasi gani…hilo halijalishi, Tujiulize Je! Katika hayo yote Yesu amejiaminisha kwetu? Hicho ndicho kinachojalisha.
Yesu akijiaminisha ndani ya mtu, Ni lazima maisha ya huyo mtu yawe na badiliko tu. Alipojidhihirisha kwa Zakayo Yule mtoza ushuru, muda ule ule aliacha rushwa zake, akasema nusu ya utajiri wangu naenda kuwapa maskini na niliyemdhulumu namrudishia mara nne… Unaona, watu waliokutana na Yesu jinsi mabadiliko yanavyoanza mara moja…ndipo Yesu akamwambia wokovu umefika nyumbani mwako.
Na sisi pia tukumbuke kuwa Yesu anatujua wote, na hana haja ya mtu kumuelezea hali za mioyo yetu, tukiwa wanafiki mbele zake atajua, vilevile tukiwa na mioyo wa kutaka kupokea mabadiliko atajua tu, haihitaji kujieleza mbele zake, haiitaji tumwimbie kwanza mapambio, hahitaji tulie kwanza, yeye atajua tu na atatupokea na kutupa msaada wa kuushinda ulimwengu.
Yesu ni upendo, lakini anachokitaka ni hichi,
[INDENT]Isaya 66:2” ……asema Bwana; lakini mtu huyu ndiye nitakayemwangalia, mtu aliye mnyonge, mwenye roho iliyopondeka, atetemekaye asikiapo neno langu”.[/INDENT]
Tuifungue mioyo yetu, Bwana ajiaminishe kwetu.
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312