Monday, August 27, 2018
[SIZE=7]Hamahama ya vyama yamkera Askofu Shoo[/SIZE]
http://www.mwananchi.co.tz/image/view/-/4730646/highRes/2091032/-/maxw/600/-/6m3fnpz/-/pic+shoo.jpg
Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Frederick Shoo
[SIZE=5]Kwa ufupi[/SIZE]
Dk Shoo pia amekemea ushindani wa kisasa usio na tija kwa wananchi na hasa miongoni mwa wanasiasa.
By Florah Temba, Mwananchi [email protected]
Moshi. Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Frederick Shoo amesikitishwa na tabia ya wanasiasa kuhamahama vyama akieleza ni jambo linalogharimu Taifa pasipo tija yoyote, lakini mkuu wa wilaya ya Moshi, Kippi Warioba akamjibu akitaka jambo hilo litazamwe pande zote.
Dk Shoo pia amekemea ushindani wa kisasa usio na tija kwa wananchi na hasa miongoni mwa wanasiasa.
Amesema tabia hizo zinapaswa kupingwa na kukemewa vikali na Watanzania wote.
Askofu Shoo alisema hayo jana alipofungua Mkutano Mkuu wa 35 wa Dayosisi ya Kaskazini ya KKKT unaofanyika katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Stefano Moshi (SMMUCo), Kampasi ya Masoka.
Mkutano huo ambao jana ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo maaskofu wa ndani na nje ya nchi na viongozi wa Serikali, utadumu kwa siku tatu.
Pamoja na mambo mengine, wajumbe watamchagua msaidizi wa Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini. Nafasi hiyo kwa sasa inashikiliwa na Mchungaji Elingaya Saria.
Askofu Shoo alisema wao kama viongozi wa kiroho wanafuatilia kwa umakini kinachoendelea nchini kwa wanasiasa kuhamahama vyama na gharama zinazotumika.
Askofu Shoo alisema wanahitaji kuona vyama vya siasa vikishindana kwa hoja.
“Sisi viongozi wa kidini tunafuatilia kwa umakini sana zoezi linaloendelea la kuhama vyama na gharama kubwa zinazotumika. Ndugu zangu, sisi tunapenda kuona vyama vya kisiasa vikishindana kwa hoja na wala si kwa matusi,” alisema.
Dk Shoo alisema, “Unakuta chama cha upinzani kinatukana chama tawala hili si sawa na hapa lazima tuseme. Upande wa chama tawala kuna vijana, unakuta mambo ni malumbano na wakati mwingine matusi yanatumika, tunasema si sawa.”
“Wakati mwingine chuki inatumika, nasema si sawa na wakati mwingine ubabe unatumika nasema si sawa,” alisema Dk Shoo.
Akitumia mfano wa timu za mpira nchini, Dk Shoo alisema, “Hapa Tanzania tunazo timu mbili za soka, na ukitaka kuzungumza habari za mchezo wa Tanzania lazima uzungumze habari za Simba na Yanga na pasipo Simba na Yanga hakuna mpira Tanzania.”
“Na Simba ili iwe Simba, inamuhitaji Yanga, tena inamuhitaji Yanga mwenye afya, mwenye kuelewa. Mimi nimesema, ni ushauri tu,” alisema.
Alisema roho za ushindani zinapaswa kukemewa na kuachwa na kwamba zinahitajika roho za ushirikiano, upendo na maridhiano na hasa wakati huu kwa maendeleo ya nchi.
[COLOR=rgb(226, 80, 65)]“Kubaguana, kusakamana, kunyimana haki hata zile za msingi kwa sababu tu za kiitikadi, kidini, kikabila hakukuwahi kuwa msingi wa maendeleo endelevu kwa Taifa lolote duniani,” alisema Dk Shoo.
Alisema kanisa halitaacha kuwa sauti ya kinabii katika kuonya, kufundisha na kukemea pale linapoona haki inakiukwa kwa misingi ya kiitikadi, dini na ukabila.
Dk Shoo alisema ni lazima watu watambue na kuheshimu kuwa kanisa ni la Mungu, naye ameliweka kwa makusudi yake na amelipa wajibu wa kuomba, kuonya na kufundisha.
[COLOR=rgb(226, 80, 65)]“Tusilegee katika hili na wala tusizuiwe na yeyote katika hili; kutimiza wajibu huo, tukaze ibada, mafundisho, maonyo na maombi na kamwe kanisa lisiache na hapa napenda kusisitiza kanisa halitaacha kuwa sauti ya kinabii,” alisema Askofu Shoo.
[COLOR=rgb(226, 80, 65)]“Kanisa limepewa wajibu, na sisi tunaomwamini Yesu Kristo, tumekuwa sehemu ya kanisa la Bwana, ni wajibu wetu kutambua vipawa ndani ya kanisa na kuvitumia kwa upendo ili kulijenga na asiwepo anayenyimwa nafasi ya kutumia vipawa katika mwili wa Kristo kulijenga kanisa,” alisema.
[COLOR=rgb(226, 80, 65)]Alisema katika kuhudumiana katika kuujenga mwili wa Kristo, kipaumbele cha kwanza cha Kanisa ni kuujenga mwili wa Kristo, roho za watu, afya na usalama wa roho ya kila mmoja, watu wa marika yote wa vyeo vyovyote na wa kila namna, wakubwa na wadogo
Uchaguzi serikali za mitaa
Akizungumzia uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika mwakani, Dk Shoo alisema ili kuwapata viongozi bora na waadilifu, kunahitajika malezi bora kwa vijana ambayo yatajikita katika uzalendo na upendo kwa nchi.
“Tunapoingia katika uchaguzi wa serikali za mitaa, tusiangalie dini ya mtu, angalieni mtu huyu ni mcha Mungu, ana maadili na tusikubali kuhongwa kwa namna yoyote. Ili kupata watu wa namna hiyo, lazima tuanze kulea watoto wetu na vijana katika maisha ya kumjua Mungu,” alisema.
Askofu Shoo alisema ni lazima kuwekeza kwa vijana na kuna haja ya kanisa kuwekeza katika kuwafundisha na kuwawezesha wazazi wachanga kuwa wazazi bora kwa watoto wao.
Kufanya hivyo alisema kutawezesha kupata viongozi na wataalamu wa baadaye ambao watakabidhiwa madaraka ya kuiongoza na kuisaidia jamii.
Alisema kuna haja ya kuimarisha malezi ya familia, wazazi kubeba jukumu la kuzilea familia na kuepuka kuiachia mitandao iwalee.
Huduma za afya
Dk Shoo aliipongeza Serikali kwa jitihada za kuboresha huduma za kijamii zikiwamo kuwawezesha wananchi kupata matibabu ya moyo na figo.
Aliishauri Serikali kuhakikisha jitihada hizo zinakwenda sambamba na upatikanaji wa idadi kubwa ya madaktari bingwa wa fani mbalimbali, ambao watapewa motisha na masilahi bora ili kuepuka kukimbilia kufanya kazi nje ya nchi.
DC Moshi amjibu Askofu Shoo
Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kippi Warioba akitoa salamu za Serikali katika mkutano huo alisema Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa kanisa kuhakikisha yale ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi kuboresha maendeleo yanafanyika. Kippi aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira katika mkutano huo, alisema Serikali inatambua mchango mkubwa wa kanisa na ina uthamini kuhakikisha linaikumbusha jamii.
Alilitaka kuongeza ushirikiano na mshikamano ili kuhakikisha malengo ya kuihudumia jamii yanafanikiwa.
Kuhusu hamahama ya wanasiasa, Kippi akitumia timu za mpira alisema, “Baba Askofu umegusa uwanja wa mpira na kutaja timu zile, timu zipo na zile timu na maeneo mengine inabidi utuachie kidogo tucheze kule uwanjani.”
Kippi alisema, “Wakati mmoja Baba Askofu walitoka viongozi kutoka timu moja wakubwa; makocha na mameneja wakaenda timu ya pili, nchi ikatikisika; tukaongea lakini ile timu ya upande wa pili iliongea na kusemezana huko ndani na kufanya fujo uwanjani. Ilionekana sawa na sahihi mbele ya macho ya watu.”
“Lakini inatokea tena sasa wachezaji, wengine wadogowadogo wa timu ya upande huohuo wanarukia upande wa timu nyingine, unasikia mambo mengi na malalamiko ya hapa na pale kwamba inawezekana wanarubuniwa ama hiki au kile. Baba Askofu, wengine ninazungumza nao mimi wanasema niko tayari kuja upande huo, iko hivyo,” alisema Kippi.
Alisema dhamira ya askofu ya kutaka uwanja mzima uwe na afya zaidi ni muhimu. Aliwataka wajumbe wote waliohudhuria mkutano huo kuepuka kuwa sehemu ya kutumika kuharibu au kubomoa uwanja huo na ushiriki wake, badala yake kuimarisha utaratibu wa uchezaji kwenye uwanja ili mchezo ufanyike katika utaratibu ambao umekubalika kisheria.
Meya atoa neno
Meya wa Manispaa ya Moshi, Raymond Mboya alisema viongozi wana wajibu wa kusimamia haki, kwa kuwa amani ni tunda la haki na hakuna sababu ya kuimba amani bila kusimamia haki.
“Jukumu letu la kwanza kama viongozi ni kusimamia haki na amani itatawala kwa watu wote. Amri kuu ya Mungu inasema tupendane na kama viongozi tuna jukumu la kuitendea haki jamii tunayoiongoza,” alisema.
Mboya alisema, “Askofu ulitoa mfano wa timu za mpira, ni kweli hukutaka kwenda ndani lakini tulijua ulimaanisha nini na ulisema ili Simba iwe imara ni lazima Yanga iwe na wachezaji imara, na timu moja ikianza kuchukua wachezaji wa timu nyingine, timu hiyo haitakuwa na wachezaji na timu iliyochukua wachezaji itabidi icheze na timu ya kata, na kiwango kitashuka.”
Alisema ili kuwe na CCM imara ni lazima kuwe na chama cha upinzani imara.
“Hatuhami hivihivi, mimi meya nimepigiwa simu nikaambiwa njoo huku upewe nafasi nimesema ili tuwe na CCM imara ni lazima tuwe na upinzani imara, Tanzania ni yetu sote,” alisema.
Waraka wa pasaka
Askofu Shoo amezungumza hayo ikiwa ni miezi mitano tangu maaskofu 27 wa kanisa hilo watoe Waraka wa Pasaka ambao licha ya kuikosoa Serikali, ulizungumzia hali ya kiuchumi nchini ukipongeza juhudi zinazofanywa za kukusanya kodi, umuhimu wa kushirikisha sekta binafsi katika mikakati ya maendeleo, utawala bora, demokrasia ya vyama vingi, usalama wa raia na masuala mengine mtambuka .
Kutokana na waraka huo wa Machi 24, Wizara ya Mambo ya Ndani iliwataka kuomba radhi ndani ya siku kumi, lakini Dk Shoo akizungumza mbele ya makamu wa Rais Samia Suluhu mkoani Tabora alisema waraka huo haukuwa wa bahati mbaya.
Dk Shoo alitoa kauli hiyo Juni 10 katika ibada ya kusimikwa askofu wa kwanza wa Dayosisi ya Magharibi Kati, Isaac Laiser mkoani Tabora ikiwa zimepita siku mbili tangu aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Mwigulu Nchemba kuikana barua ya msajili wa vyama vya hiari iliyoitaka kanisa hilo kuufuta waraka huo.
Katika ibada hiyo, wakati Dk Shoo akimpongeza Rais John Magufuli kwa kushughulikia jambo hilo, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye pia alishiriki ibada hiyo aliwataka viongozi wa dini kuendelea kuikosoa Serikali kwa kutumia lugha watakayoelewana.