HALI ZETU JINSI ZINAVYOWEZA KUATHIRI UTOAJI WETU.

[INDENT]Mithali 11:24 “Kuna atawanyaye, lakini huongezewa zaidi; Kuna azuiaye isivyo haki, lakini huelekea uhitaji”.[/INDENT]
Shalom, Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe. Karibu tena tuyatafakari maandiko.

Kuna kanuni Mungu kaziweka katika maisha ambazo ni vizuri tukazielewa ili tusije tukajikuta tunaangamia kwa kukosa maarifa, na kukosa maarifa ni pamoja na kuhangaika huku na huko kutafuta maombezi wakati misingi ya Neno la Mungu iliyo imara tumeiacha nyuma…

Kwamfano mtu anaweza akawa anasumbuliwa na tatizo Fulani labda tuseme, na nguvu za giza,… lakini kwa kukosa tu maarifa ya kujua kwamba damu ya Yesu Kristo ndiyo inayoondoa mizizi yote ya nguvu za giza ndani ya mtu, pale anapoamua tu kuokoka kwa kumaanisha na kubatizwa…Sasa mtu huyo kwa kutolizingatia hilo anataka mambo hayo yaondolewe kwa njia ya maombezi na huku bado yupo katika dhambi, bado ni mzinzi, bado anaishi na mke/mume ambaye si wake, bado ni mlevi, bado anavaa mavazi yake ya kikahaba, na wakati huo huo anataka kuombewa mapepo yamtoke.

Sasa Kwa namna ya kawaida mapepo hayo hayamwacha yamesoge pembeni tu. Atajiona kama amepata tu unafuu, lakini baada ya muda tena hali yake itamrudia, na itakuwa mbaya zaidi kuliko hata ilivyokuwa hapo mwanzo.

Hiyo yote ni kutokana na kukosa maarifa sahihi ya kulitatua tatizo lake.

Jambo lingine ambalo tunapaswa tujifunze pia, Ni katika suala la utoaji. Kwa hali ya kibinadamu kutoa huwa ni kugumu kuliko kupokea…Licha ya kuwa utoaji ni nguzo muhimu kwa mtu yeyote Yule (awe mwenye dhambi asiwe mwenye dhambi )…

Lakini linapuuziwa na wengi hata na kwa watu waliookoka.

Lakini fahamu kuwa ukitaka uwe mtoaji mzuri, unapaswa uishinde hali yako ya sasa… “Hali zetu ni adui mkubwa wa matoleo yetu”…Siku zote ukiangalia hali yako ilivyo, ukianza kupiga gharama hujafanya hiki, hujafanya kile, hata kama wewe ni bilionea utoaji wako bado utakuwa ni mgumu tu, …kwasababu Utawaza sijawekeza kwenye hichi au kwenye kile. Vivyo vivyo hata na kwa Yule aliye na kipato cha kawaida naye akishaanza kujifikiria tu hali yake ilivyo, sijanunua, tv, sijanunua simu, sijanunua viatu, n.k. basi utoaji wake naye ndipo unapopitia ukinzani.

Kwasababu kile alichonacho hakitamtosha kukidhi matakwa yake, na huku tena afikirie kumsaidia mtu mwingine bado itakuwa ngumu, au kutoa sadaka hapo hapo kwake yeye vilevile itakuwa ngumu. Nataka nikumbie kila siku tutakuwa na uhitaji tu, hatutakoma kuwa na mahitaji hata tufanikiwe vipi, kikubwa ni kuzishinda hali zetu.

Lakini kanuni za Mungu ni tofauti, kama tukiweza kuzishinda hali zetu, au bajeti zetu, na kusema ngoja nifungue mkono wangu kwa hiki au kile, kumsaidia huyu mwenye uhitaji au Yule, au kutoa sadaka, na kuisapoti kazi ya Mungu isonge mbele, kawapa mayatima kitu kidogo, tukinyoosha mikono yetu katika mambo kama hayo …Basi tujue kuwa huo ndio utakuwa mwanzo wa Baraka zetu, lile wingu la utukufu wa Mungu litatembea na sisi wakati wote.

Na andiko hili litatimia juu yetu;

[INDENT]“Kuna atawanyaye, lakini huongezewa zaidi; Kuna azuiaye isivyo haki, lakini huelekea uhitaji”.[/INDENT]
Kwa jicho la kibinadamu utaonekana kama ni mtu usiyekuwa na malengo, au mtu usiyekuwa na bajeti ya maisha, lakini Mungu hatakuacha…Siku zitakuja siku zitakwenda, ipo milango ambayo Mungu atahakikisha anakufungulia ki-miujiza miujiza, utashangaa, umewezaje kuvuka hapa au pale, Utashangaa kile ulichokipoteza Mungu anakurudishia na zaidi, na utakuwa umepata faida mara mbili…kujiwekea hazina mbinguni, na hapa duniani.

[INDENT]Luka 6:38 “Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa”.[/INDENT]
Lakini kama kila kitu tunachokipata tunasema hichi ni cha kwetu tu,.tuna malengo mengi ya kufanya, mwaka huu nataka nifanye hivi au vile hivyo kwasasa sina fedha ya kwenda nje ya bajeti yangu…Siwezi kumsaidia ndugu yangu huyu mwenye shida hii, siwezi kuwasidia yatima wale, siwezi kumtolea Mungu…nataka nikuambie tutajiona kama tunakusanya, na fedha zetu hazipotei bure,zipo katika bajeti, lakini tutabakia katika hali hiyo hiyo miaka nenda miaka rudi, na mwisho wa siku tutajikuta malengo yetu kuyafikia bado yapo mbali na sisi…

Na hivyo Neno hili nalo pia linatimia juu yetu: “Kuna azuiaye isivyo haki, lakini huelekea uhitaji”.

Tutaelekea uhitaji ikiwa tutazuia matoleo yetu,…Hivyo utoaji ni jambo la muhimu sana, katika kuvuta Baraka za Mungu katika maisha yetu. Tendo moja la utoaji lina nguvu hata mara elfu kumi zaidi ya Maneno tunayomuomba Mungu kila siku atubariki katika sala. Lakini pia kumbuka katika kumtolea Mungu madhabahuni au katika kazi yake…zingatia kuwa msafi kwasababu Mungu wetu hapedezwi tunapomtolea sadaka na wakati ndani ya mioyo yetu tupo mbali naye…

Na ili tuwe watoaji wazuri, tupunguze msisitizo katika kuzitazama hali zetu za sasa. Na Bwana atatubariki, kama alivyoahidi katika Neno lake, kwasababu yeye si mwongo.

Ubarikiwe.

https://wingulamashahidi.org/