SUNDAY, JULY 8, 2018
Bodaboda kufungwa matela kudhibiti ajali
Kwa ufupi
Mkakati huo umetangazwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola
By Kalunde Jamal, Mwananchi
Dar es Salaam. Ni siku saba tangu ameteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amekuwa mjadala katika vyombo vya habari kutokana na kauli na mikakati yake mbalimbali anayopanga kuifanya.
Jana Julai 7, 2018 katika maonyesho ya kimataifa ya biashara maarufu Sabasaba, Lugola alieleza mkakati wake wa kupunguza ajali za pikipiki.
Amesema Serikali inajipanga kuja na utaratibu wa kufunga tela katika pikipiki, kwamba abiria wataweza kupanda kati ya mmoja hadi wanne na kuketi katika tela hilo jambo ambalo litazifanya pikipiki hizo kutokimbia, kushindwa kupenya kwa vurugu katika foleni.
Amebainisha kuwa ufungwaji huo wa matela hautazihusu pikipiki za watu binafsi.
Amesema zoezi la ufungwaji wa matela hayo litafanyika nchi nzima. Lugola alitoa kauli hiyo alipotembelea banda la Jeshi la Polisi katika maonyesho hayo.
Lugola ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), amesema lengo la hatua hiyo ni kupunguza mwendo kasi wa pikipiki hizo, kushindwa kupenya katika foleni ili kulinda usalama wa raia.
"Bodaboda dawa yenu inachemka, Serikali inakuja na mpango madhubuti wa kupunguza kama si kumaliza kabisa ajali za barabarani zinazosababishwa na madereva pikipiki,” amesema.
"Tutawafungia matela ya kubebea abiria na nyie mkae kwenye foleni kama bajaji na magari mengine. Matela haya yataleta utulivu barabarani lakini pia yatawaongezea tija kwani badala ya kubeba abiria mmoja, sasa mtapakia zaidi.”