Riwaya:Dunia Haina Usawa

ERIC SHIGONGO
DUNIA HAINA USAWA

Kila mtu alitaka kufahamu kile kilichokuwa kikitaka kuzungumzwa na Bilionea Kizota. Huyo alikuwa mwanaume mwenye pesa nyingi kuliko wote nchini Tanzania, maisha yake yalikuwa ya siri sana kiasi kwamba kuna watu wengine hawakuwa wakifahamu alifananaje.
Ilikuwa vigumu kumuona katika magazeti, televisheni au sehemu nyingine, alikuwa mzee aliyeishi kisiri sana kiasi kwamba kuna wengine hawakuwa wakiamini kama mzee huyo alikuwa mwembamba, mwenye sura ya kimasikini kuliko vitu alivyokuwa akimiliki.
Baada ya saa moja, tayari waandishi wa habari walikuwa nje ya jumba lake la kifahari lililokuwa Osterbay jijini Dar es Salaam. Haikuwa rahisi kuingia hivihivi, waliambiwa mmoja mmoja kwenda kusimama sehemu moja kulipokuwa na taa ya rangi ya bluu ambayo iliwaonyesha kila kitu walichokuwa nacho.
Nyumba ilikuwa na ulinzi mkubwa sana, waandishi wa habari wote walichunguzwa lakini hakukuwa na mtu aliyeonekana kuwa na silaha yoyote ile. Wakaruhusiwa kuingia ndani na kupelekwa sehemu fulani iliyokuwa na viti pamoja na hema na kuambiwa wasubiri hapo.
Wakatulia na kuanza kufunga mitambo. Walikuwa wakimsubiri bilionea huyo ambaye alikuwa akijiandaa tayari kwa kuzungumza na waandishi hao. Alitaka kuzungumza mambo fulani ambayo yalikuwa ni siri sana, mambo ambayo hakukuwa na mtu aliyekuwa akiyafahamu.
“Bro! Nimefika,” alisema mwanaume mmoja aliyekuwa na kaera, wakati waandishi wa habari wenzake wakiwa wameingia ndani, yeye ndiyo kwanza alikuwa akifika.
“Wewe nani?”
“Mwandishi kaka!” alijibu mwanaume huyo huku akimuonyeshea kamera aliyokuwa ameishika.
“Kutoka wapi? Kitambulisho chako kiko wapi?’ aliuliza mlinzi huku akimwangalia mwanaume huyo.
Hapohapo akachukua kitambulisho na kumuonyeshea mlinzi, kitambulisho kilichomuonyesha kwamba alikuwa mwandishi wa habari kutoka katika Mtandao wa Omen ambao ulikuwa ukitikisa kipindi hicho.
Akaambiwa aende kusimama katika taa ile ya kuwachunguzia watu ili kuonekana kama hakuwa na silaha yoyote ile, akaenda, akasimama na kummulika kisha kuruhusiwa kuingia ndani.
Mwandishi huyo alikuwa Godwin. Alifika mahali hapo kwa kuwa alitaka kufanya kitu kingine kabisa. Alitembea kwa kujiamini, hakuwa na hofu hata kidogo na kila mtu aliyemwangalia, kwa jinsi alivyokuwa alionekana kuwa mwandishi kweli.
Alikwenda mpaka walipokuwa wenzake na kutulia hapo. Baada ya dakika kadhaa, Bilionea Kizota akafika mahali hapo. Kwa jinsi alivyoonekana, alikuwa amekonda, ilikuwa ni vigumu kuamini kama mtu mwenye pesa ambaye siku chache zilizopita alikuwa na mwili wa kawaida leo hii alikuwa vile.
Kichwa chake kilimpa mawazo, kila mwezi alikuwa na uwezo wa kuingiza bilioni tatu lakini kitu cha ajabu kabisa, alikuwa mtu wa mawazo mengi kuliko hata mtu masikini ambaye alilala pasipo kuwa na chakula chochote.
Waandishi wa habari wakaanza kumpiga picha tangu alipokuwa akiingia mpaka alipokwenda kukaa. Godwin hakutulia, kama walivyokuwa wenzake, naye alikuwa akishughulika sawa na wao na kutulia sehemu yake.
Alimwangalia bilionea huyo, alitia huruma, alipoteza mwili wake mkubwa, kwa kumwangalia mara moja, ilikuwa ni vigumu kuamini kama mtu huyo alikuwa bilionea. Akatulia kwenye kiti, kabla ya kuzungumza chochote kile, akaanza kuwaangalia waandishi hao.
“Nimefurahi sana kuwaona mahali hapa. Najua wengi mnashangaa jinsi nilivyopungua. Ndugu zangu, kuna wakati unakaa na kuingiza pesa nyingi lakini hiyo haitoshi kuonyesha kama umefanikiwa,” alisema Kizota huku akiendelea kuwaangalia watu waliokuwa mahali hapo.
“Siamini pesa ndiyo inaweza kumfanya mtu kuwa tajiri. Tajiri pekee ni yule ambaye ana vitu ambavyo pesa haiwezi kununua kama furaha, faraja, amani. Mimi ni masikini, nina pesa lakini haziwezi kununua furaha, kuna haja gani ya kuwa na pesa?” aliuliza Kizota, alivyokuwa akizungumza, alionekana kuwa na jambo kubwa moyoni mwake.
Alizungumza mambo mengi mno lakini mwisho kabisa aliwaambia kile kitu kilichoujaza moyo wake kwamba kuna wakati alitamani kufa, kuondoka katika dunia hii kwa kuwa kuna jambo ambalo halipo sawa kabisa.
“Jambo gani?” alidakia Godwin, hakutaka kuchelewa.
“Siipendi serikali hii, simpendi rais hata kidogo. Ninamchukia kwa sababu yeye ndiye amekuwa chanzo cha mambo yote, yeye ndiye amekuwa sababu ya mimi kukosa furaha,” alisema Kizota, machozi yakaanza kumlengalenga.
“Kwa nini?” Godwin akadakia tena kiasi kwamba mpaka baadhi ya waandishi wakaanza kushangaa kwani hakukuwa na mwandishi wa habari aliyeonekana kujiamini kama yeye.
“Nilitishiwa maisha kwa sababu ya serikali hii. Jana tu Noel alijiuzulu nafasi yake, najua inawezekana kuna kitu kimemtokea ambacho hata mimi kimenitokea. Jifikirie kwa nini yanatokea haya yote? Jibu ni jepesi kwamba rais ndiye anayesababisha haya, bila rais kuwa na serikali ya kipuuzi haya mambo yote yasingeweza kutokea. Kama wananchi wanapata wanachokitaka, unahisi haya yote yangetokea? Kama rais angekuwa siyo muuaji unafikiri haya yote yangetokea? Hakuna kitu kama hicho. Rais ndiye katunyima furaha, katufanya tutekwe. Kama Noel alisema wazi hamuungi mkono rais, hata mimi pia simuungi mkono hata kidogo,” alisema Kizota.
Hakuogopa, moyoni mwake alikuwa na mzigo mkubwa lakini baada ya kufunguka kwa kirefu na kutoa dukuduku lake, moyo wake ukawa na amani, akahisi kama alikuwa ameutua mzigo mzito aliokuwa ameubeba.
Kila mwandishi alikuwa akishangaa, hawakuamini kama bilionea huyo angezungumza maneno kama hayo tena akiwa laivu kabisa. Wengi wakahisi kwamba kungekuwa na kitu kibaya ambacho kingetokea mahali hapo kwani kama kila mtu alikiona kipindi hicho, rais Bokasa asingekubali kuona akichafuliwa, kwa kutumia cheo chake, mabavu yake basi angetuma polisi kwenda huko na kumkamata.
Walichokuwa wakikihisi ndicho kilichotokea, huku bilionea huyo akiendelea kuzungumza na waandishi, magari mawili ya polisi yakafika nyumbani hapo, kwa mwendo wa kijeshi polisi wakaingia ndani na kumkamata mzee huyo ambaye muda wote alikuwa akisema kwamba ilikuwa ni bora kukamatwa kuliko kuendelea kuishi huku akiwa hana amani moyoni mwake.
“Hata kama kufungwa nitakuwa tayari! Ninachokitaka ni kuwa na amani moyoni mwangu tu. Inatosha,” alisema bilionea huyo wakati amechukuliwa na kupandishwa ndani ya gari na kuondolewa mahali hapo.
Waandishi wa habari hawakuwa na nongwa, walichokifanya ni kuendelea kupiga picha kila kitu kilichokuwa kikitokea mahali hapo. Kwa hilo, Watanzania wengi walikasirika, chuki dhidi ya Rais Bokasa ikazidi kuongezeka kwani kwa kile alichokizungumza bilionea huyo kilikuwa kitu cha kawaida, alitoa dukuduku lake na hakutakiwa kukamatwa kama ilivyokuwa imetokea.
“Ila Kizota alikuwa na haki kabisa. Kwani katukana? Kwani kasingizia? Alichokizungumza ndiyo ukweli wa mambo,” alisema jamaa mmoja alipokuwa akizungumza na wenzake maskani.
“Shiiiii! Sasa hivi Usalama wa Taifa kila kona, unaweza kudakwa, hayo mambo kalalamikie chumbani ukiwa na mkeo,” alisema jamaa mwingine, kwa jinsi hali ilivyokuwa nchini, hakukuwa na haja ya kumwamini mtu yeyote yule.


Ndani ya siku chache tu, tayari urafiki baina ya Halima na Winfrida ulikuwa mkubwa. Walikuwa wakikutana na kuzungumza mambo mengi, alimpenda msichana mwenzake huyo kwa kuwa alikuwa na sura nzuri, msikivu na aliyeonekana kufahamu mambo mengi mno.
Halima alihisi kwamba alikuwa kwa mtu sahihi, aliamini kwamba Godwin aliyekuwa amezungumziwa ambaye alikuwa mpenzi wa Winfrida ndiye ambaye walikuwa wakimtafuta kwa udi na uvumba.
Baada ya kuzoeana sana ndipo Winfrida akaamua kumkaribisha Halima nyumbani kwake. Hiyo ikaonekana nafuu kwa msichana huyo kwani aliamini kwamba mara baada ya kufika huko angepata nafasi ya kumuona huyo Godwin na kupanga mikakati juu ya kumkamata mwanaume huyo.
Siku ambayo alikwenda nyumbani hapo alishangaa, hakukuonekana kuwa pazuri hata kidogo. Kulikuwa na godoro chini, chumba kibovu na humo ndani hakukuwa na kitu chochote kilichoonekana kuwa na gharama yoyote ile.
Halima alibaki akishangaa, alipoondoka nchini Somalia aliambiwa kwamba mwanaume aliyekuwa akienda kupeleleza huko alikuwa na uwezo mkubwa wa kuchezea kompyuta lakini pia alikuwa amehamisha kiasi kikubwa cha pesa kutoka benki lakini kwa jinsi alivyokuwa akikiangalia chumba hicho, hakikufanana na zile sifa za mtu huyo ambazo aliambiwa.
Akavumilia, alichokitaka ni kumuona mwanaume mwenyewe, alifananaje na alikuwa na uwezo gani hata kwenye kuzungumza. Hilo halikuwa tatizo lolote kwani baada ya saa mbili, Godwin akafika nyumbani hapo, alikuwa ametoka katika mkutano aliouandaa Bilionea Kizota kwa ajili ya kuzungumza na waandishi wa habari.
Alipofika nyumbani hapo na Halima kutambulishwa kwamba alikuwa mpenzi wa Winfrida aliyeitwa Godwin, hakuamini kama kweli mwanaume huyo ndiye ambaye alikuwa akiwasumbua Usalama wa Taifa wa Uswisi, FIS kwani muonekano wake ulikuwa wa kimasikini mno, alichoka na alionekana kutokuwa hata na shilingi mia tano mfukoni.
“Huyu ndiye mpenzi wako?” aliuliza Halima, hakuwa akiamini.
“Ndiye yeye! Yupoje kwani?”
“Mmh! Hakuna kitu! Ni mwanaume mzuri sana,” alijibu Halima.
Alichokifanya msichana huyo ni kuchukua miwani yake ya macho na kuivaa. Ilionekana kama miwani lakini ukweli wa mambo haikuwa miwani ya kawaida bali ilikuwa na kamera ambayo ilipiga picha moja kwa moja na kuzipeleka nchini Uswisi.
Ili kuwapa taarifa wenzake akamwambia Winfrida kwamba alitaka kwenda chooni kujisaidia haja ndogo, alipoonyeshewa, akaelekea huko, alipofika, akavua miwani ile na kuanza kuiangalia, kamera ndogo ikaanza kumpiga.
“Nimefanya kazi kwa kipindi kichache, nimempata Godwin ambaye sidhani kama ndiye yeye,” alisema Halima huku akitumia simu yake aliyoiunganisha na bluetooth ambayo ilipeleka taarifa kupitia miwani ile.
“Ndiye yule uliyempiga picha?”
“Ndiyo! Na pale ndipo anapoishi!”
“Yaani kwenye lile jalala?”
“Kile ni chumba!”
“Hapana! Atakuwa si huyo. Huyo tunayemtafuta ni yule aliyechukua pesa benki, yule ambaye anaisumbua serikali yetu mpaka ya huko Tanzania,” alisikika Bwana Kom.
“Kwa hiyo huyo si yeye?”
“Sijajua! Hebu endelea kuchunguza zaidi, nenda kampige picha zaidi,” alisema Kom.
“Sawa,” aliitikia Halima, hapohapo akaivaa miwani ile, akaufungua mlango, akashtuka, macho yake yakatua kwa Godwin ambaye naye alikuwa mlangoni hapo na dalili zilionyesha kwamba alisikia kila kitu kilichokuwa kimezungumzwa ndani.
“Ooh My Gosh…” alijikuta akisema huku macho yake yakitazamana na macho ya Godwin aliyekuwa amesimama karibu naye kabisa kwenye mlango wa choo.


Tangu Godwin alipoingia ndani ya chumba chake na macho yake kutua kwa msichana Halima, akawa na hofu kwamba inawezekana msichana huyo alikuwa mbaya kwani kwa muonekano alioonekana, hakuonekana kama msichana aliyekulia maisha ya Tanzania, ngozi yake, muonekano wake ulimtia shaka kupita kawaida.
Walikaa na kuzungumza, muda mwingi alikuwa akimwangalia Halima kiwizi, bado moyo wake ulikuwa na hofu na msichana huyo, alihisi kabisa kwamba alikuwa mtu mbaya ambaye hakutakiwa kabisa kuwa karibu naye.
Halima alizungumza mambo mengi chumbani pale mpaka alipotaka kuelekea chooni. Haraka sana naye Godwin akaaga kwamba alikuwa akienda nje, alipofika huko, alikuwa akihesabu sekunde huku akikadiria kwamba muda huu Halima alikuwa amekwenda chooni au bado.
“Atakuwa amekwenda, hebu subiri niende,” alisema Godwin.
Hakutaka kuchelewa, haraka sana naye akaelekea chooni kwani hakuamini kama kweli msichana huyo alikuwa ameshikwa na haja kweli au la. Alipofika huko, akanyata na kusogea karibu na mlango na kuanza kuisikiliza sauti ya msichana huyo ambaye alikuwa akizungumza na mtu mwingine kwa simu.
Mazungumzo yote aliyasikia, akapata uhakika kwamba Halima hakuwa msichana wa kawaida kama alivyosema Winfrida, akapata uhakika kwamba msichana huyo alifika mahali hapo kwa ajili ya kumpeleleza na kujua kama alikuwa ndiye yeye au si yeye.
Halima alipotoka chooni, macho yake yakagongana na Godwin ambaye alijifanya kutokujua kitu chochote kile kilichokuwa kikiendelea, alimwangalia msichana huyo, hapohapo akaanza kutoa tabasamu.
“Umemaliza?” aliuliza Godwin.
“Kumalizi nini shemeji?”
“Kujisaidia ili na mimi niingie manake tumbo limeanza kunivuruga,” alisema Godwin huku akiachia tabasamu pana lililokuwa na lengo la kumsahaulisha msichana huyo, asijue chochote kama kweli mwanaume huyo alikuwa Godwin aliyekuwa akimtafuta.
“Nimemaliza!” alisema Halima, akateremka ngazi ndogo na kuelekea chumbani. Godwin akaingia chumbani kwake, moyo wake ulikuwa na hofu, alijua dhahiri kwamba kama asingefanya lolote liwezekanalo basi msichana huyo angeweza kumkamata kizembe sana. Alichokihitaji kwa wakati huo ni namba yake ya simu tu.
Alipokaa kwa dakika kadhaa, akarudi chumbani ambapo akaungana na wasichana hao na kuanza kupiga nao stori. Alimuonyeshea Halima hali ya kumzoea sana, hakutaka msichana huyo awe na hofu yoyote ile, mwisho kabisa wakati akiaga, akamuomba namba ya simu ambapo kwa Halima halikuwa tatizo lolote lile, akamgawia ili kumfanya kuwa karibu naye.
“Amekwisha!” alisema Godwin.
Halima aliyejulikana kwa jina la Angelica akaondoka huku Winfrida akimsindikiza, haraka sana Godwin akachukua kompyuta yake ya mapajani na kuiwasha, alitaka kufanya vitu kwa haraka, kuingilia mawasiliano ya msichana yule.
Akaiingiza namba ile katika kompyuta yake na kisha kuifungua progamu yake iitwayo SpyGd ambayo aliitengeneza yeye mwenyewe na hakuwa ameisambaza sehemu yoyote ile. Akaiingiza namba ile, kompyuta ikaanza kumuonyeshea sehemu iliyoandikwa download ambapo kwa mbele kulikuwa na asilimia zilikuwa zikisogea mbele.
Ilipofika asilimia mia moja, ikabadilika na kujiandika searching, ikaanza kuitafuta simu ile na ilipoipata, ikaanza kuonyesha asilimia nyingine zikipanda huku kukiwa na neno lililoandikwa Hacking process.
Mpaka inafika mia moja, tayari alikuwa na uwezo wa kuingia katika simu ya Halima. Aliangalia meseji zote, aliona mawasiliano yote na kulikuwa na namba moja kutoka nchini Uswisi ambayo alikuwa amepigiwa na kupiga.
Alichokifanya ni kukata mawasiliano baina ya namba yake na namba ile ya Uswisi na kisha kuiingiza namba yake kwa namba ile na kuiiba kisha kuingia Google, akatafuta picha ya mwanaume mweusi kisha kuandika ujumbe kwenda kwa Halima huku akitumia namba ile ya Uswis, ujumbe uliosomeka:
“We have found his picture,” (tumeipata picha yake) aliandika.
Ujumbe huo ukaenda kwa Halima, alipoupata, haraka sana akaandika ujumbe wa kuomba kutumiwa picha hiyo ili aone kama kweli yule aliyekuwa amempata alikuwa ndiye yeye au mwingine.
“Send it to me,” (nitumie)
Hapohapo Godwin akamtumia picha ya mwanaume yule aliyoitoa Google. Ilikuwa picha ya mwanaume mweusi, Halima alipoiona na kuikumbuka sura ya Godwin ambaye alikutana naye, vilikuwa vitu viwili tofauti.
“Is he the one you found?” (ndiye yeye uliyempata?) aliuliza Godwin pasipo Halima kujua kama alikuwa akiwasiliana na mwanaume huyo.
“No! This is another one,” (hapana! Huyu mwingine kabisa) alijibu Halima.
Msichana huyo alichanganyikiwa, alijipa uhakika kwamba hatimaye Godwin alikuwa amepatikana lakini ujumbe wa simu alioupata kutoka nchini Uswisi tena huku ukiambatanisha na picha ya huyo Godwin aliyekuwa akitafutwa, ukamvunja moyo na kuona kwamba kazi kubwa aliyokuwa ameifanya haikuwa na faida yoyote ile.
Huo ndiyo ukawa mwisho wa kuelekea kwa Godwin kwani aliamini kwamba hata kama angekwenda huko na kudumisha urafiki na Winfrida bado kungekuwa na ugumu wa kumpata kwa kuwa yule aliyefikiri kwamba alikuwa Godwin, hakuwa mwenyewe.
Akaiprinti picha ile, akawa nayo kila alipokuwa akienda. Akaanza kumtafuta mwanaume huyo hapo Tandale. Hakujua kama hiyo ilikuwa picha ya mtandao ambayo ilitolea huko nchini Ghana. Kila siku alipokuwa akilala, aliiweka picha hiyo pembeni yake, alikuwa akiiangalia sura ile na kuikariri na kesho yake alikuwa akiingia mtaani na kuanza kumtafuta.
Ilikuwa kazi ngumu, aliuona ugumu mkubwa mbele yake, hakutaka kukata tamaa, aliendelea kupambana kwa ajili ya kuhakikisha anampata mtu huyo na kumkamata kama ilivyotakiwa kuwa.
Wakati Godwin akiwa ameidukua namba ya Bwana Kom kule Uswisi, pia aliidukua namba ya Halima, kwa maana hiyo Kom alipokuwa akimtumia ujumbe Halima, mtu aliyekuwa akijibu alikuwa Godwin na hata alima alipokuwa akimtumia Bwana Kom ujumbe, mtu aliyekuwa akijibu alikuwa huyohuyo Godwin.
“Umefikia wapi?” aliuliza Kom kupitia ujumbe mfupi wa meseji.
“Bado naendelea kumtafuta, nimejaribu kuwashirikisha baadhi ya watu na wamesema kwamba mtu huyo yupo, si mgeni machoni mwao,” alijibu Godwin na kwa Bwana Kom ilionyesha kama Halima ndiye aliyeituma meseji hiyo.


Rais Bokasa alichanganyikiwa, hakuamini kilichokuwa kikiendelea kwamba hata yule bilionea mkubwa, Bwana Kizota hakuwa akimkubali na alisema wazi kwamba alikuwa akimchukia kwa kuwa yeye ndiye alikuwa mtu aliyechangia kwa Tanzania kuwa kama ilivyokuwa.
Moyo wake ukawa na hasira kali, hakutaka kuchelea, hapohapo akampigia simu IGP Ng’osha na kumwambia kwamba ndani ya dakika kumi tu alitaka kuona bilionea huyo akikamatwa kitu ambacho kilifanyika ndani ya dakika saba tu.
Mambo yalianza kuharibika, hali ya nchi ilianza kusumbua, ilimuumiza kichwa na kuhisi kwamba watu hao walikuwa wakitumiwa na mtu fulani, alihisi kwamba alikuwa Godwin lakini baadaye akaona kwamba kijana huyo asingeweza kuwatumia watu hao, mkurugenzi wa Usalama wa Taifa na Bilionea Kizota, hakika kilikuwa kitu kisichowezekana.
Kwenye mitandao, kila mtu alikuwa akizungumza lake, watu wengi walifurahi kwani hawakumpenda rais huyo hata kidogo. Wakati mwingine watu waliona hiyo miezi miwili mpaka rais huyo kujiuzulu au kupinduliwa ilikuwa mingi mno, kila mmoja alitamani kuona jambo hilo likitokea hata muda huo.
Hakuwa na kimbilio, aliogopa, wakati mwingine aliitwa na marais wenzake wa Afrika kwa lengo la kwenda huko na kupumzisha akili lakini alikataa kabisa kufanya hivyo kwa kuhisi kwamba kama angeondoka nchini basi angeweza kupinduliwa huku nyuma.
“Bado kuna mambo mengi napambana nayo, siwezi kuja huko, nataka nipambane mpaka nitakapoona mwisho wake nini,” alisema Rais Bokasa.
Huo ndiyo ulikuwa ukweli wenyewe, hakutaka kuondoka nchini Tanzania, aliendelea kubaki huku akisimamia msimamo wake kwamba kamwe asingeweza kuondoka kwani kama angefanya hivyo basi huo ndiyo ungekuwa mwisho wa kila kitu.
Alitamani kuwa rais milele, hakutaka kuachia madaraka kwa kuamini kwamba kwa yale yote ambayo aliyafanya, ingetokea siku moja kutoka madarakani basi angeweza kushtakiwa kwa uchafu wote aliokuwa ameufanya katika kipindi chake cha madaraka.
“Ila nini kitatokea kama siku nikipinduliwa kama anavyosema Godwin kwenye mitandao? Inawezekana amewaandaa watu kwa ajili ya kufanya hivi! Nitafanya nini?” alijiuliza huku akiwa chumbani kwake.
Hapo ndipo alipopata wazo kuwasiliana na mtu aliyeitwa kwa jina la Mikel Ludovic, mwanaume aliyekuwa akiishi nchini Urusi ambaye alikuwa miongoni mwa wanajeshi waliokuwa wakitengeneza mabomu ya nyuklia nchini humo.
Akataka kuonana naye, yaani mwanaume huyo asafiri mpaka nchini Tanzania na kuzungumza naye. Hilo halikuwa tatizo, mwanaume huyo akasafiri na kuingia nchini Tanzania kisiri huku watu wakiwa hawajui kama Ludovic alikuwa nchini.
Wakakutana na kuzungumza mambo mengi, alichokuwa akikihitaji rais huyo ni gesi aina ya nitrogen trioxide iliyokuwa na sumu kali. Alimwambia kwamba alitaka aandaliwe sumu hiyo kwa kuwa alikuwa na kazi kubwa alitaka kuifanya.
“Haina shida. Nitakuletea ujazo wa kutosha kabisa,” alisema Ludovic na kuondoka.
Ulikuwa mpango wa siri ambao alikuwa ameuandaa na mwanaume huyo, hakutaka kitu chochote kile kijulikane kwani hata watu wa hapo ikulu walimuona Mzungu huyo akiingia lakini hakukuwa na aliyejua sababu ya mwanaume huyo kufika nchini na kuonana na rais huyo.
“Hakuna mtu atakayeweza kukaa ikulu. Ama zangu ama zao,” alisema Rais Bokasa huku akionekana kudhamiria hasa kuhakikisha anabaki ikulu mpaka kifo chake.
Ludovic alikuwa ndani ya ndege, moyo wake ulikuwa na furaha tele, katika maisha yake, hakukuwa na kitu alichokuwa akikichukia kama watu waliokuwa na ngozi nyeusi. Alikuwa akitengeneza mabomu ya nyuklia huku kila siku akimsisitiza rais wake kwamba kama inawezekana waende Afrika na kuhangamiza bara zima ili weusi wasiendelee kuwepo tena.
Kitendo cha kuitwa na rais huyo na kuambiwa kwamba alitakiwa kusafirisha gesi kwa ajili ya kufanya mauaji hayo, kwake alikuwa na furaha tele, tena wakati mwingine alimshukuru Mungu kwa kuwa alikisikia kilio chake.
“Hiki ndicho nilichokuwa nikikitaka. Ameagiza ujazo wa lita kumi. Mimi nitamtumia ujazo wa tani moja kabisa. Yaani ikiwezekana nchi nzima aiangamize kwa sumu hiyo,” alisema Ludovic huku ndege ikikata mawingu kuelekea Moscow nchini Urusi.


Jenerali Ojuku alikuwa chumbani kwake, kichwa chake kilikuwa na mawazo tele, aliikumbuka familia yake ambayo mpaka kipindi hicho hakujua mahali ilipokuwa. Moyo wake ulijawa na hasira tele, hakuamini kama kweli mwanajeshi yeye, mwenye cheo kikubwa nchini Tanzania ambaye nyuma yake kulikuwa na vikosi vyote vya jeshi alichezewa mchezo kama ule.
Alihuzunika, wakati mwingine alikuwa akisimama na kutembea huku na kule, aliumia moyoni mwake na hakujua ni kitu gani ambacho angefanya ili kuipata familia yake hiyo ambayo kwake ilikuwa kila kitu.
Wakati amekaa hapo, simu yake ya mkononi ambayo ilikuwa mezani ikaanza kuita, hakuifuata na kuipokea, aliiacha iendelee kuita mpaka ilipokata na baadaye kuanza kuita tena. Kwa kuwa ilikuwa ni kelele, akaifuata na kuangalia kioo, hakuiona namba bali maneno yaliyoandikwa ‘Private call’, akaipokea kwani alimjua mpigaji.
“Hallo!” aliita mara baada ya simu kuiweka sikioni.
“Nisikilize kwa makini sana. Leo inaweza kuwa siku yako ya mwisho kwa familia yako kuvuta pumzi ya dunia hii,” alisikika Godwin.
Ojuku akashusha pumzi ndefu, hakukuwa na maneno yalilouchoma moyo wake kama kuambiwa maneno mabaya kuhusu familia yake, akajua kabisa kwamba huyo mwanaume alitaka kufanya kitu fulani, hivyo akabaki akimsikiliza.
“Ninataka ufanye kitu kimoja.”
“Kitu gani mkuu?”
“Uite waandishi wa habari, useme kwamba humuamini rais na hivyo utamtaka aondoke madarakani haraka sana,” alisema Godwin.
“Unasemaje?”
“Una saa tano za kufanya hivyo! Usipofanya, utazikuta maiti za familia yako ufukweni,” alisema Godwin na kukata simu.
“Halo…halo…halo…” aliita Ojuku lakini tayari simu ilikuwa imekatwa.
Hakuamini kile alichokuwa ameambiwa, kwake, aliona mawenge, alichanganyikiwa kupita kawaida kwani katika maisha yake yote hakuamini kama ingetokea siku ambayo angeambiwa maneno kama hayo.
Kwake, familia yake ilikuwa bora zaidi lakini kile alichokuwa ameambiwa kilimchanganya sana kichwa chake. Pale kochini alipokuwa amekaa alipaona kama padogo, akasimama na kuanza kufikiria kwa makini kila neno aliloambiwa.
Hakuwa na jinsi, kama alitaka kuiokoa familia yake alitakiwa kufanya kile alichoambiwa kwani hata alipojifikiria sana, rais huyo hakuwa akipendwa, kila mtu alitamani kuona siku yoyote ile akiondoka madarakani.
Hapohapo akachukua simu na kumpigia Mhariri Mtendaji wa Global Publishers, Saleh Ally na kumwambia kwamba alitaka kuonana na waandishi wa habari kutoka katika Kampuni ya Magazeti ya Global Publishers, baada ya hapo, akavipigia simu vyombo vingine vya habari kwamba alikuwa akitaka kuzungumza nao maneno kuhusu hali iliyokuwa ikiendelea nchini.
Waandishi walipopewa taarifa, haraka sana taarifa hizo zikarushwa katika mitandao ya kijamii ambapo huko kila mtu akabaki na maswali, hali iliyokuwa ikiendelea nchini ilimfurahisha kila mmoja kwani kitu ambacho hawakuwa wakikipenda kuona kikiendelea ni kitendo cha rais huyo kuendelea kuiongoza Tanzania.
“Naye anataka kumkataa rais au?” aliuliza jamaa mmoja.
“Mmh! Kwa Ojuku? Hakuna kitu kama hicho!”
“Sasa kwa nini naye amewaita waandishi wa habari?”
“Labda anataka kuwaeleza kuhusu msimamo wake kwamba jeshi la wananchi litamuunga mkono rais mpaka mwisho,” alisema jamaa mwingine.
“Hebu tusubiri tuone!”
Kila mtu masikio yake yalikuwa huko, watu ambao walikuwa bize na mambo yao, wakaachana nayo na kuanza kusikiliza kile kilichokuwa kikiendelea huko. Mitandao mingi ya habari ikaanza kurusha kila kitu kilichokuwa kikiendelea huko.
Hakukuwa na mtu aliyejua kile kilichokuwa kikiendelea, hata Meja Jenerali naye hakujua kitu chochote kile na hata alipokuwa akimpigia simu mkuu wake kumuuliza kile alichotaka kuzungumza, hakumwambia kitu chochote kile.
Zaidi ya waandishi wa habari themanini walikusanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee kwa ajili ya kusikiliza kile walichokuwa wameitiwa mahali hapo. Baada ya dakika ishirini, magari ya kijeshi yakaanza kuingia mahari hapo na wanajeshi zaidi ya ishirini wakateremka huku wakiwa na bunduki zao kana kwamba walikuwa wakielekea vitani.
Gari alilokuwa Jenerali Ojuku likasimama, mwanaume huyo akasimama na moja kwa moja kuanza kuelekea katika ukumbi huyo huku waandishi wa habari wakimpiga picha mfululizo na wengine wakichukua video.
Alipofika ndani, akaelekea mahali ambapo paliandaliwa kwa ajili yake na kutulia hapo. Hakuzungumza kitu kwanza, akaanza kuwaangalia waandishi waliokuwa ndani ya ukumbu huo ambapo baada ya dakika kadhaa akaanza kuzungumza.
“Najua nyie wote mtakuwa mnafahamu mambo yanayoendelea ndani ya nchi hii! Ni mambo ya ajabu sana ambayo yaliwapelekea watu wengi kuona kwamba Rais Bokasa ananyanyasa watu na kujiona kwamba yeye ni rais wa milele,” alisema Ojuku, akanyamaza kidogo na kuendelea.
“Hili ni jeshi la wananchi, tunapoona mambo hayaendi sawa, chuki ya wananchi inakuwa kubwa, ni lazima tujiulize ni wapi tumekosea. Nimekaa na kujifikiria na mwisho wa siku kugundua kwamba nchi yetu inapotea, watoto na wajukuu zetu wataishi vipi kama sisi wenyewe hatutotengeneza mazingira mazuri kwa ajili yao?” aliuliza Ojuku na kuendelea:
“Jeshi la wananchi limekaa chini na kuamua kitu kimoja tu kwamba hatumuungi mkono Rais Bokasa na hivi ninavyoongea, ninampa saa moja kukusanya kila kitu kilicho chake ikulu na aondoke haraka sana,” alisema Ojuku.
Kitu ambacho hakikutegemewa na mtu yeyote ndani ya ukumbi ule, waandishi wa habari wote wakaanza kupiga makofi huku wengine wakishangilia. Tais huyo hakupendwa, kila mtu alitaka kuona akiondoka haraka sana madarakani kwani aliiharibu nchi na kujifanya mungu mtu ambaye hakusikia la mtu yeyote yule nje ya ikulu.
Ojuku hakuongea sana, alipomaliza akasimama na kuondoka zake huku nyuma akiacha shangwe ambazo hazijawahi kusikika kabla. Kwenye mitandao, kila mtu alikuwa akizungumza lake, hakukuwa na mtu ambaye hakuunga mkono msimamo wa jeshi la wananchi, kila mmoja alipongeza kwa hatua kubwa ambayo jeshi hilo limeliona, haraka sana waandishi wa habari wakaondoka hapo na kuelekea ikulu, walitaka kupiga picha kila kitu kilichokuwa kikiendelea huko, walitaka kumuona rais huyo akiondoka madarakani kwa agizo la Jenerali Ojuku au kama alishindwa, basi jeshi liingie kumtoa kinguvu.


Wiki moja ilipita tangu Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Noel kuamua kujitoa kumuunga mkono. Moyo wake ulikuwa umevurugwa na kitu pekee alichokuwa akikisubiria kipindi hicho kilikuwa ni gesi ya sumu ambayo aliiagiza kutoka nchini Urusi ifike na yeye kufanya kile alichokusudia kufanya.
Hakutaka kuondoka madarakani, alilewa, alitaka kuona akiendelea milele na wakati mwingine alikuwa akijilaumu kwamba kwa nini hakufanya yale ambayo wananchi walitakata kuona akiyafanya, alijiona kuwa mjinga, lakini pamoja na hayo yote, hakutaka kuona akiondoka ikulu pasipo kufanya jambo lolote lile.
Akaendelea kuwasiliana na Ludovick ambaye alimwambia kwamba tayari mzigo wa gesi ya sumu ulitumwa kutoka nchini Urusi kwa kutumia meli na muda wowote ule mzigo ungewasili nchini Tanzania.
“Nimekutumia tani nzima,” alisema Ludovick kwenye simu.
“Nashukuru sana kwa kunijali. Nitakuingizia pesa zako,” alisema Bokasa na kisha kuzihamisha pesa kutoka kwenye akaunti yake na kumtumia Ludovick aliyekuwa nchini Urusi kama malipo yake.
Baada ya siku mbili akawatuma vijana wake kwenda nbandarini ambapo huko wakachukua mitundi minne ya gesi na kwenda nayo ikulu. Hakutaka kumwamini mtu yeyote, alitaka kufanya jambo ambalo aliamini kwamba lingeweka historia nchini Tanzania.
Baada ya siku kadhaa kupita na kusikia kwamba Jenerali Ojuku aliita waandishi wa habari kwa ajili ya kuzungumza nao, alijua kabisa kwamba naye alikuwa akienda kwa ajili ya kumkataa kwani kama angekuwa mtu wake, angempigia simu na kumwambia kile ambacho alikuwa njiani kuwaambia waandishi wa habari.
Alifungulia redio na kusikiliza kila kitu na familia yake. Moyo wake ulimuuma kupita kawaida, akaona kwamba alibaki yeye peke yake hivyo alitakiwa kupambana yeye kama yeye. Aliposikia kwamba alipewa saa moja tu kwa ajili ya kuondoka, akaiambia familia yake kwamba walitakiwa kuelekea nje ambapo wangechukua gari na kuondoka zao kwenda uwanja wa ndege.
“Na wewe?” aliuliza mkewe.
“Nitakuja tu! Nitakimbia Kenya. Nyie nendeni kwanza,” alisema Bokasa na familia yake kuondoka.
Ikulu nzima alibaki peke yake, alikuwa akijifikiria namna ya kuanza. Akachukua mitudi ile ya gesi na kuanza kunyunyizia katika kila chumba, alitaka kumuua mtu yeyote ambaye angeingia ndani ya jumba hilo kubwa. Alipulizia kwenye kila chumba na alipomaliza, akachukua simu yake, akaenda kwenye akaunti ya serikali na kuhamisha pesa zote zaidi ya dola trilioni kumi na kuzipeleka katika akaunti yake ya siri nchini Ubelgiji.
“Yeyote atakayeingia, hakika atakufa,” alisema Bokasa, akatoka nje ambapo akachukua gari, likampeleka ufukweni kisiri, akapanda boti na kuanza safari ya kuelekea Mombasa huku akiwa ameacha sumu ya kutosha ndani ya jumba lile.
Baada ya saa moja kutimia, Jenerali Ojuku akawaambia wanajeshi wake kwenda ikulu na kuvamia ili hata kama rais huyo alikuwa ndani ya jumba hilo basi waweze kumchukua na kuondoka naye.
Hiyo ilikuwa ni amri ambayo moja kwa moja ikapokelewa na wanajeshi hao na kuanza kuelekea huko. Walipofika, wanajeshi ishirini wakaanza kuingia ndani huku wengine wakibaki nje.
Wakaingia ndani mpaka sebuleni ambapo hapo wakaanza kuelekea kwenye vyumba vingine. Walipoanza kufungua tu, wanajeshi hao wakaanza kuanguka kama mizigo, gesi kali yenye sumu ikawapata na hivyo kuwapukutisha kama kuku.

Je, nini kitaendelea?

wanakuja wenyeji

Endelea kutupia, watazikuta…

Jackal2 asante sana
@Shunie ukuje huku maa

Cc: @Mahondaw

Mkuu bora umerudi.

Leta nyingine

Goma ndo linaanza smart ???!!

Hii na ile ya kule home ni moja?? Au heading tofaut, saa hizi tungekua jf @Smart911 angesakamwa ana reply paragraph yote

Wale wasema chochote na wakuwasakama wenzao ili kupata cheap popularity wa kule Tanzania naona humu bado hawajafika…

Au na wewe unaniambia indirect @Madame S

Cc: @Mahondaw

Lipo mwisho mwisho @Mahondaw wangu…

Jamani nimefurahi kuwaona tena huku, jtatu nitaingia kwa ID yangu ya home…tangu tumefungiwa nimeshahangaika hadi basi, roho mtakatifu kaniongoza hatimae nimeipata JF, its me ram

Huu ni mwendelezo wa kile kilichokuwa kinaendelea kule JF halisi.Ukitaka mwanzo mpaka mwisho ,itabidi nikutumie WhatsApp mkuu@Mahondaw

Kumbe Smart911 na mahondaw ni jinsia tofauti?Sasa ipi ni KE na ipi ni ME?

Hapana kaka angu wallah was jokin maana forum ya huku iko vizuri sana

Mkuu ingependeza kama tungetumia majina ya Kule JF.

Asante babe hivi iliendelea ilipoishia au mbona naona kama page moja imerukwa

Cc: @Mahondaw

Usiogope Dada yangu… najua you are joking… nasemea wale wenye hizo…

Cc: @Mahondaw

Salama Shunie?
Hakuna sehemu iliyorukwa!

Woyoooo kitu kinazidi kuwa kutamu, Shanie uko wapi mamaa nimekumiss balaa